Job Ndugai aweka msimamo chanjo kwa wabunge

Job Ndugai aweka msimamo chanjo kwa wabunge

Muktasari:

  • Wakati kukiwa na mjadala wa baadhi ya wabunge kuhusu chanjo ya corona inayoendelea kutolewa nchini, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema pamoja na chanjo kuwa hiari, haimfanyi mtu kuwa na hiari ya kuambukiza wengine.

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na mjadala wa baadhi ya wabunge kuhusu chanjo ya corona inayoendelea kutolewa nchini, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema pamoja na chanjo kuwa hiari, haimfanyi mtu kuwa na hiari ya kuambukiza wengine.

Kauli hiyo imekuja kukiwa tayari kuna wabunge walioonyesha wazi kupingana na mpango huo wa chanjo wakieleza kuhofia usalama wake kwa afya ya anayechanjwa.

Hata hivyo, juzi katika mahojiano yake na BBC, Rais Samia Suluhu Hassan aliendelea kuwahakikishia Watanzania kuwa chanjo hiyo ni salama, kinyume na hapo yeye asingehatarisha maisha yake kwa kuwa wa kwanza kuchanjwa.

“Nashukuru sasa hivi Watanzania wengi wameelewa na wanaulizia chanjo, nalazimika kutuma maombi kwa nchi wahisani wanaosaidia chanjo waiangalie Tanzania wakati na sisi tukiendelea na mpango wa kununua chanjo kupitia nchi za Umoja wa Afrika (AU),” alisema Rais.

Pamoja na kauli hiyo ya Samia na uthibitisho wa wataalamu wa nchini na kimataifa, baadhi ya watu, wakiwemo wabunge kadhaa, wanaeleza waziwazi wasiwasi wao dhidi ya chanjo hiyo.

Akinukuliwa na kituo kimoja cha runinga, Spika Ndugai ambaye amekwishachanja, alisema, “tuna mabanda tayari yameshajengwa, wapo wataalamu na chanjo za kutosha zipo, kwa hiyo kila atakayekuja kwenye Bunge lijalo…(hakumalizia).

Aliongeza, “Ni hiari. “Ni hiari” alisema huku akionyesha ishara ya alama za funga usemi kwa vidole.

Kisha, Ndugai akasema, “...lakini hiari hii haikufanyi uwe na hiari ya kuchukua risk ya kuambukiza wengine.”

Mwananchi lilimtafuta Spika Ndugai jana ili aeleze alichokuwa anamaanisha, ambapo alifafanua zaidi kuwa vikao vya Bunge lijalo litakaloketi Agosti 30, ofisi yake itatoa mwelekeo huku akiwasisitiza wabunge wote kuchanja.

“Kuanzia Jumatatu (Agosti 16), wabunge wote watakuwepo (Dodoma) na uchanjaji utakuwa mkubwa. Tunaanza kwa kuhakikisha huduma zinakuwepo maana hata ukisema unachukua hatua, lazima huduma zipatikane, wenyewe ndiyo washindwe kwenda kuzipata. Natoa wito kwa wabunge wote kuchanja,” alisema Ndugai.

Miongoni mwa wabunge walioonyesha msimamo dhidi ya chanjo hiyo ni pamoja na aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, ambaye kwa sasa ni mbunge wa Kuteuliwa, Humprey Polepole.

“Ni muhimu sana watu wetu wakumbushwe tena na tena namna ya kujenga kinga ya mwili, ikiwemo elimu ya chakula na lishe bora kama hatua ya msingi ya kukabiliana na magonjwa na maambukizo yanayoweza kuzuiwa na kinga imara ya mwili. Kuchanja ni hiari lakini si kila kitu, mimi nitaimarisha kinga ya mwili na chanjo kwangu hapana,” aliandika Polepole kwenye ukurasa wake wa Instagram na kupongezwa na baadhi wafuasi wake, huku wengine wakimshukia.

Naye mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima mara kadhaa ametamka hadharani kuwa hatachanjwa chanjo hiyo kwa kuwa hana uhakika na usalama wake.

“Chanjo ni hiari anayependa aende, ila hapa hachanjwi mtu, lazima kondoo wangu niwalinde kwa namna yoyote ile, siko tayari kondoo wangu hata mmoja aangamie. Wajibu wa kulinda afya yako ni wako, huwezi kuwekewa kitu mwilini bila kutaka. Sichanjwi na sitachanjwa,” alisema Gwajima, ambaye ni askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima.

Mbunge huyo, kinyume na kauli za kitaalamu, alisisitiza kuwa hadi sasa hakuna tafiti za kutosha zilizofanywa na wataalamu wa ndani kuhusu chanjo hiyo inayotolewa nchini na kuwataka wataalamu kuweka wazi kemikali zilizomo kwenye chanjo hiyo.

Matamshi hayo yamemwibua Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka akisema msimamo wa chama hicho unaweka wazi kuwa chanjo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani yao kwenye kipengele cha utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania.

“Kwa hiyo sisi ukituuliza CCM msimamo wetu, tunasimama na Rais kwamba lazima tuwakinge Watanzania dhidi ya maradhi ya mlipuko, ikiwemo Uviko-19... tuna kanuni ya maadili, hii inawamulika viongozi wote ambao mienendo yao haiendi vizuri, ikionekana kuna mtu amekiuka kanuni, misingi ya chama ipo na haibagui, hatua zinaweza kuchukuliwa kwa yeyote,” alisema Shaka.