Prime
Hifadhi za wanyamapori za jamii hatarini kufa

Arusha. Wizara ya Maliasili na Utalii, imeshauriwa kufanya maboresho ya sheria na kanuni za maeneo ya hifadhi za wanyamapori za jamii (WMA) nchini ili kuondoa changamoto, kukimbiwa na wawekezaji na kushindwa kusimamia uhifadhi na utalii.
Kuna hifadhi za jamii za wanyamapori 38 nchini na kati ya hizo ni 16 pekee zenye wawekezaji lakini baadhi wamesitisha uwekezaji na wengine wameondoka.
Hali hiyo inatokana na baadhi ya WMA kushindwa kutimiza majukumu yake.
Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya viongozi wa hifadhi hizo, wawekezaji, wananchi na wahifadhi katika WMA za Ikona mkoani Mara, Burunge mkoani Manyara, Enduimet mkoani Arusha na Mbomipa mkoani Iringa, wamesema bila kuboresha sheria na kanuni zitashindwa kujiendesha na baadaye kufa.
Kanuni za WMA kifungu cha 59 (1) (a) hadi (d) vinaelezea uwekezaji katika maeneo ya WMA, ikitaka mwekezaji kusaini mkataba kila baada ya miaka mitano na baada ya muda wa mkataba, mali zikiwamo hoteli zinabaki kwa hifadhi.
Sheria ya fedha iliyopitishwa mwaka 2018 inaelekeza makusanyo yote ya fedha katika WMA yapelekwe Hazina.
Kauli ya Serikali
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dk Fortunata Msoffe alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia changamoto za uendeshaji wa hifadhi hizo, alishauri atafutwe mkuu wa dawati la WMA katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
“Bado nipo katika makabidhiano nina imani wizara inafanyia kazi changamoto katika WMA lakini kuna ofisa ambaye anaweza kueleza zaidi kwa sasa,” alisema.
Mkuu wa dawati la WMA katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Rose Joseph alisema hawezi kuzungumzia suala hilo bila kupata kibali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbas alisema wizara imeanza mchakato wa kuboresha sheria na kanuni za WMA.
Walichosema wadau
Mwenyekiti wa chama cha mawakala wa utalii (Tato), ambaye ni mmiliki wa hoteli na kambi za kitalii kadhaa katika maeneo ya WMA, Wilbard Chambulo alisema Serikali inapaswa kuboresha sheria na kanuni za WMA ili ziweze kufanya vizuri na kuzuia wawekezaji kuondoka katika maeneo hayo.
“Kuna shida za sheria na kanuni za WMA, mwekezaji makini anapenda kuwekeza katika eneo ambalo atakaa muda mrefu na kuna usalama wa uwekezaji wake, lakini kwa kanuni za WMA kila baada ya muda mfupi unapaswa kusaini mikataba ya kuendelea kuwekeza.
“Ikitokea baadhi ya viongozi wa WMA kushawishiwa na mwekezaji mwingine, huanzisha mgogoro kukuondoa eneo ambalo umelitunza, hii si sawa," alisema.
Anasema mwekezaji mkubwa kwa mazingira ya sasa hawezi kuwekeza katika WMA kwa kuwa hakuna usalama wa uwekezaji.
Pia alisema kuna shida kwa hifadhi hizo za jamii kushindwa kulinda maeneo yao, hivyo kuvamiwa na mifugo na majangili.
Chambulo alisema katika WMA pia kuna changamoto ya upatikanaji wa viongozi wenye sifa, akieleza baadhi hujali masilahi yao kuliko uhifadhi hatua inayochangia migogoro na hifadhi kushindwa kujiendesha.
“Kuna wajumbe ambao wanasimamia uendeshaji wa WMA, baadhi wamekuwa na changamoto, ikiwapo kutoshirikisha wawekezaji katika bajeti, kutopeleka fedha vijijini na kuingiza mifugo maeneo ya hifadhi,” alisema.
Ofisa wa kampuni ya Zara Tours iliyowekeza katika eneo la Ikona WMA, aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema mabadiliko ya mara kwa mara ya kanuni za uendeshaji wa WMA ni tatizo kwa wawekezaji na hata hifadhi.
“WMA kuna changamoto nyingi, kubwa ni kusimamia uwekezaji na uhifadhi. Pia hazina mapato ya kutosha,” anasema.
Mtafiti wa masuala ya uhifadhi, Hillary Mrosso alisema kusipofanyika maboresho ya sheria na kanuni katika WMA nyingi zitakufa.
Mrosso aliyefanya utafiti katika WMA ya Mbomipa mkoani Iringa, alisema hifadhi hizo zina matatizo katika usimamizi wa maeneo yao, upatikanaji wa fedha, kuvutia wawekezaji, kanuni na sheria zake.
“WMA zinazofanya vizuri ni za Kanda ya Kaskazini kwa sababu zinawawekezaji lakini zilizo nyingi hali yake ni mbaya,” anasema.
Katibu wa Makao WMA, Jeremiah Bishoni alisema hifadhi hizo zinakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwamo upatikanaji wa fedha za uwekezaji kwa wakati.
“Ni kweli WMA nyingi zinashindwa kufanya kazi kwa sababu fedha zinazokusanywa zote zinapelekwa Hazina na baadaye ndipo zirejeshwe, jambo hili linachukua muda mrefu, mfano sisi Makao WMA fedha za mapato ya mwaka 2023 hatujapata hadi sasa tumepata mwezi wa nne fedha za mwaka jana,” anasema.
Anasema ni vizuri Serikali kurejesha fedha za WMA kwa mkurugenzi wa wanyamapori kama ilivyokuwa kabla ya mwaka 2018 ili wapate fedha kwa wakati.
“Tumelizungumza sana hili. Fedha kuchelewa kurudishwa WMA baada ya kupelekwa Hazina huchangia kushindwa kutekeleza miradi, tunaelezwa na wizara yanatakiwa mabadiliko ya sheria ya fedha sasa hatujuwi ni lini yatapelekwa bungeni,” anasema.
Katibu wa Burunge WMA, Benson Mwaise alisema anaimani Serikali itafanya maboresho ya sheria na kanuni hizo ili kupunguza migogoro na kuzisaidia zifanye kazi kwa ufanisi.
Katibu wa Ikona WMA, Yusuph Manyanda anasema ni vigumu kupata fedha za uendeshaji na kwamba wamepeleka malalamiko ofisi ya Waziri Mkuu, kwa Spika wa Bunge na viongozi wengine bila mafanikio.
"Mwaka huu mapato yote kuanzia Januari hadi sasa hatujapata, hatuna ruzuku kutoka serikalini, hivyo kutopata fedha zetu kwa wakati kunavuruga shughuli za uhifadhi. Tunategemea fedha hizo kufanya doria, kulipa mishahara na shughuli nyingine," alisema
Jeremiah Isaya, mkazi wa Kijiji cha Tingatinga, alisema haoni sababu za uwapo wa hifadhi hizo na kuzuiwa baadhi ya maeneo kuingiza mifugo kwa kuwa hawapati fedha za kutosha.
"Kuna shida WMA, tunaona watalii wanakuja ila viongozi wanasema hakuna fedha, sijui ipo Hazina. Sasa ni bora turejeshewe baadhi ya maeneo ili tuyatumie kwa ufugaji maana hakuna faida kama zamani," anasema.