Waziri kiongozi aunda baraza la mawaziri-2

Kuelekea maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika gazeti hili linakuletea mfululizo wa makala za kumbukumbu za tukio hilo muhimu kwa historia ya nchi yetu.

Baada ya jana kuanza na hatua kwa hatua jitihada za kupata uhuru, leo tunaangazia jinsi Tanganyiko ilivyopata fursa ya kuunda Baraza la Mawaziri kabla ya kupewa uhuru kamili. Endelea.

Jumatatu ya Mei 1, 1961, ikiwa ni miezi sita kabla Tanganyika haijapata uhuru, ilipata Serikali ya kujitawala, Mwalimu Julius Nyerere akiwa waziri kiongozi.

Ingawa Gavana wa Kiingereza alikuwa bado na mamlaka fulani katika masuala muhimu ya nchi, Mwalimu Nyerere alipewa mamlaka ya kuunda baraza la hilo kama ifuatavyo:


Rashidi Mfaume Kawawa

Aliteuliwa waziri asiye na wizara maalumu kabla hajawa Waziri wa Serikali za Mitaa baadaye. Agosti 1958, Kawawa alichaguliwa kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria (Legico) na Oktoba 1960 ilipoundwa Serikali ya Tanganyika, aliteuliwa kuwa Waziri wa Serikali za Mitaa na Nyumba. Alizaliwa Wilayani Songea Alhamisi ya Mei 27, 1926. Aliaga dunia Alhamisi ya Desemba 31, 2009 akiwa na umri wa miaka 83.


Abdallah Said Fundikira

Aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Upimaji Ramani na Maji. Huyu alikuwa Mtemi wa 19 wa Unyanyembe. Utawala wake ulidumu kwa miaka 5 kuanzia mwaka 1957 mpaka 1962. Baada ya Tanganyika kupata uhuru 1961 ndipo Mwalimu Nyerere alipofuta utemi wa dola rasmi mwaka 1962. Na baada ya utemi kufutwa, alimteua Fundikira kuwa waziri.


Sir Ernest Vasey

Aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha. Huyu hakuwa Mtanganyika. Aliingia Afrika Mashariki mwaka 1936 na kukaa nchini Kenya kwa miaka 23 ambako alishika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya kikoloni nchini humo. Mwaka 1945 alichaguliwa kuwa mbunge wa Nairobi Kaskazini. Mwaka 1952 aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Maendeleo wa Kenya na kushikilia wadhifa huo hadi mwaka 1959. Alipoingia Tanganyika mwaka mmoja baadaye, Februari 1960, akateuliwa kuwa Waziri wa Fedha wa Tanganyika. Sir Vasey aliteuliwa na Gavana, kwa maombi ya Mwalimu Nyerere, kuingia katika Legico, kabla ya Nyerere kumteua kuwa Waziri. Alisoma bajeti yake ya kwanza ya Tanganyika ya mwaka wa fedha wa 1960/61 Aprili 7.


Amir Habib Jamal

Huyu aliteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda. Mwaka 1958 alichaguliwa kuingia Legco. Huyu ni Mhindi pekee aliyekuwa katika Serikali ya kwanza ya Tanganyika na ambaye aliendelea kuwamo katika awamu mbalimbali za Serikali za Mwalimu Nyerere kwa miaka mingi baada ya uhuru. Juni 1959 ndipo alipoingia serikalini kwa mara ya kwanza alipoteuliwa kuwa Waziri wa Tawala za Miji na Majengo. Uteuzi huo ulitokana na uchaguzi wa kura tatu mwaka 1958.

Amir Jamal, mwenye asili ya India, alizaliwa Alhamisi ya Januari 26, 1922 nchini Tanganyika.


Asanterabi Zephaniah Nsilo Swai

Swai aliteuliwa kuwa Waziri wa Biashara. Kabla ya hapo alikuwa meneja mkuu wa Chama cha Ushirika cha Meru na alikuwa Mwenyekiti wa Tanu wa Mkoa wa Kanda ya Kaskazini. Alikuwa pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Ustawi wa Jamii ya Tanu. Swai alipata elimu yake katika vyuo vikuu vya Makerere, Uganda; Bombay, India na Pittsburg, Marekani, ambako alipata stashahada na Chuo Kikuu cha Delhi, India, alikotunukiwa shahada ya uchumi.


Tewa Said Tewa

Huyu aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi na Upimaji. Alizaliwa mwaka 1924 mjini Dar es Salaam na alikuwa akiishi Magomeni Mikumi na mmoja wa watu wa mwanzo kumpokea na kufahamiana na Nyerere alipokuja Dar es Salaam mwaka wa 1952.


Paul Lazaro Bomani

Huyu aliteuliwa kuwa Waziri wa Ukulima na Maendeleo ya Ushirika. Bomani, mzaliwa wa Ikizu katika Wilaya ya Musoma, aliingia katika Serikali ya Nyerere akiwa na umri wa miaka 35. Kama alivyokuwa Kahama, Bomani naye alijishughulisha sana na masuala ya ushirika katika Kanda ya Ziwa na alikuwa kiongozi wa chama cha Ushirika Victoria Federation of Co-operative Unions (VFCU). Alizaliwa Januari 1, 1925 na kuaga dunia Aprili 1, 2005 akiwa na umri wa miaka 80.


Oscar Salathiel Kambona

Yeye aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu akiwa na umri wa miaka 32. Kambona alizaliwa Agosti 13, 1928 katika Kijiji cha Kwambe karibu na Mbamba Bay. Alifariki dunia mjini London Julai 1997 akiwa na umri wa miaka 69.


Derek Noel Bryceson

Yeye alikuwa mkulima, lakini aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya na Masuala ya Wafanyakazi. Kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 37. Bryceson aliingia Tanganyika kwa mara ya kwanza mwaka 1952 akitokea Kenya. Alipata elimu yake katika Chuo Kikuu cha Cambridge nchini Uingereza na alikuwa katika kikosi cha Jeshi la Anga la Uingereza wakati wa Vita Kuu, II ya Dunia.

Kwa mara ya kwanza aliingia serikalini mwaka 1957 kwa cheo cha Waziri Msaidizi wa Kazi za Starehe na baadaye, Juni 1959, akawa Waziri wa Machimbo ya Madini na Biashara na mwaka uliofuata, 1960, akaingia katika Serikali ya Mwalimu Nyerere.

Tofauti na wazungu wenzake waliokuwa katika Serikali ya Mwalimu Nyerere, Bryceson alikuwa mjumbe wa kuchaguliwa wa Legico kutoka Jimbo la Kaskazini. Bryceson ni raia wa Uingereza aliyezaliwa China Desemba 31, 1922. Hata hivyo alipata elimu yake nchini Uingereza. Alifariki dunia Oktoba 1980 akiwa na umri wa miaka 58.


Clement George Kahama

Aliteuliwa kuwa Waziri wa Usalama na Amani ya Nchi (Waziri wa Mambo ya Ndani kama ilivyojulikana wakati huo). Kahama kutoka Karagwe, Jimbo la Ziwa Magharibi, wakati huo alikuwa na umri wa miaka 32. Alipata elimu yake katika Sekondari ya Tabora na kisha Chuo cha Loughborough cha Uingereza. Alizaliwa mjini Karagwe Novemba 30, 1929. Alifariki dunia Jijini Dar es Salaam Machi 12, 2017 akiwa na umri wa miaka 88.


Job Malecela Lusinde

Aliteuliwa kuwa Waziri wa Serikali za Mitaa. Alijiunga na Tanu mwaka 1955 baada ya kurejea kutoka masomoni Makerere, Uganda. Katika Jimbo la Kati, Lusinde alikuwa naibu katibu wa Tanu wa jimbo. Alizaliwa Oktoba 9, 1930 mkoani Dodoma na kufatriki dunia Julai 7, 2020 akiwa ndiye waziri wa mwisho miongoni mwa mawaziri 11 walioteuliwa na Mwalimu Nyerere baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.

Alihudumu kama waziri wa kwanza wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuanzia 1961 hadi 1963 kabla ya kuhamishiwa katika wizara nyingine alizozitumikia hadi mwaka 1975.