Duni achaguliwa kumrithi Maalim Seif

Mwenyekiti mpya wa Chama cha ACT Wazalendo, Juma Duni Haji (katikati) akinyanyuliwa mkono katika uchaguzi wa chama hicho ACT katika ukumbi wa mlimani City jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
Wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo wamemchagua Juma Duni Haji kuwa Mwenyekiti wa chama hicho akijaza nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alifariki Februari 2021.
Dar es Salaam. Wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo wamemchagua Juma Duni Haji kuwa Mwenyekiti wa chama hicho akijaza nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alifariki Februari 2021.
Duni ambaye alikuwa akishindana na Hamad Masoud Hamad, amepata kura 339 sawa na asilimia 73.06 ya kura 464 zilizopigwa wakati mpinzani wake huyo naye akipata kura 125 sawa na asilimia 26.94.
"Kwa matokeo haya, ninamtangaza Juma Duni Haji kuwa mwenyekiti wa chama," amesema mwenyekiti wa uchaguzi, Joram Bashange wakati akitangaza matokeo hayo.
Kwa upande wa nafasi ya makamu mwenyekiti, wajumbe hao wamemchagua Othman Masoud Othman ambaye ni makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa kura za "ndio" 443 sawa na asilimia 98.83.
Othman alikuwa akishindana na Juma Said Saanane katika nafasi hiyo, hata hivyo Saanane alijitoa kwenye kinyanganyiro hicho siku moja kabla ya uchaguzi.
Akitoa shukrani baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Duni amewashukuru wanachama kwa kufanikisha uchaguzi huo salama na kwa kumwamini kuongoza chama hicho.
"Nawashukuru sana kwa dhamana hii, tumeweza kuvuka salama hata katika hili, nawashukuruni sana wajumbe" amesema Duni huku hotuba yake ikikatishwa na shangwe za wanachama.
Kwa upande wake, Othman naye aliwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu kwa kumwamini na kumpigia kura nyingi za ndiyo zilizomwezesha kuwa makamu mwenyekiti wa ACT Wazalendo upande wa Zanzibar.
Duni ni nani?
Duni alizaliwa mwaka 1950 huko Zanzibar, alisoma shule ya msingi Mkwajuni kati ya 1959 - 1965, baadaye akajiunga na sekondari ya juu ya Lumumba kati ya mwaka 1966 - 1969.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa masomo ya shahada ya kwanza ya elimu ya Sayansi kuanzia mwaka 1972 - 1975. Baadaye mwaka 1994 - 1995, alisoma shahada ya uzamili katika rasilimali watu katika Chuo Kikuu cha Manchester huko Uingereza.
Mwanasiasa huyo amefanya kazi katika Serikali ya Zanzibar katika nafasi mbalimbali ikiwa ni pamoja na katibu mtendaji wa Tume ya Mipango (1981 -1982), katibu mkuu - viwanda (1980 -1981), ofisa mipango - elimu (1976 -1979) na mwalimu wa sekondari (1975 - 1979).
Katika medani za siasa, Duni pia ameshika nafasi mbalimbali ikiwa ni pamoja na makamu mwenyekiti wa ACT Wazalendo, naibu kiongozi wa chama, Waziri wa Afya katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, naibu katibu mkuu wa Cuf, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Cuf.