Dk Chegeni: Lowassa angeweza kuishi zaidi kama si ajali za kisiasa

Dk Chegeni akizungumza leo wakati wa ibada ya kumuaga aliyewahi kuwa waziri mkuu, Edward Lowassa iliyofanyika usharika wa Azania Front, jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Mbunge wa zamani wa Busega (CCM), Dk Rafael Chegeni amemzungumza Edward Lowassa alivyokuwa anapendwa na Watanzania mbali na jinsi ambavyo angeweza kuishi zaidi, kama asingepata ajali mbalimbali za kisiasa.
Dar es Salaam. Mbunge wa zamani wa Busega (CCM), Dk Rafael Chegeni amesema isingekuwa ajali mbalimbali za kisiasa alizopitia Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Lowassa huenda leo angekuwa hai.
Chegeni ambaye alikuwa mshirika wa karibu wa Lowassa (70) amesema mwanasiasa huyo amekutana na ajali mbalimbali za kisiasa ambazo nyingine alizipata kwa kubeba mzigo usio wake.

Dk Chegeni akiwa na hayati Lowassa enzi za uhai wake. Picha na mtandao
Akitoa salamu zake wakati wa ibada inayofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Azania Front jijini Dar es Salaam, Dk Chegeni amemtaja Lowassa kuwa ni miongoni mwa viongozi wachache wenye hekima ya kubeba mizigo ya wengine.
“Huyu baba nilikutana naye bungeni mwaka 2001 akiwa waziri, 2005 aliteuliwa kuwa waziri mkuu alifanya makubwa na hata baada ya kupata ajali ya kisiasa alibeba mzigo usio wake na kuamua kujiuzulu. Ni miongoni mwa viongozi wachache wenye hekima kama aliyokuwa nayo Lowassa.”
“Mwaka 2015 tulianza safari ya matumaini, safari ambayo kweli kila tulipokwenda Watanzania walimuamini sana Lowassa kwa sababu ndiye kiongozi waliamini atawaletea mabadiliko, ameacha alama katika mioyo ya Watanzania,” amesema Dk Chegeni.
Mwanasiasa huyo pia amempongeza Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba aliyepo kanisani hapo kwa namna alivyozungumza ukweli kuhusu Lowassa.
“Nakushukuru Warioba kwa kuzungumza kilichojaa moyoni, hukuongea kama wanasiasa tumejaa lugha tofauti. Wazee kama nyie tunawahitaji kwa kuwa tunataka kujenga Taifa la wanaosema ukweli na wanaosema haki,” amesema Dk Chegeni na kuongeza:
“Ninafahamu wala sio siri…miaka 70 au 80 ya binadamu lakini ninaamini Edward Lowassa, angeweza kuishi zaidi kama sio ajali mbalimbali za kisiasa.”
Ajali anayozungumza Dk Chegeni kuhusu Lowassa ni ya Februari 7, 2008 ambapo mwanasiasa huyo aliamua kutangaza kujiuzulu nafasi ya waziri mkuu, akiwa ndani ya Bunge kutokana na kashfa ya Richmond.
Lowassa alichukua uamuzi huo kutokana na tatizo kubwa la uhaba wa umeme na Serikali kulazimika kutafuta njia za dharura za kutatua tatizo hilo, zikiwamo zilizodaiwa kukiuka taratibu na sheria.
Baada ya kashfa hiyo kuchunguzwa na taarifa kutolewa bungeni, Lowassa alilazimika kujiuzulu baada ya kutakiwa ajipime kutokana na mazingira ya kashfa hiyo.
Wengine waliong’oka madarakani ni mawaziri wa Nishati na Madini kwa vipindi tofauti, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha.
Katika mbio za urais ndani ya CCM mwaka 2015, Lowassa alikuwa miongoni mwa Wana-CCM 38 waliojitosa kuchukua fomu. hata hivyo, jina lake lilikatwa na Julai 28, 2015 aliamua kujiunga na Chadema ambapo alipitishwa kuwania urais.
Hakuwa peke yake, watu walimuunga mkono akiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Fredreck Sumaye naye alijiunga na Chadema. Mawaziri, naibu mawaziri, wenyeviti wa CCM waliungana naye kushiriki vyema kwenye uchaguzi huo.
Nguvu ya Lowassa ilionekana katika uchaguzi mkuu huo kwani licha ya kushindwa na kushika nafasi ya pili nyuma ya hayati John Magufuli wa CCM aliyeibua mshindi, ushawishi wake uliwezesha upinzani kupata wabunge, madiwani wengi na kuongoza halmashauri zaidi ya 20.
Hata hivyo, Machi 1, 2019, Lowassa alitangaza kurejea tena CCM.
Katika salamu za rambirambi kanisani hapo, Mbunge wa zamani wa Kawe (CCM), Ritha Mlaki amesema msiba wa Lowassa ni mkubwa kwa kuwa Taifa limempoteza kiongozi mahiri.

Ritha Mlaki akizungumza katika ibada ya kumuaga Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa.
“Nimemfahamu Lowassa kwa miaka 48 tangu mwaka 1976 tukiwa Chuo Kikuu, wazazi wetu walikuwa marafiki huko Monduli. Tumefanya kazi pamoja serikalini, kwenye siasa na tumesali pamoja usharika wa Azania Front,” amesema Ritha na kuongeza:
“Lowassa alikuwa mtu muwazi, hakupenda kuweka kitu rohoni, mambo ya kupinda pinda na ukifanya hivyo atakwambia ukweli. Kwa muda wote niliokuwa naye alikuwa mchapakazi mahiri, mtu safi, aliongea haraka na sauti yake ilijaa mamlaka,” amesema Ritha.
Ujasiri wa Mama Regina Lowassa
Ni mama jasiri, hivi ndiyo anavyoweza kuelezewa mjane wa Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, Regina Lowassa.

Mke wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Regina Lowassa akiwasili kanisani kwa ajili ya kushiriki ibada ya kuuaga mwili wa mwanasiasa huyo. Picha na Loveness Bernard
Ujasiri na ukakamavu wa mama huyu umeonekana alipowasili kanisani katika ibada ya kumuaga Lowassa inayofanyika katika usharika wa Azania Front.
Akiwa ameambatana na wanafamilia wengine, Regina alishuka kwenye gari, mwenyewe na kuzungumza na watu wachache waliomkaribia kisha akaanza kutembea kuingia kanisani.
Akishuhudia wajukuu zake wakisukuma toroli lililobeba jeneza lenye mwili wa mwenza wake, Regina aliendelea kuimba wimbo uliokuwa ukiimbwa na kwaya kuu ya kanisa hilo.

Hata ibada ilipoanza, mama huyu alionekana akiimba kwa ujasiri wimbo maarufu wa Kikristo ‘Bwana U sehemu yangu’ akiwa mbele ya jeneza la mumewe. Kiimani Regina ni Mkatoliki.
Wakati ibada hiyo ikiendelea viongozi mbalimbali wameendelea kuwasili akiwemo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi.
Atembea na vitabu vya dini
Mzee Ramadhani Mapande (80) ni miongoni mwa watu waliohudhuria katika ibada hiyo kwa upekee akibeba vitabu vya dini ya Kiislamu pamoja na begi lililojaa nguo za kubadilisha.

Mzee Ramadhani Mapande, akiwa anamuombea hayati Lowassa kwa kutumia vitabu vya dini ya Kiislamu.
Mzee huyo amesema tangu jana Jumanne, mzee huyo alikuwa na vitu vyake hivyo maalumu vya kumuombea Lowassa.
"Nafanya ibada kumuombea Lowassa, ninazo nguo za kubadilisha kwenye begi na vitabu vyangu vya dini, nilimpenda Lowassa alikuwa na msimamo na aliipenda nchi iwe na amani na elimu ndio maana alisisitiza elimu, elimu elimu," amesema mzee huyo akizungumza na Mwananchi Digital kanisani hapo
Ramadhan amesema Lowassa ni miongoni mwa viongozi ambao aliwapenda kutokana na kutokuwa na kinyongo na alihimiza amani.