Gaddafi mtata tangu utotoni

Tuesday October 19 2021
gadaffipic
By William Shao

Katika toleo lililopita, tuliangalia namna aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, alivyokamata na kuuawa Oktoba 20, 2011. Je, alipandaje hadi kuwa kiongozi wa nchi hiyo?

Hakuna anayejua kwa hakika ni lini Muammar Gaddafi alizaliwa, lakini kulingana na alivyokiri yeye mwenyewe ni kwamba alizaliwa mwaka 1941 katika kijiji cha Qasr Bu Hadi kilichoko mji wa Sirte nchini Libya. Hata hivyo, simulizi nyingine za kihistoria zinasema mwaka 1942 huku wengine wakiandika kuwa alizaliwa mwaka 1943. Vyovyote iwavyo, hakuna ubishi kuwa alizaliwa huko Sirte, Libya.

Muammar alikuwa mtoto wa pekee wa kiume aliyezaliwa na mfugaji wa mbuzi, Mzee Abu Miniar na mkewe Aisha Ben Niran, wote wakiishi katika hali ya umaskini na wakati mwingine wakifanya biashara ya mahema.

Soma zaidi:Ripoti yalaumu Uingereza kumuondoa Gaddaffi

Akiwa mtoto wa pekee wa kiume kwa wazazi wake, Gaddafi ni mwisho kuzaliwa baada ya kutanguliwa na dada zake watatu. Familia hiyo ilikuwa sehemu ya ‘Qaddadfa’, kabila la Kiarabu la Waberber linalojumuisha koo kadhaa ndogo ambazo zimeenea kote nchini Libya. Alipozaliwa alipewa jina la Muammar Mohammed Abu Minyar Gaddafi.

Kabila hilo, ambalo jina lake linamaanisha “kutupa”, linaweza kufuatiliwa historia yake hadi kwa mtakatifu anayejulikana kama Sidi Qaddaf Al-Dam, ambaye baada ya kufariki kwake alizikwa huko Gharyan, kusini mwa Tripoli. Haishangazi kwamba watu wa eneo hilo ndio waliosimama na Gaddafi hadi ile siku ya mwisho ya maisha yake.

Advertisement

Ingawa hapo awali kabila hilo lilikuwa dogo kwa viwango vya Libya, hatimaye kabila la Qaddafa lilikuja kuwa moja ya makabila makubwa zaidi katika mkoa wa Sirte. Hata hivyo, bado lilikuwa na watu wengi masikini.

Gaddafi mwenyewe aliwahi kuelezea jinsi walivyokuwa wakiishi katika kijumba kidogo cha mahema alichokulia na jinsi walivyokuwa wakitoka katika kijumba hicho kwenda kutafuta vyuma chakavu, maganda ya risasi tupu na mabaki mengine ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia ambavyo wangeweza kuviuza na kujipatia kipato.

Akiwa shuleni alikuwa mtulivu sana na alikuwa akitabasamu kila wakati. Hakupenda sana kucheza na wenzake na mara kwa mara alionekana akiwa katika mawazo.

Kulingana na simulizi za mwalimu wake katika shule ya upili, Shalan Abdelkhaliq, siku zote Muammar alionekana wakati wa mapumziko akiwa amesimama peke yake katika ua wa shule kana kwamba alikuwa kisiwa binafsi.

Ni wazi kwamba, kama mtoto wa pekee, Gaddafi alikuwa na nafasi maalumu katika mioyo ya wazazi wake, na baba yake alikuwa na hamu kubwa kwa Gaddafi kupata elimu. Hakukuwa na shule katika eneo ambalo familia hiyo iliishi, lakini baba yake alipanga kwamba ‘faqi’ (mwalimu wa dini), awe anakuja nyumbani kwao kumfundisha mtoto wake misingi ya elimu.

Gaddafi naye alikuwa na hamu ya kujifunza; mwaka 1954 alimshawishi baba yake amruhusu asome shule ya msingi huko Sirte ambako angelazimika kukaa mbali na nyumbani. Baba yake alisimulia kwamba hakuwa na fedha ya kulipia hosteli, kwa hiyo Gaddafi alilazimika kulala msikitini.

Lakini kila mwisho wa wiki alikuwa akirudi nyumbani kwa kutembea zaidi ya kilometa 30 kuungana na familia yake. Pia kila wakati wa mavuno alilazimika kurudi nyumbani, akikatisha masomo yake kusaidia kazi za nyumbani.

Akiwa shuleni alionekana kuwa tofauti na wenzake. Mojawapo ya mambo mengi yaliyomtofautisha na wenzake ni kwamba alikuwa na umri mkubwa kuliko wanafunzi wengine katika darasa lake.

Kwa mujibu wa chanzo fulani, binamu yake anayeitwa Muftah Ali Subaya Qaddafi anasimulia hivi: “Tulikuwa watatu au wanne kati yetu wa kabila letu shuleni, na tulidharauliwa kabisa. Tulikuwa maskini sana kiasi kwamba mara nyingi hatukuwa na chakula wakati wa mapumziko ... Tulidhihakiwa naye alichukia. Dhihaka kama hizo zilimchochea sana kuwa kiongozi na kufanya kazi kwa bidii zaidi ... Nia yake ya kujifunza ilikuwa kubwa, hususan wakati wanafunzi walipomkabili kwa dhihaka na kumwita ni ‘mkazi wa jangwani’.”

Baada ya miaka kadhaa shuleni huko Sirte, familia ya Gaddafi ilihamia Sebha, kusini mwa Libya.

Qaddafi alijiandikisha katika shule ya upili ya eneo hilo, na hapa ndipo alianza kuwa na mwamko wa kisiasa. Kama vijana wengi wa siku zake, mawazo ya Gaddafi yalichochewa sana na mapinduzi ya ya serikali yaliyofanyika Misri, na alipenda sana kusikiliza redio ya ‘Sauti ya Waarabu’. Mapinduzi hayo yalifanyika Jumatano ya Julai 23, 1952 na yalijulikana pia katika historia kama ‘Mapinduzi ya Julai 23 ambayo yaliuondoa madarakani utawala wa Mfalme Farouk.

Mapinduzi hayo yaliyoongozwa na Mohammed Naguib na Gamal Abdel Nasser yalileta wimbi la siasa za mapinduzi katika ulimwengu wa Kiarabu, na kuchangia kuongezeka kwa ukoloni, na kukuza mshikamano wa ulimwengu wa tatu wakati wa vita baridi.

Gaddafi alivutiwa sana na Rais Nasser kiasi kwamba alianza kukariri hotuba za kiongozi huyo wa Misri na kuzisoma mbele ya wanafunzi wenzake.

Licha ya ujana wake, kwa mujibu wa historia ya maisha yake, ni dhahiri Gaddafi alikuwa tayari alikuwa mtu wa haiba; wanafunzi wenzake walimbebea kiti ambacho angeweza kusimama juu yake ili kutoa hotuba zake.

Alianza pia kuandaa maandamano madogo madogo dhidi ya utawala wa wakoloni. Aliwaongoza wanafunzi wenzake katika mgomo wa jumla kila Desemba 2 kila mwaka kupinga Azimio la Balfour la 1917, ambalo lilikuwa ni taarifa ya Uingereza ya kuunga mkono kuanzishwa kwa taifa la Wayahudi huko Palestina.

Gaddafi akiwa bado shuleni pia aliitisha maandamano ya kawaida nje ya ubalozi mdogo wa Ufaransa huko Sebha, ambapo, kutoka kwenye kiti chake alichokuwa amesimama juu yake akikitumia kama jukwaa, aliweza kutoa hotuba akipinga dhuluma ambazo Wafaransa walikuwa wakifanya huko Algeria na kwingineko katika bara la Afrika.

Lakini haikuwa tu serikali ya kifalme ya Libya ambayo Gaddafi aliipinga, bali pia aliwashutumu wasomi waliokuwa kwenye utawala nchini Libya. Akiwa na hasira kutokana na ufahamu wake mpya wa kisiasa, aliongoza kikundi kidogo cha wavulana wa shule kwenda kuvunja madirisha ya hoteli ya Sebha kwa sababu ilikuwa ikiuza pombe na hivyo kuathiri maadili ya wakazi wa hapo.

Baada ya kufukuzwa shuleni Sebha kutokana na kitendo chake cha kuandaa maandamano kwenda kushambulia vituo vya Uingereza na Marekani nchini Libya, Gaddafi alianza kufahamika zaidi, na akawa kivutio kikubwa katika shule yake mpya huko Misrata.

Chuki yake dhidi ya yule aliyemtaja kama ‘mfalme dhaifu’ anayeendeshwa na ‘nguvu za kibeberu’ ilizidi kuwa kubwa kila siku, na hakuogopa kuiruhusu chuki hiyo ionekane.

Chuki yake aliidhihirisha kwa aliyekuwa mkaguzi wa shule wa Kiingereza aliyeitwa Johnson, ambaye Gaddafi alimkataa shuleni hapo akisema:

“Hatutaki wakala wa ubeberu” huku akimpungia picha ya Rais Nasser wa Misri.

Baada mkaguzi huyo kumwamuru Gaddafi aondoke kwenye chumba cha darasa la shule hiyo, Gaddafi alimwambia mkaguzi kwa ukali:

‘Wewe ndiye unayepaswa kuondoka kabisa, si tu kwenye chumba hiki bali uondoke kabisa nchini (Libya).”

Je, nini kiliendelea? Usikose mfululizo wa makala hizi.

Advertisement