Katibu mkuu mpya EAC kuanza kazi Ijumaa

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Adan Mohamed atasimamia makabidhiano ya ofisi kati ya katibu mkuu mpya wa jumuiya hiyo, Dk Peter Mathuki  na mtangulizi wake, Balozi Liberat Mfumukeko.

Arusha. Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Adan Mohamed atasimamia makabidhiano ya ofisi kati ya katibu mkuu mpya wa jumuiya hiyo, Dk Peter Mathuki  na mtangulizi wake, Balozi Liberat Mfumukeko.

Taarifa ya idara ya mawasiliano kwa umma iliyotolewa na ofisa habari mwandamizi wa sekretariati ya EAC, Simon Owaka inaeleza kuwa makabidhiano hayo yatafanyika makao makuu ya EAC jijini Arusha Ijumaa Aprili 23, 2021.

Mkutano wa 21 wa wakuu wa EAC uliofanyika Februari, 2021  kwa njia ya mtandao ulimtangaza, Dk Mathuki kutoka Kenya kuwa katibu mkuu mpya baada ya Balozi Mfumukeko kutoka Burundi  kumaliza muhula wake wa miaka mitano.

Dk Mathuki amewahi kuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) kwa kipindi kimoja cha miaka mitano na baadaye kuwa ofisa mtendaji mkuu wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) lenye makao yake jijini Arusha hadi alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Nafasi ya katibu mkuu wa  EAC ni ya mzunguko miongoni mwa nchi sita wanachama wa jumuiya hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.

Waliowahi kushika wadhifa huo ni Francis Muthaura (Kenya) mwaka 1996 hadi 2001, Amanya Mushega (Uganda) mwaka 2001 hadi 2006, Balozi Juma Mwapachu wa Tanzania (2006- 2011), Dk Richard Sezibera wa Rwanda (2011 hadi 2016) na Balozi  Mfumukeko kuanzia Aprili 2016 hadi 2021.

Katika mtandao wake wa Twitter, Balozi Mfumukeko ameishukuru Benki ya Dunia (WB) kumteua kuwa mwakilishi wa mfuko wa nchi wakopaji na mwenyekiti mwenza kundi la nchi 22 za Afrika zikiwemo za EAC .