Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fahamu kazi za Jaji Kiongozi na kesi anazopaswa kuzisikiliza

Fahamu kazi za Jaji Kiongozi na kesi anazopaswa kuzisikiliza

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Jaji Mustapha Siyani kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu nchini Tanzania,  kushika nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Elieza Feleshi, ambaye sasa amekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Jaji Mustapha Siyani kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu nchini Tanzania,  kushika nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Elieza Feleshi, ambaye sasa amekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Taarifa iliyotolewa Oktoba 8, 2021 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Jaffar Haniu, imeeleza kabla ya uteuzi huo Jaji Siyani alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.

Pia, Jaji Siyani ndiye anayesikiliza kesi ya uhujumu uchumi namba 16/2021 inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa na mashtaka sita likiwemo la kufadhili vitendo vya kigaidi katika Mahakama Kuu, Divesheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Hata hivyo, kumekuwa na maswali mengi kuhusu kama Jaji Siyani ataendelea kusikiliza kesi hiyo ama atajiweka pembeni ili kujikita katika kutekeleza majukumu yake mapya ya Jaji Kiongozi.

Majukumu au kazi za Jaji Kiongozi

Kutokana na sintofahamu hiyo, Mwananchi limezungumza na mawakili wa kujitegemea, Francis Stolla na Timon Vitalis, ambao wamesema Jaji Kiongozi ana majukumu zaidi ya mawili.

Wakili Vitalis amesema Ibara ya 109 (3) hadi (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaeleza kuwa Jaji Kiongozi ni Msaidizi wa Jaji Mkuu katika kusimamia Mahakama Kuu na Mahakama zote za chini.

“Ibara 109 (3) bila ya kuathiri masharti ya Katiba hii au sheria nyingine yoyote kuhusu madaraka ya Jaji Mkuu aliyetajwa katika ibara ya 118, Jaji Kiongozi atakuwa ndiye msaidizi maalum wa Jaji Mkuu katika utendaji wa kazi katika Mahakama Kuu na Mahakama nyinginezo zote za ngazi ya chini yake, na katika madaraka hayo Jaji Kiongozi atatekeleza kazi na shughuli atakazoagizwa au kuelekezwa na Jaji Mkuu, na kwa madhumuni ya ibara hii, Jaji Kiongozi atajulikana pia kama Mkuu wa Mahakama Kuu,” amesema Wakili Vitalis.

Kwa upande wake Stolla amesema: “Kwanza Jaji Kiongozi ana majukumu ya jaji wa kawaida wa Mahakama Kuu, yaani yeye ni Jaji wa Mahakama Kuu kwa hiyo anafanya kazi ambazo Jaji wa Mahakama Kuu yeyote yule anafaya.

“Jukumu lake la pili kwa kuwa yeye ni Jaji Kiongozi maana yake anaongoza Mahakama Kuu, yaani majaji wote wa Mahakama Kuu yeye ndio kiongozi wao.”

Jukumu la tatu la Jaji Kiongozi ambaye mbali ya kuwa msimamizi wa Masjala Kuu, pia ni msaidizi wa Jaji Mkuu wa Tanzania katika kuongoza Mahakama Kuu, kwa maana kwamba Mahakama Kuu pia inaongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania.

“Kwa maana hiyo sio kwamba Jaji Kiongozi atamsaidia Jaji Mkuu wa Tanzania kuongoza  Mahakama ya Rufaa, hapana kule ni juu kwa manaa Jaji Kiongozi hafiki Mahakma ya Rufani kuongoza kwa sababu yeye mamlaka yake inaishia katika Mahakama Kuu. Kwa maana kuwa cheo chake yeye Jaji kiongozi ni cha Mahakama Kuu na sio Makahakama ya Rufaa,” amesema na kuongeza kuwa:

“Ndio maana Jaji Kiongozi akifanya maamuzi yoyote huwa yanakwenda kukosolewa Mahakama ya Rufaa kwa sababu mahakama hiyo ipo ngazi ya juu ….kwa tafsiri rahisi Mahakama ya Rufaa haipo chini yake bali ipo juu yake.”

Je Jaji Kiongozi anaweza kuendesha kesi?

Wakili Vitalis amesema Jaji Kiongozi ana mamlaka ya kusikiliza mashauri yote ya Mahakama Kuu kama ilivyo kwa jaji yoyote wa Mahakama Kuu.

“Ndio maana ulikuwa unaona  Jaji Kiongozi alikuwa anasikiliza kesi ya mauaji iliyokuwa inamkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe na wenzake 12, Jaji Kiongozi wa wakati ule Salum Masati alikuwa anasikiliza kesi ile. Nakumbuka kesi ya Zombe ilifunguliwa katika masjala ya kawaida na sio Masjala Kuu, lakini ilisikilizwa na Jaji Kiongozi,” amesema Vitalis.

Kwa upande wake, Stolla amesema kama kutakuwa na maelekezo kutoka juu yakatolewa na Jaji Mkuu anaweza akasema Jaji Kiongozi akaendeshe kesi kama Jaji wa kawaida.

“Unakumbuka nilikuambia kuwa Jaji Kiongozi pia ana majukumu ya jaji wa kawaida, kwa hiyo hapo kuna direction (maelekezo) ambayo yanaweza kutoka kwa kiongozi wake, ambaye ni Jaji Mkuu kama kuna uhitaji na anaweza kuwa miongoni mwa majaji wa kawaida katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi akaendesha kesi kwa kutumia mamlaka yake kama Jaji wa Mahakama Kuu na akatoa  uamuzi,” amesema Stolla.