Dereva basi la Zuberi mbaroni ajali iliyojeruhi wawili Mwanza

Gari la abiria aina ya Toyota Hiace linalofanya safari zake Ngudu-Nyashishi mkoani Mwanza likiwa limedondoka baada ya kugongwa na Bus la Kampuni ya Zuberi jana usiku katika eneo la Mawe matatu kata ya Usagara wilayani Misungwi.

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa ametaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni uzembe uliosababishwa na dereva huyo baada ya kujaribu kulipita gari dogo lililokuwa mbele bila kuchukua tahadhari.

Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, linamshikilia dereva wa basi la Zuberi, Noel Lushanga (34) kwa kosa la kusababisha ajali baada ya basi hilo kugonga basi dogo aina ya Toyota Hiace na kusababisha majeruhi wawili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amewaambia waandishi wa habari Mei 2, 2024, kuwa chanzo cha ajali hiyo kuwa ni uzembe wa dereva huyo aliyelipita gari la mbele yake bila tahadhari.

“Mei Mosi, 2024, saa 2:40 usiku katika barabara ya Mwanza–Shinyanga, eneo la Mawe Matatu gari lenye namba za usajili T669 DEE, aina ya Higher Bus likitokea Mwanza kueleka Dar es Salaam ikiendeshwa na Noel Lushanga, akiwa analipita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari aligongana na gari lenye namba za usajili T858 DHE aina ya Toyota Hiace inayofanya safari yake Ngudu – Nyashishi ikiendeshwa na Isaka Bakari (32), mkazi wa Buhongwa na kusababisha majeruhi wawili waliokuwa ndani ya Hiace,” amesema.

Amewataja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Elias David (33), mkazi wa Igoma ambaye alipata majeraha upande wa usoni na mwingine ni Yazidi Swahibu (44), mkazi wa Isamilo ambaye pia alipata majeraha usoni na wote walipelekwa hospitali ya wilaya ya Misungwi kisha Hospitali ya mkoa ya Sekou Toure kwa matibabu zaidi.