Dk Nchimbi apokea kero Nyasa

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi akitazama  kikundi cha ngoma ya asili ya  Nyasa kikitumbuiza kwa lengo la kumpokea baada ya kuwasili kijijini Mbaha mkoani Ruvuma.

Muktasari:

  •  Dk Nchimbi amewaambia wakazi wa Nyasa kuwa ameona si vema kutowasalimia kisha akawataka wenye kero kuzisema ili zipatiwe ufumbuzi

Nyasa. Wakazi wa Kata ya Mbaha wilayani Nyasa Mkoa wa Ruvuma wamempa kero nne Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ikiwamo ubovu wa barabara ya kutoka Ruanda- Lituhi na  Ndumbi hadi Mbamba Bay.

Kero nyingine ni fidia kwa wananchi, umeme, ukosefu wa kituo cha afya na upatikanaji wa majisafi na salama.

Wametoa kero hizo jana Jumapili Aprili 21, 2024  wakati Dk Nchimbi aliposimama kuwasalimia wakazi wa Mbaha waliokuwa wana shauku ya kumuona baada ya kushika wadhifa huo.

Katika msafara huo, Dk Nchimbi aliyekuwa akielekea Mbamba Bay aliambatana na wajumbe mbalimbali wa kamati kuu

Kabla ya kutoa kero hizo, Dk Nchimbi aliwaambia wakazi hao kuwa ameona si vema kutowasalimia kisha akawataka wenye kero kuzisema ili zipatiwe ufumbuzi.

Mmoja wa wakazi hao, Joachim Mpangala amesema kuna changamoto katika eneo la Ndumbi kuhusu kipande cha barabara kinachotarajiwa kujenga huku watu 51 wanaomiliki nyumba hawajathaminishiwa kwa ajili ya fidia.

" Tunakuomba katibu mkuu tupo chini ya miguu yako uzione nyumba hizo ili kufanyiwa uthamini," amesema Mpangala.

Mwingine ni Ado Alex alimuomba Dk Nchimbi kuwasaidia ujenzi wa barabara kutoka Lituhi hadi Mbambay Bay na kituo cha afya akisema Mbaha kuna zanahati mbili pekee.

Alex amesema kituo cha afya ni muhimu kwa watu wa rika zote ili kupata huduma za matibabu.

"Wananchi wakipata changamoto ya afya wanalazimika kupelekwa Ruanda, sasa wakati mwingine wanajikuta wanapoteza maisha njiani,” amesema Alex.

"Jambo jingine ni maji bado changamoto tunaomba utusaidie, pia umeme licha ya Serikali kutenga fedha za huduma hii," amesema Alex.

Baada ya maelezo hayo ya wananchi Dk Nchimbi aliwaita watendaji wa sekta zilizoguswa kwa ajili ya kutoa majibu kwa wanaMbaha.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Ruvuma, Mhandisi Salehe Juma amekiri wananchi hao kuandika barua na kuziwasilisha katika ofisi na  kutofanyiwa utathimini kwa ajili ya malipo ya fidia.

"Kulikuwa na taarifa ambazo ofisini kwetu, kwamba barabara ya zamani ilipita pale ambapo Tanroads hatukupita, kwa maana hiyo wale watu walifuatwa na barabara, hivyo tumepokea changamoto hii watafanyiwa uthamini upya na kulipwa hakuna atakayedhulumiwa, " amesema Juma.

Kuhusu ubovu wa barabara, amesema ujenzi umeshaanza na kwamba kutoka Ruanda hadi Ndumbi mkataba umeshasainiwa Machi mwaka huu na wakati wowote utaanza kazi.

"Sasa kipande cha kutoka Ndumbi hadi Mbamba Bay uthamini umeshafanyika na tunaendelea kuomba fedha ujenzi uanze ili kuunganisha barabara hii hadi Mbamba Bay," amesema Mhandisi Juma.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira  Vijijini (Ruwasa) Ruvuma, Rebman Nganshonga amekiri eneo hilo kuwa na changamoto ya maji, lakini Serikali imeshaanza hatua ya kuitatua suala hilo ikiwamo kutandaza mabomba.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Nyasa, Khalid Khalifa amesema wameichukua changamoto ya kituo cha afya kwa ajili ya kuifanyia tathimini na kuiweka katika mpango wa bajeti ili iwezwe kutekelezwa kwa siku za usoni.

Kuhusu umeme, mbunge wa Nyasa, Stella Manyanya amesema awamu iliyopo ni kupeleka huduma hiyo kila kijiji.

"Mara ya mwisho tuliahidiwa vitongoji 15 lakini hatujabahatika katibu mkuu, naungana na wananchi fedha zinazotengwa ni kidogo lakini mahitaji ni makubwa," amesema Manyanya.

Baada ya majibu hayo, Dk Nchimbi amesema ataongeza msukumo katika kutekelezwa kwa changamoto hizo hasa upatikanaji wa kituo cha afya akisisitiza kitakuwa kipaumbele chake.