Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

JWTZ kuongeza nguvu kuzima moto mlima Kilimanjaro

Muktasari:

Wakati moto ukiendelea kuwaka siku ya pili katika mlima Kilimanjaro, Serikali imeliomba Jeshi la Wananchi (JWTZ) kuongeza nguvu ili kuweza kuudhibiti moto huo ambao unaeleza kusambaa kwa kasi kutokana na upepo mkali.

Moshi. Wakati moto ukiendelea kuwaka siku ya pili katika mlima Kilimanjaro, Serikali imeliomba Jeshi la Wananchi(JWTZ)kuongeza nguvu ili kuweza kuudhibiti moto huo ambao unaendelea kusambaa kwa kasi kutokana na upepo mkali.

 Tayari kundi la watu zaidi ya 500 wakiwemo askari polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, askari wa Tanapa, wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori (Mweka), mgambo na wadau wengine wa kampuni za utalii wamefika katika eneo la tukio kukabiliana na moto huo

Moto huo  ulianza kuwaka Oktoba 21 saa moja usiku, katika eneo la  Karanga kuelekea Baranco, lililopo mita 3,963 kutoka usawa wa bahari.

Akizungumza na waandishi wa habari jana usiku katika lango la Mweka, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Eliamani Sedoyeka amesema jana jioni walizunguka katika eneo linalowaka moto kwa kutumia ndege ya Tanapa na kuangalia ukubwa wa moto na eneo lililoathirika.

Profesa Sedoyeka amesema baada ya kuona bado moto huo unaendelea kuwaka ndipo walipoamua kuwasiliana na uongozi wa JWTZ na kuomba kuongeza nguvu ili kuweza kuudhibiti moto huo.

“Mpaka sasa watu 500 wako eneo la tukio wakiendelea na jitihada za kuzima moto lakini tayari tumewasiliana na Jeshi la Wananchi kwa ajili ya kuongeza nguvu kazi ili kuweza kuudhibiti moto huu na tunategemea kesho Oktoba 23 watakuwa wamefika ili kuweza kuongeza nguvu  kufanikisha jitihada za kuuzima”

“Tunachokifanya sasa ni kuzuia moto usishuke kwenye msitu mkubwa na tuna matumaini tukiongeza nguvu tutaweza kuudhibiti moto huu ndani ya siku mbili kwani tayari tumefanikiwa kuudhibiti katika maeneo mawili,"

Profesa Sedoyeka ametoa wito kwa wananchi kuacha kufanya shughuli au vitendo ambavyo vinaweza kuhatarisha usalama wa mlima ikiwemo kuwasha moto ambao husababisha majanga makubwa.

“Katika mlima wetu bahati mbaya hili limekuwa likijirudia na tumejitahidi sana kuendelea kusisitiza na kukumbushana moto ni hatari na kila mtu anayefanya shughuli za kuanzisha moto atambue hili madhara yake ni makubwa,"

Ameongeza "Inawezekana kuna mtu alifanya uzembe akiwa kwenye shughuli ya kupanda au kushuka mlima au wenzetu wanaorina asali au kuwinda na kusababisha moto huu, maana hakuna shughuli za kilimo huko”.

Amesema mpaka sasa hakuna madhara yoyote ya kibinadamu yaliyosababishwa na moto huo na kwamba shughuli za utalii za kupanda na kushuka mlima Kilimanjaro zinaendelea kama kawaida kwa kuwa hakuna njia ambayo imeathiriwa na moto huo.

“Moto huo mpaka sasa haujasababisha madhara yoyote kwa binadamu wala kuathiri njia za kupanda na kushuka katika mlima Kilimanjaro zote ziko salama, maana eneo ambalo moto upo, hauingilii safari za kupanda wala kushuka Mlima Kilimanjaro, hivyo watu wasihofu kupanda mlima na sisi tunaendelea kuudhibiti kuhakikisha hauendelei hapo ulipo”.

Amesema Wizara pia inaendelea kujikita zaidi katika kuhifadhi na kulinda na kuhakikisha kunapotokea majanga ya moto wanayadhibiti kwa haraka ili kuzuia kuleta madhara makubwa.