Dk Mwaikali, baadhi ya waumini wajitenga

aliyekuwa askofu wa Dayosisi ya Konde ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Edward Mwaikali

Muktasari:

Waumini watangaza mwelekeo mpya wakihamia Kanisa la Kiinjili la Afrika Mashariki

Moshi. Wiki moja baada ya kuvuliwa madaraka, aliyekuwa askofu wa Dayosisi ya Konde ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Edward Mwaikali na baadhi ya wachungaji na waumini wamejitenga na kanisa hilo.

Uamuzi huo ulitangazwa jana katika Kanisa Kuu la Ruanda jijini Mbeya na Dk Mwaikali aliyesema yeye, wachungaji na waumini wanaomuunga mkono sasa watakuwa wanaabudu katika Kanisa la Kiinjili Afrika Mashariki (KKAM).

KKAM lilianzishwa mwaka 1999 na kupata usajili mwaka 2005 na tayari limepanuka na kusambaa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Manyara, Singida, Tabora, Shinyanga, Dar es Salaam na lipo katika hatua za mwisho kuanzisha tawi mkoani Mwanza.

Jumapili ya Juni 5, KKKT Dayosisi ya Konde ilitangaza kumvua uaskofu Dk Mwaikali na liliviondolea wakfu vifaa vya uaskofu ambavyo ni pete, msalaba, fimbo na mavazi ambayo bado anayo askofu huyo.

Uamuzi huo umetokana na mgogoro uliodumu katika dayosisi hiyo kwa muda mrefu ambapo wajumbe wa mkutano mkuu maalum uliofanyika Aprili walipiga kura ya kumwondoa madarakani na kumchagua Geofrey Mwakihaba kuirithi nafasi yake.

Hata hivyo, wiki moja tu baada ya kuondolewa, Dk Mwaikali jana alitangaza kujiunga KKAM, kanisa lililoasisiwa na Askofu Mkuu Jesse Angowi aliyewahi kuwa kingozi wa KKKT.

Bado haijawekwa wazi Dk Mwaikali, wachungaji wake na waumini waliotangaza kuondoka naye watatumia majengo gani kuendesha ibada kwa kuwa tayari mkuu wa KKKT, Askofu Fredrick Shoo alionya wasizitumie rasilimali za kanisa hilo.


Alichokisema Dk Mwaikali

Akizungumza ndani ya Kanisa Kuu la KKKT Ruanda jana, Dk Mwaikali alisema tayari KKAM walishawaandikia barua ya kuwapokea na walishawatumia cheti cha usajili wa kanisa.

“Hawa ndugu zetu wa Kanisa la Kiinjili la Afrika Mashariki tayari walishatuandikia barua ya kutupokea na wametutumia cheti cha usajili,” alisema Dk Mwaikali ambaye anakubalika kwa baadhi ya washarika wa Dayosisi ya Konde.

“Na sisi kwa uamuzi wa kura zenu natangaza rasmi kwamba na sisi tutakwenda kwenye mwavuli huo. Kama nilivyowatangazia kwamba siku ya utambulisho rasmi tutawaalika maaskofu wa kanisa hilo waje,” alisema Dk Mwaikali.

Mchungaji Nyibuko Mwambola aliwatoa hofu waumini wanaohamia KKAM kuwa Dk Mwaikali hakushindwa kesi bali mahakama iliwataka wapatane hivyo wapo kwenye utaratibu huo.

“Kama mahakama imesema mkapatane si Serikali wala polisi wanaoweza kuingilia. Tujitahidi sana kutunza amani. Sisi ni wachungaji tukitoka huko nje ni wananchi tuna haki ya kusema na asiwepo wa kunyanyaswa,” alisema Dk Mwambola.

Mmoja wa waumini, Baraka Mwasambamba alisema wamefurahi kuhamia KKAM na popote atakapokuwapo Dk Mwaikali watakuwa upande wake.

“Mzazi akikuambia sikutambui unatafuta namna ya kujisitiri ili maisha yaendelee. Huu mgogoro umetutesa sana na unatuumiza vichwa,”alisema.