Hussein Jumbe: Nilikataliwa kuposa mke kisa uanamuziki

Saturday November 21 2020
jumbepic
By Nasra Abdallah

Hussein Jumbe ni kati ya wasanii wa muziki wa dansi ambao wanaendelea kutesa hadi sasa katika muziki huo ikiwemo kwenye kumbi mbalimbali za burudani.

Katika maisha yake, msanii huyu ameshawahi kutumikia bendi mbalimbali zikiwemo Msondo Ngoma, Sikinde, Tabora Jazz, Tanzania One Thetre(TOT) na sasa anamiliki bendi yake aliyoipa jina la Talent Band.

Jumbe amewahi kutikisa na vibao mbalimbali vikiwemo “Siri”, “Nachechemea”, na kibao cha “Ajali” alichoimba akiwa Msondo.

Hivi karibuni Mwananchi ilifanya naye mahojiano maalumu ambapo alifunguka mambo mbalimbali ikiwemo historia yake ya kimuziki, maisha yake nje ya muziki na mipango yake katika tasnia hiyo.

Historia yake katika muziki

Jumbe anasema ametokea kuupenda muziki wa dansi tangu akiwa shule ya msingi na mwanamuziki aliyemvutia ni Marijani Rajabu. Anasema alikuwa akienda kuangalia maonyesho yake baa ya Prince iliyokuwa maeneo ya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam, kwa kiingilio cha Sh5.

Advertisement

Anasema ili apate kiingilio hicho alikuwa akihifadhi fedha aliyokuwa akipewa kwa ajili ya matumizi ya shule, inapofika Jumapili anakwenda kumuona msanii huyo ambaye ameacha alama ya sanaa katika muziki wa Tanzania.

Anasema akiwa anasoma shule ya msingi alijiunga na bendi ya Ochestra Siza iliyokuwa mtaani kwao ambapo alikuwa akipiga ngoma, alipofika sekondari alichukuliwa na bendi Asilia Jazz iliyokuwa ikimilikiwa na Baraza la Muziki la Taifa (Bamuta) lakini walishindwa kumuajiri kwa kuwa alikuwa na umri mdogo.

Pamoja na kupita katika bendi mbalimbali katika safari yake ya muziki, zikiwemo Mlimani Park, TOT, Mikumi Sound, Jumbe anasema bendi aliyokaa muda mrefu ni Msondo ambapo alidumu kwa miaka 15 kuanzia mwaka 1987 hadi 1992.

“Mbali na kudumu pia niliishi kwa amani kuliko zote hii ni kutokana na kuwepo kwa uongozi bora chini ya marehemu Maalim Gurumo na Mabere Marando na meneja wa bendi Said Kibiriti” anasema.

Hata hivyo anasema kutokana na kuupenda muziki walijikuta na baba yake wakitofautiana baada ya kuacha kazi ya kiwandani aliyokuwa amemtafutia na kutimkia mkoani Tabora, ambapo alijiunga na bendi ya Tabora Jazz.

“Nakumbuka nikiwa Tabora Jazz, mwaka 1983 mwanamuziki Shem Kalenga alinisikia nikiimba katika treni, tukiwa safarini kwenda Mpanda akaniambia niachane na kupiga gitaa badala yake niimbe.

“Alitunga wimbo wa “Mwanzo wa Mwanadamu” na kunipa nafasi kubwa kuuimba na safari yangu ya kuimba ikaanzia hapo na bendi mbalimbali zilinichukua kwa ajili hiyo,” anasema.

Alikataliwa kuoa kisa kuwa mwanamuziki Wakati akijivunia kuwa mwanamuziki, Jumbe anasema huwa anawachukia watu wanaochukulia muziki kama uhuni.

Anasema jambo hilo lilishawahi kumpa shida katika maisha yake, ambapo alifika hatua ya kukataliwa kuposa kutokana na kufanya kazi hiyo.

Jumbe alimposa Zakia Hussein miaka 27 iliyopita, ambaye ndiye mkewe huku akisema hawajawahi kupelekana hata kwa mjumbe kushtakiana, licha ya kuwa ni mwanamuziki.

Hata hivyo anasema anashukuru pamoja na ndugu hao kumkazia, mke wake aliamua kusimamia msimamo wake kwamba ataolewa naye na hatimaye wapo naye hadi leo huku wakijaliwa kupata watoto wanne.

“Wakati ule kutokana na dhana ya muziki ni uhuni, hakuna mzazi aliyekubali mwanaye aolewe na msanii, kama si mke wangu nilikuwa nimeshamkosa baada ya familia yake kukataa posa yangu,” anasema Jumbe.

Anasema amefanikiwa kudumu katika ndoa na mkewe kwa sababu ya kutumia maneno matatu ambayo ni pole, samahani na asante.

“Wanandoa wengi wanashindwa kuyatumia ipasavyo maneno haya na kuzigharimu ndoa zao,” anasema huku anacheka.

“Kuishi kwetu ndani ya ndoa kwa miaka 27, kumeondoa dhana ya muziki ni uhuni, hata baadhi ya ndugu zake wanajifunza kwetu,” anasema.

Azunguzmia mauzauza anayopitia katika maisha yake

Anasema katika safari yake ya muziki amekuwa na changamoto nyingi ikiwemo kuumwa mara kwa mara tena magonjwa ya mauzauza.

“Nilishawahi kutokewa na mauzauza mengi, kuna siku katika kipaza sauti ninachotumia kuimba kulikuwa na mjusi na kali ni hii nimeota napigana na kuku hadi kuvunjika vidole vinne.

“Hata hivyo kwangu kila linalonitokea nachukua ni mipango ya Mungu, hivyo ninachokifanya ni kuomba dua ili yaniepuke mabalaa ya aina hii,” anasema.

Advertisement