Hukumu kesi ya Sabaya yapigwa kalenda

Muktasari:

  • Hukumu ya kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili iliyokuwa itolewe leo imeahirishwa hadi Oktoba 15, 2021.


Arusha. Hukumu ya kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili iliyokuwa itolewe leo imeahirishwa hadi Oktoba 15, 2021.

Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa Oktoba mosi, 2021 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Amalia Mushi.

Sabaya na wenzake, Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, wanakabiliwa na mashtaka matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha. Inadaiwa katika shtaka la kwanza kuwa Februari 9, 2021 katika Mtaa wa Bondeni, Arusha, washtakiwa hao waliiba Sh2.769 milioni, mali ya mfanyabiashara Mohamed Saad.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa kabla na baada ya kufanya wizi huo, washtakiwa waliwashambulia Numan Jasin, Harijin Saad Harijin, Bakari Msangi, Salim Hassan na Ally Shaban kwa kuwapiga kwa kutumia bunduki, ili kufanikisha wizi huo.

Katika shtaka la pili, Sabaya na wenzake wanadaiwa kuiba Sh390,000 kutoka kwa diwani wa Kata ya Sombetini, Bakari Msangi wakiwa katika Mtaa wa Bondeni.

Walidaiwa kumfunga pingu, kumpiga na kumshambulia huku wakimtishia kwa bunduki kabla ya kufanya tukio hilo.

Sabaya na wenzake wanadaiwa katika shtaka la tatu kuiba Sh Sh35,000 na simu ya mkononi aina ya Tecno kutoka kwa Ramadhan Rashid wakiwa katika mtaa huohuo.

Baada ya kufanya wizi huo, walidaiwa kumfunga pingu na kumtishia Rashid kwa bastola.

Wanashtakiwa chini ya kifungu cha 287 (A) cha Kanuni ya Adhabu ambacho adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 30.

Chini ya kifungu hicho, mtu yeyote anayeiba kitu chochote na kutumia silaha kutishia kabla au wakati akitekeleza wizi huo atakuwa ametenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Endapo watatiwa hatiani, Sabaya na wenzake watakabiliwa na adhabu ya kifungo cha miaka isiyopungua 30 jela.

Washtakiwa hao wamekuwa rumande tangu kukamatwa kwao kwa sababu kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha halina dhamana kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Awali kesi ya kina Sabaya ilikuwa ikitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salome Mshasha lakini kuanzia Julai 18, 2021 kesi hiyo ilianza kusikilizwa mfululizo na hakimu Amworo aliyekuja Arusha akitokea Geita.