Halmashauri Jiji la Arusha yakabidhi hundi Sh2.6 bilioni kwa vikundi 169

Arusha. Halmashauri ya jiji la Arusha imekabidhi hundi  ya Sh2.6 bilioni kwa vikundi 169  vya wanawake, vijana na walemavu vilivyokidhi vigezo vya kikanuni kupata mikopo  hiyo.


Akizungumza  leo Machi 22, 2023 jijini Arusha Kaimu Mkurugenzi jiji la Arusha, Hargeney Chitukuro amesema jumla ya vikundi 205 viliwasilisha maombi yao kwenye mfumo wa TPLMIS, ambapo uhakiki ulifanyika na kubaini kuwa vikundi saba vimejikita katika shughuli zenye mwelekeo wa uzalishaji kupitia vikundi vidogovidogo na usindikaji.

Aidha amesema vikundi 28 vinafanya miradi ya uzafirishaji 77 vinajihusisha na miradi ya kilimo na ufugaji na vikundi 93 vinajihusisha na biashara na ujasiriamali ambapo katika hivyo vikundi 169 ndivyo vilivyokidhi  vigezo.

Aidha amesema Halmashauri ya Jiji la Arusha kuanzia Julai  hadi sasa hivi walishatoa kiasi cha Sh3.9 bilioni kwa vikundi 339 hadi sasa hivi ambapo zimewawezesha kutengeneza  ajira mbalimbali kwa makundi hayo.

Amesema kati ya vikundi hivyo jumla ya vikundi 127 ni vya wanawake huku vikundi vya vijana vikiwa 32 na watu wenye ulemavu vikiwa 10 .

"Haijawahi kutokea  jiji la Arusha kupata mikopo ya fedha nyingi hivi, hivyo tunawaomba sana mnaopatiwa mikopo hii leo mkawe  warejeshaji wazuri na mkarejeshe  kwa wakati  ili na wenzenu waweze kunufaika kupitia  mikopo  hiyo na kujikwamua  kiuchumi," amesema Chitukuro


Naye Mkuu wa wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa amepongeza jitihada hizo za jiji la Arusha kuhakikisha makundi hayo yanawezeshwa na kujikwamua kiuchumi na haijawahi  kutokea halmashauri kutoa kiasi kikubwa cha fedha namna hiyo.

Amesema mikopo hiyo ina nia mjema ya kuwakomboa wananchi wake kutoka kwenye hali duni zaidi ili waweze kufanya biashara na kujikwamua kiuchumi.

"Nawaomba sana mkafanye biashara zenye ubunifu ili muweze kurejesha kwa wakati na wenzenu wengine waweze kupata na hata kuiga mfano kutoka kwenu kwani itawasaidia  kutoka sehemu moja kwenda nyingine," amesema Mtahengerwa.

Meya wa jiji la Arusha, Maximilian Iraghe amesema kwa mara ya kwanza jiji la Arusha limevunjuka rekodi ya kutoa pesa nyingi kupitia mapato ya fedha za ndani .

Amesema kuwa Arusha mapato yameongezeka kutoka  Sh30.5 bilioni kwa mwaka 2022/2023  hadi kufikia Sh60.6 kwa mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 100 .

"Kupitia fedha hizi  zilizotolewa leo tunatarajia  kuwa na jiji la Arusha litabadilika na vijana kuweza kujikwamua kiuchumi kwa kujihusisha na shughuli mbalimbali na hatimaye kuweza kutengeneza ajira kwa vijana wengine," amesema Iraghe.

Kwa upande wake Mjasiriamali kutoka kikundi cha Genevaglory kutoka Kaloleni, Neema Koya amesema kuwa mikopo  hiyo itawasaidia sana kujikwamua kiuchumi na kuweza kuondokana na changamoto mbalimbali huku wakijitahidi kurejesha  kwa wakati.