Ipo haja wazazi kuwaambia ukweli watoto kuhusu ubakaji na ulawiti

Muktasari:

Nimekuwa nikisikia hili suala la wazazi kuzungumza na watoto wao, lakini sikuwahi kulifuatilia kwa kuwa mtoto wangu ndiyo kwanza ana miaka sita. Sikuwahi kuona kama kuna kitu cha maana kinachoweza kutuweka chini kuzungumza zaidi ya kumtuma lete hiki na kile na kumsaidia kazi zake za shule.

Nimekuwa nikisikia hili suala la wazazi kuzungumza na watoto wao, lakini sikuwahi kulifuatilia kwa kuwa mtoto wangu ndiyo kwanza ana miaka sita. Sikuwahi kuona kama kuna kitu cha maana kinachoweza kutuweka chini kuzungumza zaidi ya kumtuma lete hiki na kile na kumsaidia kazi zake za shule.

“Ila baada ya kusikia mfululizo wa matukio ya watoto kubakwa na kulawitiwa, moyo ukanisukuma kuongea naye, ili kumuelekeza jinsi ya kukabiliana na hatari yoyote inayoweza kuwa mbele yake na kumsababishia kufanyiwa vitendo vya ukatili. Hakika nilishtushwa na namna alivyoelewa kwa haraka kile nilichomuelezea, huku akinipa stori za wanafunzi wenzake ambao inadaiwa wamefanyiana vitendo hivyo”.

Hiyo ni kauli ya Faraja Mhagama, mama ambaye hakuwahi kuelewa umuhimu wa kuzungumza na mtoto wake, lakini amesukumwa kufanya hivyo baada ya kukithiri kwa matukio ya ubakaji na ulawiti ambayo yanaendelea kuripotiwa kila kukicha kwenye vyombo vya habari.

Wiki hii iliyoisha katika mahakama mbalimbali nchini zimesikilizwa kesi za ubakaji na ulawiti, nyingine zikitolewa uamuzi huku zikiripotiwa kesi mpya, ikiwemo la padri aliyepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuwanajisi watoto watatu huko mkoani Kilimanjaro.

Wakati matukio haya yakiendelea kuwa mengi, imebainika yanachangiwa na watoto kutokuwa na elimu ya kutosha na sahihi kuhusu vitendo hivi na matokeo yake wamekuwa wakishambuliwa na kutishiwa kuuawa wao au wazazi wao pale watakaposema kuhusu ukatili waliofanyiwa.

Kati ya watoto wanaonajisiwa au kubakwa, mara nyingi wengi wao hufanyiwa vitendo hivyo zaidi ya mara moja, lakini hushindwa kutoa taarifa kwa kuhofia au kutojua kwamba kitendo alichofanyiwa ni kibaya na kina madhara makubwa kwake.

Kilichomshtua Faraja ni matukio ya aina hiyo kuhusisha watu wa karibu na wanaoaminiwa zaidi kwenye jamii, hali ambayo inamfanya aone kuwa watoto hawako salama, hivyo nguvu na maarifa ya ziada yanahitajika katika kuwalinda.

Anasema: “Kiukweli haya matukio ninavyoyasikia kila siku nakosa amani, hofu inakuwa kubwa zaidi nikisikia wanayofanya haya na wazazi, ndugu, walimu, madereva wa magari ya shule, mbaya zaidi tunasikia hadi viongozi wa dini. Mbona hawa ndio tulikuwa tunawaamini katika malezi ya watoto wetu?”

Mama huyu anaeleza kuwa baada ya kutafakari kwa kina akaona njia sahihi ya kupunguza wasiwasi wake ni kuzungumza na mwanaye, ili ikitokea anakutana na mazingira ya aina hiyo ajue jinsi gani ya kujisaidia au kutoa taarifa kwa haraka kuwezesha hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mhusika.

“Tofauti na nilivyofikiria kwamba mtoto anaweza kupata wakati mgumu kuelewa kile nilichokuwa namwambia au atakuwa na maswali mengi, alinistaajabisha kwa kuelewa haraka zaidi na kadiri nilivyojishusha kwake na kutaka afunguke zaidi alinieleza kila anachofahamu.

“Kengele ikagonga kichwani mwangu kwamba huwa tunahofia au hatuna muda wa kuzungumza na watoto, ila wanafahamu vitu vingi na maswali mengi vichwani mwao sasa ni uamuzi wetu kuamua kuwapatia majibu sahihi au wakatafute majibu kwa watu wabaya,” anasema.

Gervas Deusdedith, baba wa watoto wawili anaeleza wasichoelewa wazazi wengi ni kwamba watoto wa sasa wana uelewa mkubwa na wanaweza kufanyia kazi kile kinachoingizwa kwenye ubongo wao bila kujali kuwa kina faida au hasara kwao.

“Ninachokiona ni sisi wazazi tunafanya makosa tukiamini watoto wa sasa ni kama tulivyokuwa sie, ukweli ni kwamba hawa watoto wanaelewa mno tukiwapa nafasi ya kuelewa. Sasa hivi mambo yanayohusu ngono yamerahisishwa kuanzia kwenye mazungumzo hadi ufanyaji kiasi kwamba ni kitu cha kawaida kwa mtoto mdogo kuelewa mtoto anapatikanaje.

“Sasa kuwasaidia wasiingie mikononi mwa watu wabaya ni lazima tuzungumze nao kwa uwazi kabisa, umuelezee ukiona mtu anakwambia hivi kimbia au piga kelele. Unapozungumza naye kuhusu ubakaji mueleze kabisa unafanyikaje na afanye nini akikutana na mtu mwenye nia ya kumfanyia hivyo au akifanikiwa afanye nini, tusizungumze kwa kufichaficha ndio maana hawa wabakaji wanaendelea kufanya uchafu wao.”

Hilo linaelezwa pia na mwanasaikolojia Deogratius Sukambi, anayesema wakati mwingine mambo haya yanatokea kwa sababu wazazi wameshindwa kuendana na kasi ya mabadiliko ya mazingira, hali inayotoa mwanya kwa watoto kujifunza vitu visivyofaa.

Anasema changamoto iliyopo ni wazazi kuendelea kutumia mfumo wa malezi wa miaka mingi iliyopita ambayo hakukuwa na teknolojia, televisheni wala tamthiliya ambazo watoto wanaziangalia kwa sasa.

“Watoto katika umri wa miaka minne hadi 17 wanakuwa kwenye umri wa udadisi wa kila wanachokiona na kusikia, bahati mbaya siku hizi wazazi hawana muda wa kuwasaidia kupata tafsiri ya vitu hivyo au wanakwepa kutoa ufafanuzi, au wanaona sio wajibu wao.

“Mtoto anaweza kuingia kwenye simu na kukutana na vitu vingi, anaachwa peke yake anaangalia tamthiliya na kukutana na vitu vingi ambavyo vina uhusiano na masuala ya ngono. Hii inamfanya kuwa na maswali mengi yenye udadisi na anakosa majibu yake. Anapokwenda huko shule anakutana na watoto wenzake ambao wana mawazo kama yeye, hivyo wanashawishika kuvifanyia majaribio,” anasema.

Anachozungumzia Sukambi ni mfano wa tukio lililotokea hivi karibuni mkoani Iringa ambapo mtoto wa miaka 13 alikutwa na hatia ya kumbaka mtoto mwenzake mwenye umri kama huo na kuadhibiwa kwa kuchapwa viboko sita, hii ni kwa mujibu wa sheria ya mtoto inavyoelekeza.

Kwa upande wake, mwanasaikojia Lucy Noel anaeleza kwamba kuna uwezekano mkubwa wa mtoto kuweka kichwani kitu anachoambiwa na mzazi wake kwa kuwa ni mtu wa kwanza anayemuamini endapo atakuwa na ukaribu naye.

Anasema pindi mzazi atakapokuwa na ukaribu wa kuzungumza na mtoto wake atamjengea hali ya kujiamini na kuwa mwepesi wa kumshirikisha kila anachokutana nacho, hata kama kuna vitisho na ukatili anafanyiwa.

“Mtoto ukizungumza naye kwa uwazi kulingana na umri wake hata yeye atakuwa muwazi kwako, nasema hivi kwa sababu kuna matukio tunayasikia mtoto amekuwa akinajisiwa au kubakwa zaidi ya mara moja, lakini hajawahi kutoa taarifa huenda ni kwa sababu ya vitisho anavyopata kwa anayemfanyia vitendo hivyo au huna muda naye kiasi kwamba hajui wapi aanzie,” anasema Lucy.