Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jokate ataja alama za uongozi alizoacha Kisarawe, Temeke

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Jokate Mwegelo akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na waandishi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ofisini kwake. Picha na Elizabeth Edward

Tukiendelea kuchapisha mahojiano maalumu tuliyofanya na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mkoa wa Tanga, Jokate Mwegelo ambaye ameeleza mambo mengi kuhusu maisha yake binafsi na utumishi wake katika nafasi hiyo tangu alipoteuliwa Julai, 2018.

Jokate alieleza licha ya kupenda siasa hakuwahi kufikiri kama angeteuliwa katika nafasi hiyo, aliamini kwamba ndoto yake ya kuingia kwenye siasa ilitakiwa ianze na kugombea ubunge iwe wa jimbo au kupitia jumuiya mbalimbali ndani ya CCM.

Katika sehemu hii ya tatu na ya mwisho, mazungumzo yamejikita kumuangalia Jokate katika nafasi ya ukuu wa wilaya na alama alizoacha kwenye wilaya alizowahi kuhudumu na mipango yake wilayani Korogwe.

Mwananchi: Umekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, nini kilikuwa kipaumbele chako baada ya kuteuliwa?

Jokate: Nilipofika niliona kuna kazi ya kufanya katika eneo la elimu na bahati nzuri mbunge wa Kisarawe, Dk Sulemani Jafo naye alikuwa na ajenda hiyo, hivyo akaniita akanieleza maono yake.

Kwa pamoja tukakubaliana kushirikiana kuweka nguvu katika eneo hilo na kuongeza usimamizi katika kuyatekeleza maono yake. Mbunge alitaka wananchi wake wakombolewe kupitia elimu na hicho ndicho kilifanyika Kisarawe.

Mwananchi: Ni alama gani unajivunia kuiacha Kisarawe?

Jokate: Tulijenga Shule ya Wasichana ya Jokate Mwegelo ambayo ni matokeo ya kampeni ya ‘Tokomeza Ziro’. Najivunia shule ile imekuwa miongoni mwa shule ambazo zinasaidia kuwawezesha watoto wa kike kupata elimu.

Kwangu ni faraja kila ninaposikia mazuri ya shule ile, kwa kuwa lengo letu lilikuwa kuwatengeneza mabinti kuweka elimu kama kipaumbele chao. Hii imekuwa tofauti na ilivyokuwa awali, kwani mwamko wa elimu katika Wilaya ya Kisarawe ulikuwa mdogo hasa kwa watoto wa kike.

Kingine ambacho najivunia Kisarawe ni tamasha la Ushoroba ambalo lililenga kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo kule. Kabla ya tamasha hili, watalii waliokuwa wanatembela ule msitu walikuwa 250 kwa mwaka, lakini hadi natoka walifika watu 18,000.

Naamini utalii ni njia mojawapo ya kufungua eneo, watu wanaweza kuja kutalii, lakini wakafungua maeneo mengine ya uchumi.

Mwananchi: Temeke inatajwa kuwa miongoni mwa wilaya ngumu kuziongoza kwako, ilikuwaje ulivyohamishiwa wilayani humo?

Jokate: Maneno, historia na mazoea yanakuwepo, lakini kinachohitajika ni kujiamini kwa kile ambacho umeaminiwa kukifanya. Nashukuru kila ninapokwenda naiweka akili yangu kuishi kulingana na mazingira na kusikiliza mawazo ya wenyeji.

Bahati nzuri sikuwa mgeni Temeke, nina historia na ile wilaya. Nilikuwa Miss Kurasini na hatimaye Miss Temeke, nimesoma pia St Antony pale Mbagala, kwa hiyo kupelekwa kule ni kama ilikuwa eneo langu la kujidai.

Nilivyofika nilikuwa na wazee wa pale baba zangu ambao walinipokea na kuniambia mambo kadha wa kadha ambayo yalinisaidia katika utumishi wangu.
Mwananchi: Alama gani uliacha Temeke?

Jokate: Yapo mengi tumefanya na viongozi wenzangu katika kuhakikisha wilaya yetu inakuwa na maendeleo na watu wanashiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo hayo.
Nakumbuka wiki ya kwanza baada ya kuanza kazi Temeke wazee wangu walinifuata na kuniambia changamoto ya usalama katika barabara nje ya uwanja wa Taifa kutokana na kukosekana kwa taa.

Waliniambia watu wengi wanakwenda uwanja wa Taifa, lakini wanapotoka usiku kuna hofu ya kukabwa kwa sababu ya giza katika barabara hiyo, niliona hoja yao na nikasimamia kikamilifu tukaweka taa hadi sasa ile barabara hakuna matukio ya uhalifu ikizingatiwa uwanja ule unabeba taswira ya Taifa kimataifa.

Mwananchi: Baada ya kuhudumu Kisarawe na Temeke, sasa upo Korogwe ni eneo gani utawekea nguvu katika wilaya hii (Korogwe)?

Jokate: Kitu ambacho nimekigundua ambacho nakiona changamoto ni kutokana na historia ya maeneo niliyopita, watu wa Korogwe wana matarajio makubwa kwangu. Hii ni changamoto chanya kwangu kama kiongozi maana hata mapokeo ya watu na utayari wao katika kufanya kazi unakuwa mkubwa, ili kwa pamoja tupate matokeo kama yale yaliyotokea kwenye wilaya nilizopita.

Hili linanifanya nifikirie tufanye nini, ili kufikia hayo matarajio ya wananchi, kwa kiasi fulani inanipa pressure maana inawezekana matarajio ni makubwa kuliko yale unayoweza kuyafanya. Kikubwa naendelea kupokea maelekezo kutoka viongozi wa juu tukiongeza na ubunifu wetu kusonga mbele.

Mwananchi: Changamoto ipi unaiona inasumbua watu wa Korogwe?

Jokate: Elimu ni ajenda ya kitaifa ambayo hata hapa Korogwe kwa kushirikiana na wenzangu tutaifanyia kazi. Kubwa ninaliona hapa ni umbali wa zilipo shule, hali inayowalazimu watoto kutembea umbali mrefu.

Hii inaweza kuwa kikwazo kwa wanafunzi hasa watoto wa kike kukatisha masomo na kuingia vishawishi kwa sababu ya kutembea umbali mrefu. Kwa kuanzia tunashirikiana na wadau kutekeleza programu ya kugawa baiskeli. Pia Serikali inatekeleza mpango wa kujenga mabweni na tutaangalia programu nyingine.

Mwananchi: Wakulima wa mkonge Korogwe wanalalamikia mashine ya kuchakata zao hilo na tozo nyingi wanazotozwa. Serikali inafanya nini katika hili?

Jokate: Ni kweli kuna hiyo changamoto na ni ajenda ambayo nimeibeba kwa uzito mkubwa, nilishakua na kikao na wakulima wa mkonge tumezungumza mengi, wakaeleza changamoto zao ikiwemo hizo za tozo. Nimezichukua na kuahidi kuzifanyia kazi maana nyingine ni za kisera ambazo zinahitaji maamuzi ya ngazi ya juu.

Tumeunda kamati ndogo ya kupitia changamoto za kisera, tunaamini kilimo cha mkonge kikifanyika kwa ubora wake uchumi wa Korogwe utaimarika. Kuhusu mashine tulikuwa na mazungumzo na benki walisema wataleta mashine mpya, tunaamini itasaidia kupunguza tatizo hilo.

Pia hivi karibuni amejitokeza mwekezaji mwingine ambaye ataweka kiwanda cha kuchakata mkonge. Pamoja na hayo yote, tunaendelea kutangaza zao hili, ili kuongeza mnyororo wake wa thamani isiishie kwenye nyuzi, ni muhimu tuboreshe soko kwa Serikali kusimamia katazo la matumizi ya kamba za plastiki.

Mwananchi: Nini tofauti ya kuongoza wilaya za mjini na zile za pembezoni?

Jokate: Hakuna tofauti kubwa zaidi ya shughuli za kiuchumi kwa sababu mjini kuna mambo mengi na mwingiliano mkubwa wa watu tofauti na vijijini, lakini kwenye uongozi hakuna tofauti.

Nikiangalia hapa Korogwe mwingiliano wa watu ni mkubwa, halafu ni wilaya yenye barabara kubwa kwa hiyo watu wengi wanapita. Suala la ulinzi na usalama linapaswa kuangaliwa kwa kiasi kikubwa.