Jinsi TADB inavyo chochea Taifa kuwa na utoshelevu wa chakula

Muktasari:
- Ripoti ya Shirika la kimataifa la chakula na kilimo (FAO, 2018) inabainisha kuwa ifikapo mwaka 2050, ziada ya asilimia 60 ya chakula itahitajika ili kukidhi mahitaji ya watu. Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 dunia itakuwa na watu wapatao bilioni 9.8.
Ripoti ya Shirika la kimataifa la chakula na kilimo (FAO, 2018) inabainisha kuwa ifikapo mwaka 2050, ziada ya asilimia 60 ya chakula itahitajika ili kukidhi mahitaji ya watu. Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 dunia itakuwa na watu wapatao bilioni 9.8.
Kwa ongezeko hili la watu duniani, kwa pamoja mataifa yanatahadharishwa kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha kwa pamoja janga la njaa linatokomezwa, kuhakikishaongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula, kupunguza upotevu wa chakula na kuwa na utoshelevu na usalama wa chakula.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ni moja ya taasisi muhimu nchini katika kuwezesha mafanikio ya jitihada za Taifa katika kuwezesha nchi kuwa na uhakika na usalama wa chakula. Kwa kutambua uhitaji wa mitaji katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya Kilimo, TADB ilianzishwa kama chombo kitakacho chagiza upatikanaji wa mitaji na kuwa chachu katika kufikia mapinduzi ya kilimo.
“Kwa kuzingatia dhana ya uwepo wa benki yetu ya maendeleo ya kilimo Tanzania, waasisi walitambua umuhimu wa kuchagiza mapinduzi katika kilimo, uvuvi na mifugo kwa kuanza na kuangalia upatikanaji wa mitaji katika kuzalisha mazao ya chakula. Sekta hizi ni muhimu katika juhudi za nchi kuwa na uhakika wa chakula. Hivyo, kama taasisi, tumekuwa na njia mbalimbali za kuwezesha nchi yetu kuwa na uhakika wa chakula,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege.
Kupitia ripoti na tafiti mbambali ambazo TADB imezifanyia kazi, baadhi ya mambo yanayobainishwa kama changamoto katika kuwezesha Taifa kuwa na uhakika wa chakula ni pamoja na; kasi ya ongezeko la watu, upatikanaji wa mitaji, matumizi hafifu ya kilimo cha umwagiliaji na kutokuwa na matumizi ya teknolojia sahihi katika kilimo. Changamoto nyingine ni pamoja na; ubora wa mbegu, upatikanaji wa pembejeo na upotevu wa mazao.
Uwezeshaji mitaji katika sekta ya chakula.
Zaidi ya asilimia 35 ya Sh99.4 bilioni ya mikopo ya TADB imeelekezwa moja kwa moja kwenye minyororo ya thamani ya mazao ya chakula. Ambapo asilimia zaidi ya asilimia 8 imeelekezwa katika pembejeo kama vile mbegu bora, mbolea na viwatilifu.
“Matumizi ya mbegu bora katika kilimo ni jambo muhimu sana. Hata kuwa na mbegu bora ya ng’ombe, kuku au mbuzi ni jambo linalochagiza ongezeko la chakula nchini,” anasema Nyabundege.
Pamoja na kuwezesha mitaji miongoni mwa wakulima na miradi ya kilimo cha mazao ya chakula, TADB pia imeshirikiana na taasisi mbalimbali kama Wakala wa Mbegu (ASA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) n.k ili kuchochea kuongeza uzalishaji wa mbegu bora. Kwa ushirikiano kama huu TADB inasaidia ongezeko la upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima chini.
Kilimo cha umwagiliaji
TADB imewezesha zaidi ya Sh9 bilioni katika kuwezesha kilimo cha umwagiliaji. Mabadiliko ya tabia nchi yameathiri kiwango cha upatikanaji wa mvua na kubadili muundo uliozoeleka wa hali ya hewa. Kumekua na baadhi ya maeneo yakikabiliwa na vipindi virefu zaidi vya jua na hivyo kupelekea ukame, baadhi ya maeneo yakipata mvua chache zaidi, na mengine kupata mvua nyingi zaidi ya inayohitajika. Mabadiliko haya yamechangia kupunguza mavuno ya mazao ya chakula katika baadhi ya maeneo.
“TADB imeona fursa ya kuwezesha wakulima kuendelea kuzalisha pasi kutegemea mvua kwa kuwezesha miundombinu inayowezesha kilimo cha umwagiliaji. Kwa kuboresha miundombinu hii tumeweza kuwa na uhakika wa mazao kama ya mpunga yanayozalishwa kwenye skimu za umwagiliaji kama vile skimu ya umwagiliaji Mombo, chama cha wakulima na Umwagiliaji Ruvu (CHAURU) ambapo zaidi ya wakulima wadogo 1,500 wanalizalisha mpunga,” anasema Nyabundege.
Uhifadhi na uchakataji wa mazao ya chakula
Wakati Taifa likijizatiti kuwa na uhakika wa chakula, upotevu wa mazao nao unabainishwa kuwa moja ya changamoto katika kufikia lengo hilo. Upotevu wa mazao ya chakula huchangia upungufu wa mavuno na kupunguza ubora wa mazao na virutubisho katika mazao. Ripoti ya shirika la kimataifa la IITA inaonesha kuwa Tanzania hupoteza asilimia 25 ya mazao wakati wa mavuno na kupoteza asilimia 15 ya mavuno kwa kutokuwa na uhifadhi bora.
Kwa kutambua haya, TADB imewezesha jumla ya Sh 3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa maghala yenye uwezo wa kuhifadhi mazao zaidi ya tani 50,000. Pamoja na kujenga maghala ya kuhifadhi chakula, benki imewezesha zaidi ya Sh100 bilioni iliyokwenda katika viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali kama vile mahindi, maziwa, nyama na samaki.
“Kupitia mfumo wa kuunganisha wadau muhimu katika mnyororo wa thamani (IVCF model) TADB imewaunganisha wakulima wadogo na wachakataji wa mazao ilikuhakikishia wa zalishaji masoko na pia kupunguza upotevu wa mazao kutokana na kuharibika wakati wa kuhifadhi.
Kwa kuongeza thamani ya mazao ya chakula tunawezesha chakula kuhifadhiwa kwa ubora zaidi na hivyo kufaa kwa matumizi ya muda mrefu,” anasema Nyabundege.
Zana bora za kisasa
Kama ilivyo muhimu kuwa na simu ya kiganjani katika zama hizi za kidigitali, ndivyo ilivyo pia muhimu kutumia zana bora za kilimo kwa kilimo chenye tija. Matumizi sahihi na zana sahihi za kilimo ni moja ya njia inayochochea kuongeza tija katika mazao ya chakula.
Tanzania ina jumla ya hekta millioni 44 zinazofaa kwa kilimo huku asilimia 33 tu ya eneo hilo ikitumika kwa sasa. Kwa kuwezesha upatikanaji wa zana bora za kisasa, tutaweza kuchagiza ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula hivyo kuwezesha Taifa kuwa na utoshelevu wa chakula.
Akifafanua zaidi, Nyabundege anasema TADB imewezesha jumla ya Sh5.9 bilioni ambapo wakulima wameweza kupata trekta na mashine za kuvunia mazao ya nafaka kama vile mpunga. Katika sekta ya uvuvi pia wamewezesha ufugaji wa vizimba katika Ziwa Victoria na boti za uvuvi.
Pamoja na kuchangia jitihada za kuweza kuwezesha taifa kuwa na utoshelevu wa chakula nchini, TADB imeendelea kujikita katika kuwezesha ongezeko la uzalishaji, kuongeza thamani, uchakataji na uhifadhi wa mazao ya mifugo, uvuvi na kilimo.
“Mfano katika sekta ya uvuvi na mifugo, TADB imewezesha upatikanaji wa mfumo baridi (cold chains) ili kuhakikisha ubora na usalama wa mazao yatokanayo na uvuvi. Tumewezesha zaidi ya Sh2.2 bilioni kwenye sekta ya uvuvi na Sh9 bilioni kwenye sekta ya mifugo,” anasema Nyabundege.
Zaidi ya asilimia 80 ya chakula nchini huzalishwa na wakulima wadogo. Kwa kuzingatia hilo, TADB kupitia mfuko wake wa dhamana kwa wakulima wadogo (SCGS) imewezesha jumla ya Sh57.5 bilioni ambapo zaidi ya wakulima wadogo 3,962 wamenufaika.
TADB inatambua umuhimu na kuamini katika ushirikiano katika juhudi za kuwezesha Taifa kuwa na utoshelevu wa chakula. Hivyo kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuleta mapinduzi halisi na yenye tija katika sekta ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo.
“Kwa pamoja tutaweza kutengeneza mazingira bora kwa ajili ya uzalishaji wenye tija na mavuno bora kwa lishe na maisha ya watanzania,” anasema Nyabundege.