Jela miaka 20 kwa kukutwa na silaha iliyotengenezwa kienyeji

Watuhumiwa wa makosa mbalimbali  Kiteto wakiwa kwenye gari la Polisi Kiteto kupelekwa Mahabusu wakitokea mahakama ya Wilaya ya Kiteto hii leo Aprili 19, 2023. Picha na Mohamed Hamad Kiteto.

Muktasari:

  • Simongo Kibindia (35) mkazi wa Kijiji cha Enguserosidani wilayani Kiteto amehukumiwa adhabu ya miaka 20 jela kwa kukutwa na silaha iliyotengenezwa kienyeji aina ya gobole.

Kiteto. Mahakama ya wilaya ya Kiteto imemtia hatiani  Simongo Kibindia (35) mkazi wa Kijiji cha Enguserosidani miaka 20 jela kwa kosa la kukutwa na silaha iliyotengenezwa kienyeji aina ya gobole kinyume cha sheria.

Hakimu mkazi wa mahakama ya Wilaya ya Kiteto Boniphace Lihamwike hii leo Aprili 19.2023 ametoa hukumu hiyo ya kifungo cha miaka 20 jela kwa Simon Kibindia (35) kwa kukutwa na silaha aina ya gobole lililotengenezwa  kinyume na kif cha 20(1) na (2) sheria ya silaha na milipuko.

"Polisi Dongo wakiwa doria walimkamata Simon Kibindia (35) akiwa nyumbani kwake Kijiji cha Enguserosidani na silaha aina ya gobole lililotengenezwa kienyeji na kufikishwa polisi Kiteto na baadaye mahakamani," amesema.

Alisema mtuhumiwa alikutwa na silaha hiyo Februari 21.2022 na kufikishwa Polisi na baadaye Mahakama ya Wilaya ya Kiteto ambayo ilipata kibali cha kusikiliza kesi hiyo kutoka kwa Mwendesha Mashataka Mkuu wa Serikali DPP.

Hata hivyo mtuhumiwa aliposomewa shitaka lake alikiri kukutwa na silaha hiyo aina ya gobole iliyotengenezwa kienyeji akiwa nyumbani kwake

Hakimu Boniphace Lihamwike alimuuliza mshitakiwa kama kweli alikuwa na silaha hiyo na kukiri kisha kumweleza baada ya kukiri kinachofuata ni kupatiwa adhabu.

Mwendesha mashtaka wa olisi Salumu Issa alipoulizwa kama mtuhumiwa huyo ana rekodi ya makosa mengine yeye alisema hana kisha kumwomba Hakimu wa Mahakama hiyo Lihamwike kutoa adhabu kali kwa wenye tabia za kumiliki silaha kama hiyo kinyume cha sheria.

"Vitendo vya watu kukutwa na silaha Kiteto kinyume cha sheria tena zilizotengenezwa kienyeji kama bastola, raifo na magobole wanaendelelea na ili iwe fundisho mtuhumiwa apatiwe adhabu kali," amesema.

Mtuhumiwa alipoambiwa ajitetee aliomba huruma ya hakimu kuwa yeye hakuwa anajua kama kumiliki silaha hiyo ni kosa, kuhusu mwedesha mashtaka wa Serikali akisema kutojua sheria sio kinga ya mtuhumiwa kutopata adhabu mahakamani.