Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kesi ya anayedaiwa kughushi nyaraka za mafao kuunguruma Januari 29

Muktasari:

  • Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, Desemba 8, 2023, katika ofisi za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Ilala Boma jijini hapa.

Dar es Salaam. Serikali imesema inatarajia kuwa na mashahidi wanane na vielelezo vinne katika kesi ya kughushi nyaraka inayomkabili mshtakiwa, Idd Mmanga.

Mmanga ambaye alikuwa mfanyakazi wa Kampuni ya A one Products and Bottlers Limited, anadaiwa kughushi nyaraka hizo ili ajipatie mafao kutoka Mfumo wa Hifadhi wa Jamii (NSSF), wakati akijua ni kosa kisheria.

Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.

Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama hiyo, leo Jumatatu Januari 20, 2025 wakati akimsomea hoja za awali (PH) mshtakiwa huyo.

Kasala amemsomea maelezo hayo, mbele ye Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu.

Akimsomea hoja zake, Wakili Kasala alidai mshtakiwa alikuwa mfanyakazi wa Kampuni ya A one Products and Bottlers Limited.

Alidai Desemba 8, 2023, akiwa katika ofisi za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Ilala Boma wilaya ya Ilala, saa 7 mchana, mshtakiwa alikamatwa na maofisa wa Polisi baada ya mfanyakazi wa mfuko huo kudai kuwa kuna mwanachama wao amewasilisha nyaraka za kughushi.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo aliwasilisha fomu ya kudai mafao na cheti cha huduma kutoka kampuni ya A one Products and Bottlers Limited akidai ameachishwa kazi hivyo anahitaji mafao yake.

Mahakama iliendelea kuelezwa kuwa Mmanga ambaye alikuwa Mdhibiti Ubora wa kampuni hiyo, baada ya kukamatwa, alipelekwa Kituo cha Kikuu cha Polisi Dar es Salaam (Central) kwa ajili ya mahojiano.

"Katika mahojiano hayo, mshtakiwa alikiri kosa lake na kwamba nyaraka alizodaiwa kughushi zilipelekwa ofisi ya Maabara ya Maandishi kwa uchunguzi zaidi," amedai Wakili Kasala na kuongeza kuwa,  uchunguzi ulibaini kwamba nyaraka hizo zilighushiwa na ndipo mshtakiwa alifikishwa mahakamani kukabiliana na kesi yake.

Mshtakiwa baada ya kusomewa hoja hizo, alikana maelezo hayo isipokuwa jina na anwani yake, kukamatwa na polisi, kuhojiwa, kufikishwa mahakamani na kufanya kazi katika kampuni ya A one Products and Bottlers Limited.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, hakimu Magutu aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 29, 2025 itakapoanza kusikilizwa na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.