Familia ya mume, mke na watoto wasioona wasiojutia maisha

Monday February 22 2021
Familia pic

Busega. Suzana Ndekeja na Josiah Athumani ni wanandoa wenye historia ya kipekee maishani.

Kwanza wao wenyewe wana ulemavu wa kutoona, lakini hata watoto wao watatu kati ya wanne nao wana ulemavu huo.

Hata hivyo, mtoto wa nne wa wakazi hawa wa kijiji cha Kalemela-Mayega Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, japo anaona, lakini anasumbuliwa na ugonjwa wa akili.

Kwa walio wengi hisia inayojengeka, ni kuwa pengine wanandoa hawa na watoto wao wangekuwa wanyonge wa nafsi, lakini kwa Suzana na Josiah, hali ni tofauti .

Maisha yao yamegubikwa na furaha, amani na mapenzi tele huku wakitumia mazingira yao kumudu maisha waliyojaaliwa na Mola.

Advertisement


Simulizi ya Suzana

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake mwishoni mwa wiki, Suzana alisema ulemavu wa macho umemsababishia madhila kadhaa ikiwamo kukataliwa familia za wanaume watatu aliozaa nao.

“Mimi nilizaliwa nikiwa na ulemavu wa macho; sijabahatika kuona katika maisha yangu yote na watoto wangu watatu nao nimewazaa wakiwa na ulemavu wa macho,” anaanza kusimulia Suzana.

Alisema alianza kumzaa mtoto wa kwanza mwenye ulemavu wa macho akifuatiwa na wa pili anayeona lakini akiwa na ulemavu wa akili.

Suzana anasema mtoto wake wa tatu naye ni mlemavu wa macho kama alivyo yeye. Wa nne naye ni mlemavu licha ya kuzaa na mwanaume ambaye sio mlemavu wa macho.

“Kuzaa watoto wasioona kumenisababishia matatizo siyo tu kwa wanaume ninaozaa nao, bali hata kwenye familia yangu. Baba yangu mzazi alinishauri nifunge uzazi kuepuka kuzaa watoto walemavu. Namshukuru mama yangu aliungana nami kupinga wazo hilo,” alisema Suzana kwa hisia.


Mume wa sasa

Kutokana na changamoto na ugumu wa maisha, Suzana anasema alijikuta akiingia mitaani kuomba misaada ya kumudu maisha ikiwamo kuwalea watoto wake.

Akiwa katika shughuli hizo jijini Mwanza ndipo alipokutana na mume wake wa sasa, Josiah Athumani ambaye pia ni mlemavu wa macho.

“Tulijikuta tunapendana na kuamua kuoana tukiwa Mwanza na tunapendana kwa dhati huku tukishirikiana kuwalea na kuwahudumia watoto wetu,” anasema Suzana.


Simulizi ya Josiah

Josiah ambaye muda wote wa mahojiano alikuwa pembeni mwa mke wake anathibitisha kuwa ulemavu wa kutoona, siyo kikwazo katika ndoa yao anayosema imejaa mapenzi ya dhati.

“Mimi nilizaliwa nikiwa naona kabla ya kupata ulemavu wa macho baada ya kuugua. Nafanya shughuli mbalimbali ikiwamo biashara ndogondogo inayoniwezesha kuhudumia familia yangu kwa mahitaji yote,” anasema

Licha ya ulemavu wao, wana ndoa hao wanapambana kupata mahitaji yote muhimu kwao wenyewe na kwa watoto wao ambao sasa wanafikiria namna ya kuwapeleka shule maalum ya walemavu ya Mitindo iliyopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.


Ombi kwa jamii, Serikali

“Hatutaki kusaidiwa kwa kulishwa kama watoto wadogo. Hapana! Tunachoomba ni kuwezeshwa kufanya shughuli halali za kutuingizia kipato cha kumudu maisha na kuwalea watoto wetu,” alisema Suzana.

Aliongeza: “Kuna wakati tunalazimika kuingia mitaani kuomba misaada. Lakini kamwe hatupendi unyonge huu kwa sababu ukiondoa kutoona, Mungu ametuachia viungo vingine vyote. Tunaweza kufanya shughuli zote za kuzalisha mali. Tunachohitaji ni kuwezeshwa kwa njia yoyote ile,” aliongeza.

Akizungumzia maisha ya wanandoa hao, Hoja Masanyiwa, mmoja wa majirani alisema ni watu wema wenye upendo na wanaopenda kufanya shughuli zao zote bila kutegemea usaidizi kutoka kwa watu wengine.

“Mwanamke anafanya kazi zote za nyumbani kama wanawake wengine hapa kijijini. Ni mara chache huwa wanahitaji msaada kwa jambo lililo nje ya uwezo wao,” alisema Masanyiwa.

Ofisa ustawi wa jamii Wilaya ya Busega, Kubagwa Madadela, anasema ofisi yake tayari imeitembelea familia hiyo na tayari inafanya taratibu za kuiingiza kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini.

Advertisement