Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

G7 waahidi kuimarisha mapambano dhidi ya saratani duniani

Muktasari:

  • Kupitia Mkutano wa Viongozi wa G7 wa 2026 uliofanyika Evian, nchini Ufaransa, viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya kimataifa yakiwemo amani na usalama duniani, utulivu wa uchumi wa dunia, ukuaji wa uchumi pamoja na maendeleo ya teknolojia zinazoibukia.

Dar es Salaam. Viongozi wa mataifa saba yenye uchumi mkubwa duniani (G7) wameahidi kuongeza juhudi za pamoja katika mapambano dhidi ya saratani, ugonjwa unaosababisha vifo vya karibu watu milioni 10 kila mwaka duniani.

Tamko hilo limeungwa mkono na nchi washirika za G7 ambazo ni Brazil, Misri, India, Kenya na Jamhuri ya Korea Kusini, zikisisitiza umuhimu wa kuharakisha hatua za kuzuia, kugundua mapema na kutibu ugonjwa huo.

G7 inaundwa na mataifa ya Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uingereza, Canada na Japani.

Kwa mujibu wa viongozi hao, idadi ya wagonjwa wapya wa saratani inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2050 kutokana na ongezeko la umri wa watu, athari za mazingira na mienendo ya maisha inayochangia hatari ya ugonjwa huo.

Taarifa ya pamoja ya viongozi wa G7 iliyotolewa na Baraza la Umoja la Ulaya jana Juni 17, 2026 imebainisha ongezeko la ugonjwa huo, ni mzigo kwa mifumo ya afya, jamii na uchumi wa nchi mbalimbali ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa mapema.

Katika tamko lao, viongozi hao wameeleza licha ya mafanikio makubwa ya kisayansi yaliyopatikana kupitia tafiti za saratani, bado kuna haja ya kuharakisha utafiti na kuhakikisha ubunifu wa kisayansi unawafikia wagonjwa kwa haraka zaidi.

"Maendeleo yaliyofikiwa dhidi ya mapambano ya saratani ya mlango wa kizazi yanaonesha uwezekano wa kutokomeza ugonjwa huo siku zijazo, hivyo kuahidi kuongeza juhudi za kufanikisha lengo hilo," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, viongozi hao wameeleza dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwenye tafiti za kisayansi, kuziba mapengo yaliyopo eneo la kinga na uchunguzi wa mapema wa saratani, pamoja na kuhakikisha maendeleo ya tiba yanawanufaisha wagonjwa wote bila ubaguzi.

Miongoni mwa maeneo yatakayopewa kipaumbele yaliyoanishwa na viongozi hao, ni  kuimarisha upatikanaji wa taarifa na takwimu za saratani zinazowaathiri  watoto, vijana balehe na watu wazima.

"Hakuna nchi moja yenye taarifa za kutosha kutoa ushahidi wa kisayansi kuhusu aina zote za saratani zinazowapata watoto na vijana, hivyo kuna umuhimu wa kushirikiana katika ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa hizo," taarifa hiyo imeeleza.

Chini ya mpango huo, nchi hizo zinalenga kuunganisha mifumo ya taarifa za saratani, kuboresha viwango vya ubadilishanaji wa taarifa na kuruhusu ushirikiano wa kimataifa kwa kuzingatia sheria za faragha, ulinzi wa taarifa na haki za ubunifu.

Pia zimeahidi kuendeleza matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo akili unde (AI), kuchanganua taarifa za kitabibu, vinasaba na picha za uchunguzi kwa lengo la kuboresha utafiti na matibabu ya saratani.

Katika hatua nyingine, viongozi hao wamesema saratani zenye kiwango kikubwa cha vifo bado ni changamoto kubwa kwa dunia, hivyo wataongeza uwekezaji katika tafiti zinazolenga kuboresha matokeo ya matibabu ya saratani hizo.

"Tutaweka malengo ya kuongeza programu za uchunguzi wa saratani na kuimarisha utambuzi wa ugonjwa huo katika hatua za awali, hatua ambayo inaongeza nafasi za wagonjwa kupona," taarifa hiyo imeeleza.

Kwa mujibu wa tamko hilo, juhudi maalumu pia zitaelekezwa kupunguza vifo vinavyotokana na saratani ya mapafu kwa miaka 10 ijayo.

Viongozi hao wameahidi kuimarisha ushirikiano eneo la majaribio ya kitabibu, kuharakisha matumizi ya teknolojia za kidijitali, akili unde (AI) na tafiti za teknolojia za kisasa na huduma za wagonjwa.

Kuhusu huduma za matibabu, G7 imesema itaunga mkono juhudi za nchi mbalimbali katika kuimarisha mifumo ya afya ili iweze kutoa huduma bora za saratani kwa wananchi wote.

Pia imehimiza kuanzishwa na kuimarishwa kwa vituo maalumu vya saratani vitakavyokuwa kitovu cha tafiti, elimu na utoaji wa huduma bora za matibabu.

"Matumizi ya teknolojia za kidijitali na akili unde(AI) yanapaswa kufanyika kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi, usalama wa wagonjwa na ulinzi wa faragha zao," amesema.

Taarifa hiyo imetolewa baada ya majadiliano ya viongozi wa G7 kwa kushirikiana na nchi washirika, ambapo wameahidi kuendelea kufuatilia utekelezaji wa hatua walizokubaliana ili kuimarisha mapambano dhidi ya saratani duniani.