ETDCO yajenga njia ya kupeleka umeme Dar hadi JNHPP

Muktasari:
Katika kuhakikisha mradi wa kuzalisha umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) unakamilika kwa wakati, Kampuni tanzu ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imefanikiwa kujenga njia ya kupeleka umeme kutoka Gongo la Mboto hadi kwenye mradi huo.
Dar es Salaam. Katika kuhakikisha mradi wa kuzalisha umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) unakamilika kwa wakati, Kampuni tanzu ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imefanikiwa kujenga njia ya kupeleka umeme kutoka Gongo la Mboto hadi kwenye mradi huo.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano Novemba 24, 2021 na kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Maclean Mbonile wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania bara.
Amesema wamejenga njia hiyo katika mradi huo uliopo katika bonde la mto Rufiji kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme kwa mkandarasi wa mradi.
“Kupitia mradi huo kampuni ilifanikiwa kuingiza kiasi cha Sh17.8 Bilioni, pamoja na fedha hizo hadi kufikia Juni 30 mwaka huu ETDCO imetengeneza faida ya jumla ya Sh9.6 bilioni hii ni tangu kampuni hii ilipoanzishwa,” amesema
Amesema kampuni hiyo pia imetekeleza ujenzi wa njia ya kusambaza umeme kutoka Morogoro hadi kwenye mradi huo wa JNHPP.
“Mradi huu ulianza kutekelezwa mwaka 2017 na ulikamilika mwaka 2018, uliingizia kampuni kiasi cha Sh5.8 bilioni,” amesema
Mbonile amesema ETDCO imefanikiwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye uwezo wa 132KV kutoka Mtwara hadi Lindi.
“Huu ulikuwa mradi mkubwa wa kwanza kutekelezwa na kampuni tangu kuanzishwa kwake, mradi huu ulihusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye umbali wa Kilomita 80 kutoka kituo cha umeme Mtwara hadi kwenye kituo cha umeme cha Mahumbika Lindi.
“Ukamilishwaji wa mrdai huu uliwezesha mji wa Lindi kuanza kutumia umeme unaozalishwa na mitambo inayotumia gesi iliyopo Mtwara badala ya matumizi ya umeme wa jenereta,” amesema Mbonile