Jeshi la Polisi lapiga marufuku kumiliki gobore, laruhusu Shortgun
Muktasari:
- Jeshi la Polisi nchini limetahadharisha mambo matano kuhusiana na umiliki wa silaha, kampuni binafsi za ulinzi, wanaomiliki silaha za mirathi pamoja na silaha zaisizolipiwa leseni wapewa muda kujisalimisha.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limepiga marufuku kampuni binafsi za ulinzi zinazotumia silaha zilizotengenezwa kienyeji (Gobore), badala yake imeshauriwa kufuata utaratibu wa kisheria wa kumiliki silaha aina ya “shotgun” kwani ndizo zinazoruhusiwa kutumika kwa shughuli za ulinzi.
Pia, Jeshi la Polisi linawakumbusha wananchi kusalimisha silaha zilizokuwa zinamilikiwa kihalali na ndugu zao ambao kwa sasa ni marehemu ili silaha hizo zisilete madhara katika jamii.
Taarifa iliyotolewa kwa umma leo Ijumaa Juni 28, 2024 na Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime, inahusu masuala matano yanayohusiana na umiliki wa silaha.
Katika taarifa hiyo, Jeshi la Polisi limetoa muda wa miezi miwili kuanzia Julai Mosi hadi Agosti 31, 2024 kwa kampuni binafsi za ulinzi na baada ya kipindi hicho, msako mkali utaanza na atakayebainika akimiliki silaha hizo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mbali na kampuni za ulinzi, pia, jeshi hilo limewataka wanaomiliki silaha za mirathi kutambua kuwa kuendelea kuhifadhi silaha hizo nyumbani ni kinyume cha sheria na yeyote atakayepatikana atakuwa ametenda kosa endapo atapatikana na hatia.
“Siku za karibuni, Jeshi la Polisi limebaini kuwepo kwa baadhi ya kampuni binafsi za ulinzi ambazo zinamiliki silaha aina ya gobore bila kuwa na vibali, kinyume na utaratibu wa sheria inayozitaka kampuni za ulinzi kumiliki Shortgun kwa ajili ya shughuli za ulinzi,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa upande wa wamiliki wa silaha wasiolipia ada za leseni zao, jeshi hilo limetoa miezi mitatu kuanzia Julai Mosi, 2024 hadi Septemba 30, 2024 ili kuwapa nafasi wananchi wanaomiliki silaha kulipia ada na madeni ya leseni zao.
Hata hivyo, taarifa hiyo imebainisha kuwa wapo baadhi ya wamiliki wa silaha ambao wamekuwa hawalipii leseni zao kwa miaka kadhaa bila kuwa na sababu za msingi.
“Kwa mujibu wa kanuni namba 16 na 20 ya Kanuni za Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Risasi za Mwaka 2016, mmiliki wa silaha anapaswa kulipia ada ya leseni yake kila ifikapo Julai kila mwaka.
“Baada ya muda huo kupita, wamiliki ambao watakuwa hawajalipa ada ya mwaka 2023/2024 pamoja na madeni ya ada za miaka ya nyuma watafutiwa leseni zao kwa mujibu wa kifungu cha 8 (1) (b) cha Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Risasi ya Mwaka 2015,” amesema.
Kuhusu umiliki wa silaha bandia (toy guns) haziruhusiwi kumilikiwa na mtu, taasisi au kampuni yoyote kwa mujibu wa kifungu cha 70 cha Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Risasi ya Mwaka 2015.
“Zuio la umiliki wa silaha hizi umetokana na ukweli kwamba ni kinyume cha sheria na kwamba silaha hizo zimeshawahi kutumika katika kutenda uhalifu hasa unyang'anyi wa kutumia silaha, hivyo wananchi wote wanaomiliki silaha bandia wazisalimishe katika vituo vya Polisi kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
Amesema hivi karibuni kumeibuka baadhi ya wananchi kutaka kuingiza nchini silaha zisizo na maafa kwa ajili ya kuendesha michezo ya ulengaji shabaha.
“Hivyo, Jeshi la Polisi linawataka wananchi watambue kuwa silaha zisizo na maafa haziruhusiwi hapa nchini isipokuwa kwa kibali maalumu.
“Kwa mantiki hiyo Jeshi la Polisi, halitasita kumchukulia hatua za kisheria mtu yeyote au kikundi cha watu watakaopatikana wakimiliki silaha hizo kinyume cha sheria ikiwa ni pamoja na kukiuka maelekezo yaliyotolewa kwenye namba moja hadi tano hapo juu,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika maonyesho ya 48 ya Sabasaba ya mwaka huu, Jeshi la Polisi litakuwa na dawati la umiliki wa silaha ambapo wamiliki wa silaha watapewa namba za malipo kwa ajili ya kulipia ada pamoja na madeni ya leseni kulingana na kiasi wanachodaiwa.