Kwa nini Julius Nyerere alijiuzulu uwaziri mkuu

Dar es Salaam. Mwalimu Julius Nyerere alipoteuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Tanganyika Mei 1, 1961, alidumu katika wadhifa huo kwa siku 241 tu hadi alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika, Desemba 9, 1961 Tanganyika ilipopata uhuru.

Katika wadhifa wake wa uwaziri mkuu alikaa kwa siku 266 tu tangu alipoteuliwa hadi alipojiuzulu na kurudi kijijini kwake Butiama mkoani Mara.

Alipojiuzulu uwaziri mkuu na Rashidi Kawawa kuchukua nafasi yake, Nyerere alitoa sababu za kujiuzulu huko kuwa ni kwenda kujenga Chama cha Tanganyika Africans National Union (Tanu), lakini hiyo ndiyo ilikuwa sababu?

Hakukuwa na hakuna sababu yoyote ya kutilia shaka kile kilichotajwa na Mwalimu Nyerere kama sababu za kujiuzulu kwake uwaziri mkuu kwa wakati huo. Hata hivyo, kitendo cha Tanu kuimarika zaidi na kurudi kwake madarakani kama Rais wa nchi, kilifanya sababu alizozitaja zionekane halisi kuliko ilivyodhaniwa awali.


Kwa nini Nyerere alijiuzulu uwaziri mkuu?

Sababu kubwa aliyotoa Nyerere ya kujiuzulu kwake uwaziri mkuu ni kwenda kuimarisha chama.

Waandishi wawili, Florence Lemoine na John Strickland, katika ukurasa wa 137 wa kitabu chao, 'Government Leaders, Military Rulers, and Political Activists', wameandika kuwa "Nyerere aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Taifa hilo (Tanganyika), lakini akajiuzulu wiki chache tu baadaye kwa sababu ambazo hazikuwahi kuwekwa wazi."

Kitabu 'The Europa World Year: Kazakhstan—Zimbabwe, Book 2004', chapa ya 2004 katika ukurasa wake wa 4,094 kinasema "Nyerere alijiuzulu uwaziri mkuu wa nchi Januari 1962 ili ajitoe kwa ajili ya kukiimarisha chama."

Mwandishi wa historia, Godfrey Mwakikagile, katika ukurasa wa 28 wa kitabu chake, 'Tanzania Under Mwalimu Nyerere: Reflections on an African Statesman' aliandika Januari 22, 1962 kuwa, Alijiuzulu kama Waziri Mkuu na kumteua Rashidi Kawawa kuwa waziri asiye na wizara maalumu, kama mrithi wake.

Alisema amejiuzulu ili akakijenge chama alichosema kilikuwa kimepoteza mwelekeo.

Kitabu cha 'Yearbook of the Encyclopedia Americana' chapa ya mwaka 1965 kilichoandaliwa na Alexander Hopkins McDannald kinasema, "Nyerere alijiuzulu uwaziri mkuu ili kuongoza Tanu."

Hata hivyo, mwandishi Theodemidrovich Lugomola katika ukurasa wa 15 wa kitabu chake, 'Uhuru Ulioporwa', anasimulia kuwa kulikuwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Tanu siku 40 baada ya Uhuru wa Tanganyika.

Wajumbe walioaminiana walifanya kikao cha siri siku moja kabla ya kikao chenyewe kilichofanyika katika Hotel ya International kuzungumzia tetesi za tuhuma dhidi ya Mwalimu Nyerere za kwamba alikuwa amejengewa nyumba na Amir Jamal eneo la Kinondoni ili ampe uwaziri. Katika kualikana, mmoja wa waalikwa alikuwa Bibi Titi Mohamed.

Mwandishi huyo anadai kuwa habari hiyo ilibaki kuwa siri karibu kwa Watanganyika wote isipokuwa kwa waliokuwa wajumbe wa mkutano huo wa siri wa ndani hadi aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Katibu Mkuu wa Tanu.

Inaelezwa kuwa Kambona hakuwa kwenye mkutano huo, lakini alifikishiwa taarifa na Bibi Titi, naye akazifikisha kwa Nyerere.

Baada ya siri ya mkutano wa siri kumfikia Mwalimu Nyerere, alilazimika kujiuzulu kabla ya kutakiwa kufanya hivyo.

Madai kama hayo yaliwahi kutolewa na Oscar Kambona, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Tanu wakati Nyerere akijiuzulu.

Baada ya kurejea nchini kutoka uhamishoni ili ashiriki mageuzi ya kisiasa baada ya kuanzishwa kwa vyama vingi vya siasa, Kambona alizungumza na waandishi wa gazeti la 'Wasaa' kwa kile alichodai kuwa ni kurekebisha historia 'ambayo haikuwa sawa' kuhusu kujiuzulu kwa Mwalimu Nyerere hata baada ya kula kiapo cha kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika.

Kambona aliwaambia waandishi hao kuwa sababu ambazo historia inasema kuhusu kujiuzulu kwa Nyerere si za kweli, bali alijiuzulu kutokana na tuhuma za kupokea rushwa ya nyumba kutoka kwa Amir Jamal.

Habari hiyo ilichapwa katika toleo la pili, namba 20 la Mei 1993 katika ukurasa wa mbele, wa tano na wa 11 chini ya kichwa cha habari kinachosomeka, "Siri ya kujiuzulu kwa Nyerere yafichuka.'

Pia, mwandishi Ronald Aminzade katika ukurasa wa 108 wa kitabu chake, 'Race, Nation, and Citizenship in Post-Colonial Africa: The Case of Tanzania' anaandika "Amir Jamal alimlipia Nyerere nauli ya kwenda Umoja wa Mataifa mwaka 1955.”

Kambona alikaririwa na Wasaa akisema: "Nakumbuka, tena nakumbuka vizuri sana kuwa Nyerere hakujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 1962 kwa sababu ya kwenda kuimarisha chama cha Tanu. Fikiria Uhuru ulipatikana Desemba 9, 1961, kwenye Januari 22 Nyerere alisimama na kutamka mbele ya Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Tanu kuwa anajiuzulu uwaziri mkuu kwa sababu ya kurudi kwenye chama ili kukiimarisha.

"Sababu hiyo haiingii akilini,” alisema Kambona. “Iweje Tanu iliyokuwa na nguvu ya kumwondoa mkoloni, baada ya siku zipatazo 40 imezorota kiasi cha kuhitajika msaada wa kuimarishwa.”

Alihoji: “Yaani Tanu kilichokuwa kina mshikamano wa wananchi wote waliodhamiria kuichukua nchi yao kutoka kwenye utawala dhalimu wa wakoloni imezorota siku 40 tu baada ya kupata uhuru? Hiyo haikuwa sababu ya Nyerere kujiuzulu uwaziri mkuu, ila sababu hiyo ilitumiwa na Nyerere ili kumkinga na aibu iliyotaka kumkuta, pamoja na kuwageresha Watanzania wasifahamu ukweli halisi wa mambo."

Kambona alisema kilichomshangaza ni kwamba Watanzania wengi waliikubali sababu hiyo bila kuitafakari, na vitabu vingi vya historia viliandika juu ya sababu hiyo. Alidai kuwa yeye alikuwa Katibu Mkuu wa Tanu na Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo na kwamba alijua kuwa ukweli wa mambo haukuwa ule.

"Kikao (cha siri) kilikuwa na ushahidi wa kutosha wa kuonyesha kuwa Nyerere alijengewa nyumba na Jamal huko Magomeni, na kujengewa huko kulizaa fikra kuwa Jamal amemjengea nyumba Nyerere ili apewe uwaziri. Hivyo wajumbe kadhaa wa Halmashauri Kuu ya Tanu waliamua kuzungumzia juu ya tuhuma hizo kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya TANU uliokuwa unafanyika Januari 20, 1962.

Alisema kwa kuwa walikuwa na ushahidi, kuna wajumbe waliomba kuungwa mkono na wenzao ili wamshtaki Nyerere mbele ya Halmashauri Kuu ya Tanu iliyokuwa ikutane Jumapili iliyofuata, Januari 21, 1962.

Kambona alisema katika mazungumzo yake na Nyerere, alimuuliza kuhusu suala la kujengewa nyumba na Jamal, Nyerere alikiri.

"Nilimwambia Nyerere amwite mdogo wake, Joseph (Nyerere), ili tujadiliane jambo hilo. Joseph alipoletwa, tukawa mimi, Nyerere, Bibi Titi na Joseph. Nikamweleza Nyerere ni vyema yeye akajiuzulu mwenyewe kabla ya kulazimishwa kujiuzulu kwa tuhuma hizo, kwa hiyo mbele yetu Nyerere akakubali kujiuzulu lakini akaniuliza akishajiuzulu nani atapewa uwaziri mkuu na atatoa sababu gani ya kujiuzulu."

Kambona alidai alimwambia Nyerere kuwa wajumbe walimtaka yeye (Kambona) awe waziri mkuu, lakini akapinga hoja zao na kulikuwa na sababu nyingi za kupinga. Baada ya majadiliano ya muda fulani ndipo jina la Kawawa likaletwa.

Baada ya kumpata Waziri Mkuu, Kambona alisema, kihunzi kingine kikawa "sababu ya kujiuzulu."

"Ndipo nilimshauri Nyerere aueleze mkutano kuwa anajiuzulu kwenda kuimarisha chama cha Tanu, sababu hiyo ingekubalika kwa watu wengi. Kwa hiyo Januari 20, 1962 kwenye ufunguzi wa mkutano wa Halmashauri ya Tanu, katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano Nyerere alitangaza kujiuzulu kwa ajili ya kukiimarisha chama."

Je, sababu alizotoa Nyerere za kujiuzulu kwake ni za kweli? Ni vigumu kujua. Je, sababu alizotoa Kambona za kujiuzulu kwa Nyerere ni za kweli?


Tukutane toleo lijalo