Kardinali Pengo aongoza ibada kutakatifuza Kanisa Katoliki Geita

Maandamano ya Ibada maalum ya kutakatifuza Kanisa kuu la Kiaskofu Jimbo Katoliki Geita.

Muktasari:

  • Ibada maalum ya kutakatifuza Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo Katoliki Geita imeanza ambapo mamia ya waumini kutoka ndani ya na nje ya jimbo wameshiriki ibada hiyo inayoongozwa na Askofu mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polcycarp Pengo.

Geita. Mamia ya waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Geita wameshiriki Ibada maalum ya kutakatifuza Kanisa Kuu la Kiaskofu inayofanyika katika kanisa hilo lililopo mjini Geita.

Ibada hiyo imetanguliwa na maandamano ya amani yaliyoanza katika Parokia ya Fatima yakiongozwa na mapadri, mafratee, makatekista, watawa na waumini kutoka Jimbo Katoliki Geita na majimbo mengine ya jirani.

Ibada hiyo imeanza kwa Askofu mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo kubariki maji ya baraka kwa ajili ya kutakasa Kanisa na maaskofu kunyunyuzia maji  hayo kwa mamia ya waumini walioshiriki ibada kisha kuta za kanisa.

Shughuli nyingine zitakazofanyika katika ibada hiyo ni pamoja na harambee ikifuatiwa na hotuba za viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Baraza la Maaskofu (TEC), Gervas Nyaisonga ,Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella pamoja na Askofu wa Kanisa Kuu Katoliki Jimbo la Geita, Dk Flavian Kasala.

Ibada ya kutakatifuza Kanisa imetokana na Kanisa hilo kufanyiwa kufuru na najisi kufuatia tukio la kijana mmoja kuvunja kioo cha lango kuu la kanisa Februari 26 na kufanya uharibifu eneo la sakramenti ya ekaristi takatifu na uharibifu wa vifaa mbalimbali vya madhabahuni vyenye thamani ya zaidi ya Sh40 milioni.

Kanisa hilo lilifungwa kwa siku 20  ambapo waumini na viongozi waliingia kwenye adhimisho la toba ya malipizi, kusali, kutubu, kupokea sakramenti ya upatanisho na kuomba huruma ya Mungu katika matendo yaliyotendeka Kanisani hapo.