Je, chanjo hizi zitatulinda na covid 19?

Muktasari:
- Gumzo kubwa mitandaoni na mitaani ni kuhusu kutua kwa chanjo ya kukabiliana na janga la Covid-19 ya Covax kutoka Marekani ambazo tayari Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima ameeleza kuwa ni salama.
Gumzo kubwa mitandaoni na mitaani ni kuhusu kutua kwa chanjo ya kukabiliana na janga la Covid-19 ya Covax kutoka Marekani ambazo tayari Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima ameeleza kuwa ni salama.
Tanzania ina wanasayansi wabobezi wa kutosha katika vyuo vya tiba, hospitali kubwa na taasisi kubwa za ndani na nje zinazofanya utafiti mbalimbali wa magonjwa, ikiwamo ile ya taifa, yaani NIMR.
Na hata vituo vya utafiti vilivyopo vimesheheni vifaa vya kisasa vinavyotafiti magonjwa ambavyo vinashirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na taasisi nyingine za kimataifa.
Uwepo wa chanjo ya corona nchini Tanzania ni dhahiri usalama kwa watumiaji umezangatiwa, ingawa madhara machache ya kawaida hayakwepeki.
Taarifa za machapisho ya karibuni yaliyotolewa na WHO na vituo vya kimataifa vya udhibiti wa Magonjwa kama CDC cha Marekani vinathibitisha kuwa chanjo hizi ni salama na madhara machache yanayojitokeza hayaondoi faida kubwa ya kuzitumia.
Chanjo ni mchakato wa kisayansi ambapo mfumo wa kinga unaimarishwa dhidi ya uvamizi wa vimelea au sumu za vimelea ambavyo huweza kuleta uchokozi kwa kinga ya mwili.
Mfano mwili utakapokutana na kitu hicho kigeni kwa mara ya kwanza kinga ya mwili hujibu mapigo kwa kutiririsha askari wake ambao huweza kukitambua, kutunza kumbumbuku na hatimaye kukiangamiza.
Kinga huwa na tabia ya kuzalisha askari ambao watakuwa ni kwa ajili ya kukabiliana na kitu hicho kwa muda mrefu na huku pia ikijiimarishia uwezo wa kukabiliana na kitu hicho hapo baadaye.
Pale itakapotokea kitu hicho kikavamia tena mara ya pili huweza kuangamizwa kwa haraka na kwa ufanisi zaidi kuliko hapo awali.
Hapa utaona kuwa mfumo wa kinga ya mwili una hatua kuu tatu, ikiwamo kukibaini kitu, kuangamiza na kuweka kumbukumbu.
Ingawa unaweza kuchanjwa na ukapata maambukizi, lakini yanakuwa si makali yakilinganishwa na asiyechanjwa.
Kwa mujibu wa WHO, inaonyesha kupata dozi mbili za chanjo ya AstraZeneca na Pfizer-BioNTeck kunaifanya kinga ya mwili kuwa imara na kukabiliana na aina ya virusi Delta na Alpha vya wimbi la tatu.
Hapa tunapata picha kuwa ni salama zaidi kwa yule aliyechanjwa kuliko yule ambaye hajachanjwa.
Kuna vitu vingi vinavyowafanya wanadamu kuwa na kinga imara au mafanikio ya chanjo yanategemea na vitu kama hali ya hewa au mazingira ya kijiografia, vina vya urithi, hali ya kinga, umri, jinsia, tabaka la mtu, umri, uwepo wa magonjwa mengine, lishe, hali ya kiuchumi ya mhusika na eneo lake na mfumo wa matibabu.
Hivi ni vitu ambavyo vinaweza kumfanya mtu kuwa na mapokeo mazuri au mabaya ya chanjo au kuugua na kupata madhara.
Tayari pia tamko limetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa kuchanja ni hiari, Rais amechanjwa Julai 28, hivyo ni dhahiri usalama wa chanjo hizo ni mkubwa.
Tusubiri tuone kama chanjo hizi zitatupa kinga salama katika wimbi la tatu la coroa.
Katika jamii wapo wanaotumia tiba asili na mbadala kukabiliana na virusi vya mafua makali, ila ni muhimu kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya. Endelea kujikinga kwa kuvaa barakoa katika mikusanyiko na kunawa mikono na maji tiririka na sabuni au kitakasa mikono.