Kampuni ya kimataifa kuwekeza vituo vya CNG Tanzania

Thursday August 04 2022
kampuni pic
By Kelvin Matandiko

Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakiendelea kulalamikia uhaba wa vituo vya kujazia gesi katika magari yao, Kampuni ya GRAF Industries imeahidi kuwekeza hapa nchini ili kutoshereza mahitaji.

 Kampuni hiyo kutoka Italia ilianza uzalishaji wa bidhaa zinazotumika katika usimikaji wa vituo vya gesi iliyosindikwa(CNG) na gesi iliyopo kwenye kimiminika (LNG) mwaka 1994 huku ikiwa katika mataifa ya Misri, nchi za Umoja wa Ulaya, Urusi na Amerika ya Kati.

“Tunatafuta ubia na kampuni za ndani na tuko tayari kwa ajili ya kuwezesha ongezeko la vituo vya kujaza gesi katika magari(CNG), tumeshawishika na mwenendo wa mahitaji kwa sasa hapa Tanzania,” amesema Federico Soragni, Meneja wa mauzo wa Kimataifa wa kampuni hiyo.

Federico ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Agosti 4, 2022 wakati wa Kongamano la Kimataifa la Nishati linaloendelea Jijini Dar es Salaam kwa mara ya nne tangu lilipoanzishwa mwaka 2017.

Pamoja na uwepo wa gesi nchini, tangu 2009 bado kumekuwapo na vituo viwili tu vya CNG: Kituo cha Ubungo chini ya Kampuni ya Uzalishaji Gesi ya PanAfrican Energy Tanzania (PAET) na kile cha Tazara chini ya Kampuni ya Enric Gas Technology Tanzania Limited, vinavyotoza Sh1,550 kwa kilogramu vyote vikiwa jijini Dar es Salaam.

“Tuko hapa kuhakikisha tunawezesha zaidi mahitaji ya vituo vya CNG na tumeona kuna mwitikio mkubwa wa sekta binafsi, bado hatujapata kampuni ya kitanzania lakini tunaamini tutafanikiwa,” amesema Federico.

Advertisement
Advertisement