Hatua kwa hatua jitihada kupata Uhuru wa Tanganyika

Desemba 9 mwaka huu, Tanzania inatimiza miaka 62 tangu ipate Uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Uingereza.

Kuanza na kukua kwa mwamko wa utaifa na harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika zilipitia hatua tatu.

Hii ni pamoja na shughuli za chama cha TAA (Tanganyika African Association) kuanzia mwaka 1945 hadi 1954, shughuli za Tanu (Tanganyika African National Union) kuanzia 1954 mpaka 1958 na shughuli nyingine zilizofanyika kuelekea kwenye Uhuru kuanzia mwaka 1958 hadi 1961.

Hatua ya kwanza ilkuwa ni kukibadilisha chama cha TAA kuwa asasi ya kiraia. TAA kilianzishwa mwaka 1929 ikiwa ni matokeo ya kukibadilisha Chama cha Watumishi wa Serikali kilichojulikana kama Tanganyika Africans Civil Servants Association (TACSA) ambacho kilianzishwa mwaka 1922.

Kuanzia mwaka 1929 mpaka 1945, TAA kilifanya kazi kama asasi ya kiraia kikitetea haki za Waafrika waliokuwa wakibaguliwa na kukandamizwa chini ya sheria za kikoloni. Wakati huo TAA kilikuwa kikijishughulisha zaidi na wasomi maeneo ya mjini.

Kuanzia 1945 hadi 1954, ingawa kiliendelea kufanya kazi kama asasi ya kiraia, shughuli zake zilianza kuchukua mwelekeo wa kisiasa. Kilianza kufungua matawi vijijini. Mikakati ya aina mbili ilitumika kufungua matawi vijijini na nchi nzima ya Tanganyika.

Moja ilikuwa ni kufungua matawi mapya na nyingine ilikuwa kuyabadilisha matawi ya asasi nyingine za kiraia kwa mfano vyama vya ushirika kuwa matawi ya TAA. Matokeo ya shughuli hiyo wanachama waliongezeka kutoka 3,000 hadi 30,000 ilipofikia mwaka 1954.

Licha ya kuongezeka kwa matawi, TAA ilianza kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima katika jitihada za kuwahamasisha wananchi wawe na mwamko wa siasa. Hata ilipofika 1954 TAA ikawa imeshajiaandaa kubadilika kuwa chama cha siasa cha kupigania uhuru, kwa jina la Tanganyika African National Union (Tanu).

Hatua ya pili ya utaifa na kupigania uhuru katika Tanganyika inazungumzia kipindi cha kuanzia 1954 hadi 1958. Tukio kubwa katika kipindi hicho ilikuwa ni kuanzishwa kwa chama cha Tanu Julai 7, 1954, chama ambacho kimetokana na kubadilishwa kwa TAA kuwa Tanu. Zoezi lenyewe lilianza kwa kumchagua Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1953 kuwa Rais wa TAA.

Wakati huo Mwalimu Nyerere alikuwa akifundisha Shule ya Sekondari Pugu, jijini Dar es Salaam. Alipewa jukumu la kuandaa katiba ya Tanu, chama ambacho sasa ni cha kisiasa. Kulikuwa na wanachama 17 waanzilishi na Mwalimu alichaguliwa kuwa Rais wa Tanu.

Chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, Tanu ilifanya mambo mawili makubwa kuanzia 1954 hadi 1958. Jambo la kwanza, ilifungua matawi nchi nzima na kuwahamasisha wananchi wajiunge na Tanu na kushiriki harakati za kudai uhuru. Matawi yote ya TAA yaligeuzwa kuwa matawi ya Tanu na matawi mengine mapya yalifunguliwa.

Tanu ilitumia neno moja tu kama kikorombwezo katika mikutano yake —– “Uhuru”. Matokeo ya kampeni hiyo yalikuwa mazuri , watu walijitokeza kwa wingi kujiunga na Tanu. Mwalimu Nyerere na viongozi wengine walizunguka nchi nzima kuwahamasisha wananchi kuhudhuria mikutano ya hadhara.

Jambo la pili ilikuwa kwenda Umoja wa Mataifa (UN). Februari 1955, Tanu iliamua kumpeleka Mwalimu Nyerere Umoja wa Mataifa kama Rais wake kueleza namna Tanganyika inavyoendesha ‘vita’ ya kutafuta uhuru. Safari hiyo iligharamiwa na wanachama wa Tanukwa njia ya michango.

Katika hotuba yake Umoja wa Mataifa, Mwalimu aliliambia Baraza hilo jinsi Tanu ilivyoundwa na kwamba madhumuni ya chama hicho ni kudai Uhuru wa Tanganyika. Alieleza pia kuwa watawala wake wote wa kikoloni—Waingereza na Wajerumani—walikuwa wakandamizaji na wanyonyaji, hivyo hawakuleta maendeleo yoyote kwa watu wa Tanganyika.

Aliutaka Umoja wa Mataifa umsaidie katika jitihada zake hizo. Umoja wa Mataifa ulimwambia kuwa utatuma ujumbe kufanya utafiti juu ya uhalisia wa mambo katika Tanganyikam ili uweze kusaidia katika mapambano hayo ya kudai uhuru.

Kipindi cha tatu cha kuanzia 1958 hadi 1961 kilitawaliwa na matukio mengi muhimu. Tukio la kwanza lilikuwa mkutano mkuu wa kihistoria wa Tanu uliofanyika Januari 26, 1958 mjini Tabora ukiwa na agenda mbili: i, Sera ya Tanu Tanganyika itakapopata uhuru na ii, ilikuwa kama Tanu ishiriki kwenye uchaguzi mkuu wa kwanza uliokusudiwa kufanyika Septemba 1958 au la.

Kutokana na busara ya Rais wa chama, Mwalimu Nyerere, iliamuriwa kuwa Tanu ishiriki katika uchaguzi huo, licha ya mazingira ya ubaguzi wa rangi yaliyowekwa na wakoloni.

Tukio la pili lilikuwa Juni 1958. Mwalimu Nyerere alishtakiwa mahakamani kwa kosa la kuwatukana makamishna wawili wa wilaya kutoka Mkoa wa Ziwa. Shabaha ya serikali ya kikoloni ilikuwa ni kumfunga Mwalimu.

Kesi yenyewe ilisikilizwa kuanzia Julai hadi Agosti 1958. Na hukumu yake ilikuwa alipe Sh3,000 au aende jela miezi sita. Tanu na mashabiki wake walichanga papo hapo Sh3,000 na hivyo kumwezesha kulipa faini na kuachiwa huru. Huu ulikuwa ushindi mkubwa kwa Mwalimu na Tanu.

Tukio la tatu lilikuwa chaguzi za 1958, 1959 na 1960. Uchaguzi wa 1958 ulifanyika kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza, ikihusisha mikoa mitano, ulifanyika kuanzia Septemba 8 hadi 10, 1958 na awamu ya pili, ikihusisha mikoa mingine mitano, ulifanyika kuanzia Februari 9 hadi 17, 1959.

Matokeo ya chaguzi zote mbili Tanu ilishinda viti vyote. Wakati wa chaguzi hizo vyama ya siasa vitatu vilishiriki. Vyama hivyo vilikuwa United Tanganyika Party (UTP) ambacho kilianzishwa mwaka 1957, Tanu na African National Congress (ANC) ambacho kilianzishwa mwaka 1958 baada ya kujitenga na Tanu.

Uchaguzi wa 1960, Tanu kwa mara nyingine ilishinda kwa asilimia 98.59 sawa na viti 70 kati ya 71 vya Baraza la Kutunga Sheria. Kiti hicho kimoja kilichukuliwa na mgombea wa kujitegemea.

Safari hii, tofauti na chaguzi za 1958 na 1959, vyama vinne vya siasa vilishiriki badala ya vitatu vya awali. Chama cha nne kilikuwa All Muslims National Union of Tanganyika (AMNUT) ambacho kilianzishwa mwaka 1959. Kimsingi, hiki kilikuwa chama cha Waislamu.

Tukio la nne lilikuwa kuanzishwa kwa Serikali ya madaraka. Baada ya uchaguzi wa 1960, Tanu ilipewa jukumu la kuunda Serikali ya madaraka. Katika serikali hiyo, Mwalimu Nyerere alikuwa Waziri Kiongozi, naye aliwateua mawaziri kumi wa kufanya nao kazi. Nyerere hakuwa tu kiongozi wa serikali ya madaraka bali alikuwa kiongozi wa Baraza la Kutunga Sheria pia.

Matukio ya tano na sita yalijumuisha kuanzishwa kwa Serikali ya Ndani na kupatikana kwa uhuru. Serikali ya Ndani iliundwa Mei 1961. Katika muundo wa serikali hiyo, nafasi ya Mwalimu ilibadilishwa kutoka kuwa Waziri Kiongozi na kuwa Waziri Mkuu.

Katika azma hiyo, Mwalimu aliandaa itikadi na mwelekeo wa sera za chama katika kulijenga taifa jipya. Desemba 9, 1962 Tanganyika ilijitangaza kuwa Jamhuri na katika uchaguzi uliofanyika Novemba 1962, Mwalimu alishinda na kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika.