Huyu ndiye Ummy Mwalimu aliyedumu baraza la mawaziri kwa miaka 14
Muktasari:
- Alianza akiwa Naibu Waziri kisha kupandishwa kuwa waziri. Amehudumu kwa marais watatu mfululizo, Jakaya Kikwete, John Magufuli na Samia Suluhu Hassan.
Dar es Salaam. Usiku wa Agosti 14, 2024 unaweza usisahaulike haraka katika maisha ya kisiasa ya Ummy Mwalimu.
Hii inatokana na uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kumweka kando katika mabadiliko madogo aliyoyafanya katika Baraza lake la Mawaziri.
Ummy ambaye ni Mbunge wa Tanga Mjini (CCM) ni miongoni mwa mawaziri wachache waliodumu katika Baraza la Mawaziri kama wawaziri kamili kwa takribani miaka tisa mfululizo. Alihama kutoka hapa kwenda pale.
Ukijumuisha miaka tisa ya uwaziri na miaka mitano ya naibu waziri kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, Ummy anakuwa na miaka 14 ndani ya baraza la mawaziri akihudumu katika tawala tatu. Ya Jakaya Kikwete, John Magufuli na sasa ya Samia Suluhu Hassan.
Ummy amekuwa mmoja wa mawaziri waliohudumu Wizara ya Afya kwa kipindi kirefu na ndani ya utawala wa awamu ya tano ulioingia madarakani Novemba 5, 2015 ulipounda Serikali Desemba mwaka huo hadi ulipokoma Machi 17, 2021 alikuwa wizara hiyo.
Huo ulikuwa utawala wa Rais John Magufuli ambaye alifariki dunia Machi 17, 2021 na nafasi yake kushikwa na Samia ambaye wakati huo alikuwa Makamu wa Rais.
Katika utawala wa Magufuli, Ummy ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alikuwa miongoni mwa mawaziri sita ambao hawakuwa wanaguswa kwenye panga pangua.
Wengine ambao hawakuguswa na wizara zao kwenye mabano ni, Jenista Mhagama (Sera, Bunge, Uratibu), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu), William Lukuvi (ardhi) na Dk Philip Mpango (Fedha na Mipango) na Dk Hussein Mwinyi wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Kwa sasa Dk Mpango ni Makamu wa Rais wa Tanzania na Dk Mwinyi ni Rais wa Zanzibar.
Ummy aliyezaliwa Septemba 5, 1973 alikuwa sehemu ya baraza la kwanza la Magufuli alilolitangaza Desemba 10, 2015 alipoteuliwa kuwa Waziri wa Afya.
Miongoni mwa mambo ambayo yatakumbukwa katika uongozi wake, ni pamoja na namna alivyopambana na mlipuko wa Uviko-19 mwaka 2020.
Mlipuko huo wa kidunia ulisababisha vifo na kuathiri shughuli mbalimbali za uzalishaji na maendeleo.
Safari ilivyoanza
Ummy alichaguliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum wa Wanawake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, nafasi ambayo aliitumikia hadi mwaka 2015.
Akarudishwa tena bungeni katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kupitia tiketi ya CCM Viti Maalum kwa mara nyingine kabla hajagombea jimbo la Tanga Mjini mwaka 2020 na kutangazwa mshindi.
Ummy Mwalimu ameshika nafasi mbalimbali katika ulingo wa siasa. Mwaka 2015 alikuwa mjumbe wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na mwaka 2014 hadi 2015 alikuwa mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Amewahi kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Mazingira na mwaka 2010 hadi 2014 alikuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto.
Mwaka 2014 alikuwa Naibu Waziri wa Sheria na Katiba nafasi aliyohudumu mpaka mwaka 2015.
Mwaka 2015 mwishoni aliteuliwa kuwa Waziri kamili katika Wizara wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mwaka 2021 aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, kuwa waziri katika Wizara ya Nchi Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kabla ya kurejeshwa tena afya.
Januari 8, 2022 Rais Samia alimrejesha Ummy Mwalimu kuwa Waziri wa Afya baada ya kutenganisha wizara hiyo na kuunda wizara mpya ya Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, inayoongozwa na Waziri Dorothy Gwajima ambaye alikuwa Waziri wa Afya.