Hiace yapinduka, yaua nane Bukoba
Muktasari:
Chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na kwamba baada ya dereva kuona gari lina hitilafu na kushindwa kulimudu, alilishusha chini kwenye mteremko mkali ng'ambo ya barabara ambako kuna shimo la maporomoko ya maji.
Bukoba. Watu wapatao nane wamepoteza maisha na wengine sita kujeruhiwa katika ajali ya gari la abiria lenye namba za usajili T.471 DCG linalofanya safari za kubeba abiria kutoka Kemondo kwenda Bukoba Mjini, baada ya gari hilo kufeli breki na kupinduka.
Ajali hiyo ilitokea Novemba 22 saa 1:45 usiku na gari hilo aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajili T. DCG lilikuwa likiendeshwa na Ismail Rashid (37) mkazi wa Kemondo.
Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo Johanes Gilbert, amesema akiwa barabarani kutokea fukwe za Ziwa Victoria kabla ya kupata ajali aliona gari ikitokea upande wa juu kushuka chini aliendelea kutembea usawa wa gari hilo ambapo baadaye alijikuta hospitali bila kujua amefikaje akiwa ameumia jicho na kidevu.
Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa Bukoba, Charles Kahigi alisema Novemba 22 usiku walipokea miili sita ya marehemu na baadaye kuongezeka wawili na majeruhi sita.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi alisema kuwa baada ya ajali hiyo watu watano walikufa papo hapo ambapo wawili walikuwa ni watembea kwa miguu na watatu walikuwa abiria na majeruhi walipelekwa hospitalini ambapo wakati majeruhi wakiwa mapokezi mmoja alipoteza maisha.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na kwamba baada ya dereva kuona gari lina hitilafu na kushindwa kulimudu, alilishusha chini kwenye mteremko mkali ng'ambo ya barabara ambako kuna shimo la maporomoko ya maji.