Jenereta chanzo huduma kusimama KCMC, wagonjwa wahaha
Muktasari:
- Baadhi ya huduma za matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC zimesimama kwa muda usiojulikana na kuzua taharuki kwa wagonjwa ambao wamefika hospitalini hapo tangu asubuhi.
Moshi. Baadhi ya huduma za matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC mkoani Kilimanjaro zimesimama kwa muda usiojulikana na kuzua taharuki kwa wagonjwa ambao wamefika hospitalini hapo leo asubuhi Jumanne Agosti 22,2023.
Kusimama kwa huduma hizo kumetokana na kukatika kwa umeme huku jenereta la hospitali hiyo nalo likipata hitilafu na kushindwa kufanya kazi.
Hali hiyo imetokea ikiwa ni saa chache tangu Shirika la umeme Tanzania (Tanesco) leo kutoa taarifa kwa umma kuwa kuna hitilafu ya mfumo katika kituo cha uzalishaji umeme wa gesi cha Ubungo II.
Taarifa hiyo ambayo imetolewa na Kurugenzi ya mawasiliano na Uhusiano makao makuu imeeleza kuwa hitilafu hiyo imesababisha upungufu ya uzalishaji wa umeme kwa jumla ya Megawati 268 kutokuwa kwenye mfumo wa usafirishaji wa umeme na kwamba baadhi ya maeneo kwenye mikoa nchini yatakosa huduma ya umeme kwa nyakati tofauti.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wagonjwa, ndugu na jamaa waliopeleka wagonjwa wao hospitalini hapo wamesikitishwa kukosekana kwa huduma katika hospitali hiyo kubwa na kudai kuwa ni uzembe.
Dementria Joseph, mmoja wa wagonjwa waliofika hospitalini hapo, amesema tangu hajafanikiwa kupata huduma zaidi ya kuambiwa subiri bila mafanikio.
"Wanapaswa kuwa na jenereta lenye uwezo mkubwa wa kuendesha mitambo mikubwa ya mashine za hospitali.
"Nimefika hapa hospitalini tangu asubuhi sijapatiwa huduma yoyote nimeambiwa huduma hamna kwa sababu ya kukosekana kwa umeme, nikaambiwa nisubiri nimekaa mpaka saa saba hii naambiwa niende nyumbani nirudi kesho, kwa kweli hali hii imetuumiza sana maana hospitali kubwa kama hii kukosa umeme ni fedheha,"amesema.
Alipotafutwa mkurugenzi mtendaji wa KCMC, Profesa Gileard Masenga, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema jenereta la hospitali hiyo lilipata hitilafu lakini linafanyiwa matengenezo.
"Ni kweli kuna changamoto ya umeme na hili linafahamika ni la maeneo mengi, wakati tukiendelea kutoa huduma jenereta letu kubwa lilileta shida baada ya kupata hitilafu na tatizo linashughulikiwa,"amesema Profesa Masenga