Prime
Dk Biteko azitega Tanesco, Ewura
Muktasari:
- Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewataka watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kufanya kazi kama timu moja huku akiagiza bodi ya mamlaka hiyo kuwachukulia hatua watumishi wasio waaminifu.
Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewataka watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kufanya kazi kama timu moja huku akiagiza bodi ya mamlaka hiyo kuwachukulia hatua watumishi wasio waaminifu.
Alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alizungumza na wafanyakazi wa Ewura ikiwa ni siku moja imepita tangu alivyofanya kikao kama hicho na watumishi na menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kutoa maagizo kama hayo kwa watumishi sambamba na kuondoa makundi.
Alisema uhalali wa wafanyakazi wote waliopo sasa pamoja na viongozi wake akiwamo yeye ambaye pia ni Waziri wa Nishati uko rehani endapo Watanzania hawatakuwa na uhakika wa nishati hiyo.
Awali Dk Biteko aliwataka watumishi wa Tanesco kufanya kazi kwa kujituma, kuepuka majungu na makundi badala ya kuingia kwenye mitego ya kuwa kikwazo cha ukuaji wa huduma za nishati kabla ya kuondolewa na kusisitiza: “Watanzania wanataka umeme na si vinginevyo.”
Jana, ilikuwa zamu ya Ewura ambapo Dk Biteko alisema lengo la ziara yake hiyo ni kujifunza kuona mipango yao na kusikiliza ili kuona namna ya kwenda sambamba na maono ya Rais ambaye anataka Watanzania wapate nishati nafuu, ya uhakika na wakati wote huku udhibiti ukifanywa kwa maslahi ya Watanzania.
Alieleza mkakati wa Serikali kukabiliana na changamoto za upatikanaji na bei ya mafuta, huku akigusia gesi kama nyenzo ya muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara hiyo, alisema baadhi ya watumishi wa mamalaka hiyo sio waaminifu kiasi cha kuleta changamoto katika sekta ndogo ya mafuta.
Alisema Ewura ni taasisi ambayo ni jicho la wananchi kwenye kudhibiti masuala ya umeme, mafuta, gesi asilia na maji, ikilegalega Watanzania wataumia sana lakini ikiwa na nguvu Watanzania watapata nafuu sana ya maisha.
Alisema ameipa malekezo taasisi hiyo kufanya kazi kama timu moja na migawanyiko ya huyu ni wa nani haitakiwi kufikiriwa hata kidogo katika taasisi kubwa kama hiyo.
"Lazima watu wawe kitaaluma kwa mujibu wa taratibu na kwa mujibu wa sheria. Zipo taarifa vilevile tumezipitia za watu wachache wasio waaminifu ndani ya mamlaka ambao wanajihusisha na vitendo vidogo vidogo wanatoa siri kwa maeneo ambayo tunataka kufanya operesheni,’’ alisema na kuongeza;
Unakuta kuna changamoto ya mafuta tunaenda kukagua unakuta watu tayari wana taarifa wamefunga hawapo kwa sababu ndani ya Ewura kuna watu wana taarifa hizo wanazitoa, hivyo kazi inakuwa ngumu.’’
Watumishi
Alisema kutokana na hilo wameamua kwa pamoja kufanya mageuzi makubwa ya kupitia rasilimali watu ili kujiridhisha na kubaki tu na wale ambao ni waaminifu katika kazi na ambao sio waaminifu wafundishwe namna ya kuwa waaminifu kwasababu nyenzo za kuwafundisha zipo.
Alisema suala hilo amelielekeza kwa bodi kuangalia na kupitia upya kuangalia ni wapi kuna matatizo.
Uhaba wa mafuta
Kuhusu changamoto ya mafuta alisema zipo sababu zilizo nje ya Tanzania ambazo zinaweza kuwa bei ya mafuta kupanda, kukosekana kwa dola au gharama kubwa za uletaji wa mafuta Hata hivyo, alisema zipo ambazo zinapaswa kuangaliwa kwanda ndani kama nchi.
"Tukiziangalia hizo zitatusaidia kupunguza mzigo kwa wananchi, mahali ambapo tunadhani kuna vitu bei zake zimekuwa kubwa sana ni kazi ya Ewura kuzipitia, kufanya utafiti na kujiridhisha kama viwango vinavyotozwa ni halisi, tutapitia upya kuona kama gharama ya uagizaji ni halisi ili Watanzania wapate nishati hiyo kwa bei halisi.
Alisema haimaanishi Serikali inataka kupunguza bei au kufanya chochote, kinachotakiwa ni kupitia kujiridhisha na uhalisia.
"Kama tumeambiwa bei ya kuleta mafuta ni Dola 200 kweli ni 200 na kama sio 200 kwanini ilikuwa inapandishwa? alihoji.
Alieleza menejimenti ya Ewura kuwa suala la upangaji bei linawapa simanzi Watanzania hasa mafuta kuadimika pindi bei inapokuwa inabadilika na baada ya bei mpya yanapatikana, akisema huo ni mchezo ambao Watanzania hawapendi kuuona.
"Lazima wafanyabiashara wajue kuwa kupewa leseni lengo lako ni kupata faida na kukuza mtaji lakini hudumia Watanzania ili shughuli za kiuchumi zizitatizike, zikitatizika hutapata hata watu wa kununua hayo mafuta, akishafunga kiwanda chake atakuwa hana hela," alisema.
Alisema kuficha mafuta ni kujihujumu mwenyewe kwani nguvu ya manunuzi manunuzi ikiathirika hawatanunua tena hivyo aliwakumbusha wafanyabiashara wajibu wa kuwahudumia Watanzania kwa uaminifu.
Aliongeza Serikali imejipanga kudhibiti changamoto zote za mafuta ili kuhakikisha maumivu ya changamoto ya nishati hayawapati na kama yapo yanapunguzwa kwa kiwango kikubwa.
Aidha alisema kuna shida ya mafuta yanayotokana na kupungua kwa uzalishaji huku mahitaji yake yakiongezeka kwakuwa shughuli za uchumi zinaongezeka duniani hivyo lazima kufikiri kimkakati ili kumaliza changamoto hiyo ikizingatiwa kuwa nishati hiyo haizalishwi hapa nchini.
"Mkakati wa kukabiliana na changamoto hiyo ni matumizi ya gesi asilia (CNG) kwenye magari, Ewura hakikisheni magari yanayotumia nishati hiyo na vituo vya kujazia mafuta vinaongezeka ili tuhame kwenye kutumia mafuta na hilo linawezekana kama wote kama Serikali tutakubali," aliesema Dk Biteko.
Alisema wakati viongozi wakiwaambia wananchi watumie CNG ni vyema kuanza na magari ya Serikali ambayo yanaweza kubadilishwa hivyo kupunguza uhitaji wa mafuta jambo ambalo linapunghza hata mzigo wa kuagiza mafuta.
"Huo ni mkakati wa muda mrefu ambao Ewura lazima muuchukue kwa kasi kubwa kwa namna ambayo itatupa matokeo ya haraka kwa manufaa makubwa ya kukuza uchumi wa nchi," alisema Biteko.