DRC, Tanzania zazindua kituo kupima madini bandarini

Muktasari:

 Nchi za Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimeanzisha kituo cha pamoja katika Bandari ya Dar es Salaam cha kupima na kuthibitisha madini ya shaba kutoka DRC ili kuthibiti utoroshaji

Dar es Salaam. Kituo maalumu cha kupima na kuthibitisha madini kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kimeanzishwa  katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuthibiti utoroshaji wa madini ya shaba.

Hatua hiyo ya ushirikiano baina ya Tanzania na DRC kinakwenda kumaliza tatizo la wizi wa madini hayo ambayo umekuwa ukitokea na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara na Serikali za nchi hizo mbili.

Kituo hicho kidogo cha biashara za madini, kipo chini ya ofisi ya Mamlaka ya Tathmini na Uthibitishaji wa Utaalamu (CEEC) ya nchi hiyo, kitathibitisha madini yote kutoka DRC yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam.

 Hatua hiyo itasadia kuongeza imani kwa wawekezaji na hatimaye kuzinufaisha nchi zote mbili.

Ripoti kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa inamiliki asilimia 68 ya soko la shehena ya DRC inayopitia bandari nyingine shindani, jambo linalomaanisha wawekezaji bado wana imani na wako tayari kutumia miundombinu vya bandari hiyo.

Akizungumza baada ya uzinduzi wa kituo hicho cha biashara leo Jumatatu, Machi 25, 2024, jijini Dar es Salaam, Mwambata wa Kibiashara kutoka Ubalozi DRC nchini Tanzania, Kasongo Yampanya amesema kwa muda mrefu nchi hiyo ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya wizi wa bidhaa za madini hasa shaba.

“Tunashukuru Serikali za nchi zote mbili kwa kuungana na kukubali kuanzisha kituo hiki. Itahakikisha bidhaa zote za madini zinafika kwenye nchi husika bila vizuizi.

Wafanyabiashara wetu wamekuwa wakipata hasara kubwa wakati mwingine, hata zinaweza kuisha muda wake wakati usafirishwaji ikiwa gari litaharibika, na kufanya shehena hiyo isitambulike na kuwa hatarini kutaifishwa,“ amesema.

Yampanya amesema kutokana na kutokuwepo kwa ukaguzi wa kutosha wa madini nchini Tanzania, baadhi ya wafanyabiashara hutumia njia zisizo halali za kusafirisha madini na kutengeneza nyaraka feki, hivyo wawekezaji kupata hasara kutokana na mizigo yao kuathiriwa na nyaraka za kughushi.

Amesema ofisi hiyo itaharakisha mchakato wa vibali, hata kwa hati zilizokwisha muda wake, na kushughulikia changamoto zilizojitokeza lengo ni kuwawezesha wafanyabiashara wa DRC kwenye sekta ya madini, kutonyanyasika na kuporwa mali zao, hatimaye kukuza mapato ya nchi zote mbili.

“Baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakijihusisha na usafirishaji haramu wa madini hivyo kusababisha kukamatwa na kuibiwa.

Aidha, kukosekana kwa ofisi ya madini nchini kumechochea changamoto kwani wafanyabiashara wasio waaminifu hughushi nyaraka,” amesema.

Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa TPA, Dk George Fasha amesisitiza umuhimu wa DRC kuwa moja ya masoko sita muhimu kutokana na ongezeko la mizigo inayopita katika bandari ya Dar es Salaam tangu 2018.

"Kuanzishwa kwa ofisi katika nchi yetu kunatoa ujumbe wa wazi kwamba wako tayari kufanya biashara na sisi, kwa hiyo, natao wito kwa wafanyabiashara kutumia fursa hizi ili kuvutia wawekezaji zaidi,” amesema.

Amesema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24, kiasi cha mauzo ya nje na ndani ya bidhaa ilifikia tani milioni 2.5, ikilinganishwa na tani milioni 1.9 katika miaka iliyopita, ikiwa ni ongezeko la asilimia 15 kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Dk Fasha amesema,"Bandari ya Dar es Salaam ina soko kubwa, ikijivunia asilimia 68 ikilinganishwa na washindani wake wanaotaka mizigo kutoka DRC, na kuongeza kuwa tukio hilo linatarajiwa kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili."

Amesema TPA ina mpango wa kuzindua ofisi nyingine Mashariki mwa nchi hiyo, ambako rasilimali za madini zinapatikana kwa wingi, lengo ni kurahisisha biashara kati ya Tanzania na DRC, kwa sasa mamlaka hiyo ina ofisi za uwakilishi Lubumbashi.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Edward Urio, amesema miaka ya nyuma kulikuwa na migogoro iliyohusisha malori yenye shaba kutekwa na kuibwa, halafu baadaye inasafirishwa tena.

Amesema kuzinduliwa kwa ofisi hiyo kutatatua changamoto hiyo na kuwahakikishia wafanyabiashara kutoka DRC akisema bandari ya Dar iko salama.

Ameongeza kuwa shaba ni bidhaa kuu inayosafirishwa nje ya nchi, pamoja na usafirishaji wa bidhaa za kemikali kwenda Lubumbashi kwa ajili ya sekta ya madini.

“Sisi wadau tunatarajia kuongeza tija kwa kufunguliwa kwa ofisi hii ni hakikisho utawajengea imani watumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam kutoka DRC, kuhakikisha uhalali wa usafirishaji wa madini yao na kupunguza wizi wa shaba. Zaidi ya hayo, itasaidia Serikali katika kuthibitisha uhalali na asili ya madini hayo,” amesisitiza.