Heche ‘awasagia kunguni’ Mawaziri, watendaji ripoti ya CAG

Mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) John Heche akifafanua jambo wakati wa mkutano wake na Waandishi wa Habari jijini Mwanza kuhusu masuala kadhaa ikiwemo Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha wa 2021/22. Picha na Mgongo Kaitira
Muktasari:
Kwa mujibu wa kanuni na maelekezo ya Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) utajadiliwa bungeni mwezi Novemba baada ya Kamati za PAC na LAAC kuifanyia kazi ikiwemo kuwapa nafasi ya kujitetea wanaotuhumiwa.
Mwanza. Mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini, John Heche amewachongea kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Mawaziri, viongozi na watendaji wa wizara, mashirika na taasisi za umma zinazotajwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akitaka wawajibishwe.
Heche ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema amemshauri Rais Samia kuanza kwa kuiwajibisha kwa kuiondoa ofisini manejimenti ya Shirika la Reli nchini (TRC) kama alivyofanya kwa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo baada ya ripoti ya CAG kuibua kashfa ya hasara ya Sh1.7 trilioni kwa kutoa zabuni bila ushindani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Jumatatu Aprili 24, 2023, Heche amesema manejimenti ya TRC haistahili kuendelea kuwepo ofisini kwa sababu siyo tu ndiyo inayoandaa taarifa na kuzitekeleza baada ya kupitishwa na bodi, bali pia ndiyo husaini mikataba ukiwemo unaodaiwa kuisababishia Taifa hasara ya Sh1.7 trilioni.
Kauli ya Heche aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) inatokana na ripoti ya CAG ya mwaka 2021/22 iliyobaini ukiukwaji wa sheria katika baadhi ya mikataba ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ikiwemo ya kipande cha Makutupora -Tabora na Tabora – Isaka iliyosababisha hasara ya Sh 1.7 trilioni baada ya kutolewa bila kushindanisha wazabuni.
“Sh1.7 trilioni ni fedha nyingi ambazo zinebadilisha maisha ya Watanzania iwapo zingeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo. Tungeboresha huduma ya maji, afya, na hata miundombinu ya barabara. Rais awawajibishe wote wanaotajwa kuhusika katika ubadhirifu huu. Fedha hizi ni jasho za walipa kodi wa nchi hii. Tusikubali zichezewe,” amesema Heche
Mwanasiasa huyo amesema kama ambavyo Bodi imewajibishwa, menejimenti ya TRC ambayo ndiyo huwajibika kwa utendaji na shughuli za kila siku unastahili kuwajibishwa.
Katika mlolongo huo, Heche amewataja Mawaziri, viongozi na watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma yanayotajwa kwenye ripoti ya CAG kuwa nao wanatakiwa kuwajibika au kuwajibishwa na mamlaka zao za nidhamu.
“Rais Samia akishindwa kuchukua hatua kwa kuwawajibisha wote wanaotajwa kwenye ripoti ya CAG, basi wananchi watachukua hatua kupitia sanduku la kura kwa kuiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachounda Serikali kwa kushindwa kuwajibika,” amesema Heche
Mjadala ripoti ya CAG bungeni
Akizungunmzia mjadala rasmi wa ripoti ya CAG bungeni na hatua dhidi ya wanaotajwa kuhusika kwenye ubadhirifu wa fedha na mali ya umma, mwansiasa huyo amema mjadala huo haustahili kusubiri hadi mwezi Novemba, bali ni vema wahusika wote ama kuwajibika au kuwajibishwa mara moja ili kuzuia uwezekano wa fedha na mali za umma kuendelea kutumika vibaya.
"Watu wafuje fedha na mali za umma leo halafu tunasubiri hadi Novemba ndipo suala lao lijadiliwe na kuwajibishwa. Huko mitaani wanaotuhumiwa kwa wizi hushughulikiwa mara moja kulingana na ushahidi uliopo. Hivyo ndivyo wanaotajwa kwenye ripoti ya CAG wanavyostahili kushughulikiwa,” amesema Heche
Ametoa mfano wa madai ya zaidi ya Sh442.1 milioni kulipwa kwa wazabuni wasio na mikataba kwa mujibu wa ripoti ya CAG, lakini wanaodaiwa kushiriki bado wako ofisini wakiendelea na kazi zao za kila siku ikiwemo kusimamia fedha na mali za umma.
Sakata la Tanga Cement
Akizungumzia sakata la ununuzi wa kampuni ya Tanga Cement, Heche ameiomba Serikali kuheshimu maamuzi ya Mahakama kwa kuzuia ununuzi huo kulinda maslahi ya umma utakaoathirika iwapo uzalishaji na biashara ya saruji utahodhiwa na kampuni moja.
“Chama cha Walaji tayari imefungua na kushinda shauri mahakamani kuhusu ununuzi huu. Sasa ni kipimo cha utii wa sheria kwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia kwa kuiagiza Tume ya Ushindani (FCC) kutekeleza amri ya Mahakama,” amesema Heche
Amesema iwapo Twiga Cement itanunua Tanga Cement, ni dhahiri ushindani katika uzalishaji na biashara ya saruji utaondolewa kwa sababu kampuni moja itahodhi soko na biashara ya bidhaa hiyo.
Sakata la ununuzi wa kampuni ya Tanga Cement liliibuka bungeni Aprili 8, 2023 baada ya baadhi ya wabunge kuhoji kwanini Serikali imeruhusu ununuzi huo utakaotoa fursa kwa kampuni moja kuhodhi biashara ya saruji nchini.
Wakijadili makadirio ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2023/24, wabunge hao walionyesha hofu yao kuwa ununuzi wa Tanga Cement kwa thamani ya Sh137 bilioni utapandisha bei ya saruji kwa mzalishaji kupata mwanya wa kupunguza uzalishaji kusababisha mahitaji makubwa kuliko bidhaa iliyoko sokoni.
Wakati mjadala huo unaibuliwa bungeni, tayari FCC ilishaidhinisha ununuzi wa kampuni hiyo kwa sharti kuwa kampuni inayoinunua Tanga Cement siyo tu haitafunga shughuli kampuni hiyo, bali pia itaendelea kuzalisha na kuitangaza chapa ya Simba Cement (Tanga Cement) na kuendeleza ajira za wafanyakazi walioko Tanga Cement.