Familia sita zavamiwa, wanne wajeruhiwa kwa mapanga Dar

Friday May 20 2022
Familia pc
By Fortune Francis

Dar es Salaam. Familia sita zinazoishi mtaa wa Kwembe Mpakani jijini hapa, zimevamiwa na watu wanaodaiwa kuwa wahalifu, wakiwa na mapanga nondo na mawe kisha kuwajeruhi watu wanne na kupora vitu mbalimbali.

Tukio hilo la aina yake lilitokea usiku wa kuamkia juzi ambapo vijana zaidi ya kumi, walivunja mlango mmoja baada ya mwingine na kuamuru kupatiwa fedha na simu.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa Mei 20, 2022 wananchi hao waliojeruhiwa wamesema, majira ya saa tisa usiku vijana hao wakiwa na mapanga, nondo na mawe walivunja milango na kuamuru kupewa fedha na simu.

Godfrey Kimaro aliyejeruhiwa kichwani amesema, usiku wa kuamkia juzi wakiwa wamelala, alishtuka kusikia mlango wa jirani ukigongwa kwa nguvu, lakini alijua ni mwenzao anawaamshwa wakalinde.

Amesema kabla hajakaa sawa alisikia kishindo cha nguvu, lakini wakati anataka kutoka nje, mke wake alimkataza na ndipo aliposogeza kitanda mlangoni kisha kupanda juu na kuchungulia na kuona kundi la vijana zaidi ya kumi.

“Nilisikia wakisema toa hela na wakati huo watu wanalia, walipomaliza waliingia chumba kingine ndipo niliposikia mmoja wao akisema, bado chumba hiki (cha kwagu) walivunja mlango na mimi nilijaribu kuzuia lakini ilishindikana,”amesema Kimaro.

Advertisement

“Baada ya kuingi ndani walinipiga panga la kwanza kichwani, kisha wakanivuta nje na kunipiga panga la pili, walifanikiwa kuchukua simu mbili, flashi mbili, waleti iliyokuwa na kitambulisho na kadi ya benki pamoja na Sh 50, 000,”amesema.

Akisimulia mkasa huo majeruhi mwingine, Ismail Mande amesema akiwa amepumzika baada ya mihangaiko ya kutwa nzima alisikia kelele jirani, ndipo alipoamua kuamka na kuchukua panga kama shemu ya kujihami.

Amesema akiwa anasikiliza kinachoendelea alisikia mlango ukigongwa na kitu kizito, ndipo walipofanikiwa kuingia akiwa ametaharuki alisikia kitu kimemgonga kichwani lakini hakujua kama ameumia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Ramadhani Kingai amesema, tukio hilo ni la kiuhalifu kama yalivyo matukio mengine na halihusiani na Panya Road.

“Tusizue taharuki kwa wananchi, sio kila tukio la kihalifu ni panya road kilichotokea Kwembe ni watu kuvunja nyumba, kujeruhi na kuiba,” amesema Kingai.

Advertisement