Dk Mwele: Wataalamu fanyeni kazi bila woga

Dk Mwele: Wataalamu fanyeni kazi bila woga

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa Magonjwa ya Kitropiki kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Mwele Mal[1]ecela amesema wataalamu wa sekta mbalimbali wafanye kazi na kuzingatia weledi bila woga.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Magonjwa ya Kitropiki kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Mwele Malecela amesema wataalamu wa sekta mbalimbali wafanye kazi na kuzingatia weledi bila woga.

Dk Mwele pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua anazochukua kupambana na corona. Dk Mwele, anayefanya kazi makao makuu ya WHO jijini Geneva Uswisi, amesema wataalamu waachwe wafanye kazi yao kwa weledi ili kupata matokeo chanya dhidi ya ugonjwa huo unaoenea kwa kasi duniani.

 Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi kupitia mtandao, Dk Mwele, anayeshughulikia magonjwa ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele (NTD), alisema anaipongeza pia tume iliyoundwa na Rais kwa kazi nzuri na mapendekezo muhimu waliyotoa.

Kauli hiyo ya Dk Mwele inakuja hivi sasa wakati baadhi ya wataalamu wamepata misukosuko, ikiwemo ya kuondolewa kwenye nyadhifa zao au kufukuzwa kazi wakati wakitekeleza majukumu yao, akiwemo yeye (Dk Mwele) aliyetumbuliwa katika nafasi ya Ukurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa magonjwa ya binadamu Tanzania (NIMR).

 Dk Mwele alifikwa na mkasa huo Desemba 17, 2016 mara baada ya kutangaza kugunduliwa kwa virusi vya Zika hapa nchini. Mei 5, 2020 Mkurugenzi wa Maabara ya Afya Tanzania, Dk Nyambura Moremi alisimamishwa kazi baada ya aliyekuwa Rais, John Magufuli kupe[1]wa majibu ya vipimo vya corona yaliyoonyesha kuwa mapapai na mbuzi yana virusi hivyo.

Wakati Dk. Mwele akiwataka wataalamu waachwe wafanye kazi yao bila woga, mpaka sasa Tanzania haijatoa takwimu za idadi ya vifo na waliougcorona tangu ifanye hivyo Mei 7, 2020 ilipotangaza kuwa na wagonjwa 509 na vifo 21.

Hata hivyo, Februari 17, mwaka huu lilipozuka wimbi la pili lililotajwa kuwa ni ugonjwa wa changamoto ya mfumo wa upumuaji, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kupitia Rais wa chama hicho, Dk Shadrack Mwaibambe kilitoa tamko la kutaka wataalamu wa sekta ya afya wakingwe kwa kupewa vifaa vya kujikinga na corona wakati waki[1]wahudumia wagonjwa.

Hata hivyo, katika uongozi wa awamu ya sita, Rais Samia amejipambanua na kutaka sayansi ichukue nafasi yake baada ya Aprili 6, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwaapi[1]sha makatibu wakuu na manaibu wao, kusema ataunda kamati ya wataalamu watakaochambua kwa kina ugonjwa wa Covid-19 na kuishauri Serikali jam[1]bo la kufanya.

“Katika kipindi hiki cha corona tumeona kuwa nchi zilizotoa kipaumbele kwa ushauri wa wataalamu wamekuwa na mafanikio makubwa katika kupambana na ugonjwa huu. Nimependa sana jinsi Tume ilivyosisitiza masuala ya maadili katika utendaji wakati tunapopambana na ugonjwa huu,” alisema Dk Mwele.

Dk Mwele, ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu nchini Tanzania (NIMR), amesema wataalamu wanapambana na wakati mgumu kutokana na habari potofu zinazohusu kupambana na ugonjwa wenyewe.

“Bahati mbaya wakati tunapopambana na corona inabidi kupambana na mlipuko wa habari potofu na moja ya maeneo yanayoongelewa habari poto[1]fu ni chanjo,” alisema.

Alisema Tanzania ina wataalamu wazuri katika kupambana na magonjwa ya milipuko na wengi wana shahada za uzamili katika epidemiolojia kupitia mpango unaoitwa ‘Field Epidemiology and Laboratory Training Network’, hivyo ni vyema wakaachwa wafanye kazi. “Cha muhimu wapewe nafasi ya kushauri bila woga, wakati huo huo nao wawe tayari kufanya kazi kwa weledi na maadili,” alisisitiza Dk Mwele.

Alisema anakubaliana na ushauri wa tume kuhusu chanjo, kwani zinasiadia kinga dhidi ya corona na kwa ujumla ni salama. Dk Mwele alisema ni muhimu chanjo iwe sehemu ya afua za kupambana na corona na anaafiki kuwa zitolewe kwa hiari lakini ziwepo.

“Mpango wa Shirika la Afya Duniani wa Covax utatuwezesha kupata chanjo hizo.” Alisema tume iliyoundwa na Rais imegusia kila eneo muhimu katika mapendekezo na anaamini yakifuatwa nchi itafika mbali.