Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

FCC yawaonya wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa bandia

Tume ya Ushindani (FCC) Nyanda za Juu Kusini imewaonya wafanyabiashara wasiowaaminifu kujiepusha na uagizaji, uzalishaji na uuzaji wa bidhaa bandia ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiwadhuru watumiaji wa bidhaa hizo hapa nchini.

Muktasari:

  • FCC nyanda za juu Kusini yawaonya wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa bandia sokoni na kusababisha madhara kwa wananchi.

Njombe. Tume ya Ushindani (FCC) Nyanda za Juu Kusini imewaonya wafanyabiashara wasiowaaminifu kujiepusha na uagizaji, uzalishaji na uuzaji wa bidhaa bandia ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiwadhuru watumiaji wa bidhaa hizo hapa nchini.

Onyo hilo limetolewa leo na Mkuu wa Kanda Ofisi ya Tume ya Ushindani (FCC) Nyanda za juu Kusini, Dickson Mbanga wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Maonesho ya Nne ya Sido kitaifa ambayo yanafanyika Sabasaba hapa mkoani Njombe.

Amesema wafanyabiashara na wazalishaji wana wajibu wa kusajili nembo zao ili kulindwa na sheria ya alama za bidhaa zao dhidi ya wazalishaji wanao iga bidhaa zao kwa nia ya kudanganya au kutapeli.

Amesema wazalishaji au wajasiriamali wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanaonyesha taarifa zote muhimu katika vifungashio­ kama Sheria ya alama za bidhaa ya mwaka 1963 ilivyoelekeza.

Amesema sheria imeweka wazi kuwa atakayekutwa na bidhaa bandia kwanza anatakiwa kulipa faini ya fedha kulingana na thamani ya bidhaa husika kisha bidhaa hiyo inateketezwa kwa moto.

Amesema lengo la tume hiyo ni kukuza na kusimamia ushindani wa biashara katika uchumi wa soko na kumlinda mtumiaji dhidi ya mienendo hadaifu na kandamizi sokoni na kudhibiti biashara ya bidhaa bandia.

"Kama kuna malalamiko yamekuja mmiliki wa nembo analalamika kwamba bidhaa yangu imehujumiwa anatoa vielelezo vyote na sisi tunashirikiana na vyombo vya dola tunakwenda kuondo hiyo bidhaa sokoni" amesema Mbanga.

Ofisa Uraghibishi kutoka Tume ya Ushindani (FCC,) Diana Augustine amesema ipo tofauti kubwa kati ya bidhaa bandia na bidhaa hafifu ambapo bidhaa hafifu ni ile ambayo imetengenezwa chini ya viwango vilivyowekwa kitaifa au kimataifa wakati bidhaa bandia ni ile ambayo imetengenezwa kwa kuiga nembo ya mzalishaji halisi bila ya ridhaa ya mhusika.

"Athari ya bidhaa bandia kwa nchi ni kubwa kwani hata wawekezaji pia wanakimbia hakuna mwekezaji ambae atawekeza katika nchi ambayo sheria ya bidhaa yake hailindwi," amesema Augustine.

Mmoja ya wakazi wa mkoa wa Njombe Feledea Mhagama ambaye amefika na kujionea bidhaa mbalimbali kwenye maonesho hayo ya Sido amesema shughuli za tume hiyo ya Ushindani zisogezwe karibu zaidi na wananchi katika ngazi ya mikoa na wilaya.

"Elimu pia iongezwe kwa wananchi kuhusu haki, wajibu na nafuu zinazopatikana kwa mujibu wa sheria za ushindani na kumlinda mlaji na uthibiti wa bidhaa bandia" amesema Mhagama.