Kesi ya Sabaya yamuibua Askofu KKKT

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, DkSolomon Masangwa akiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakati kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita ilipokuwa ikiendelea. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

Kwa mara ya kwanza katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya ameshuhudiwa kiongozi wa kiroho ambaye ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Solomon Masangwa.

Arusha. Kwa mara ya kwanza katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya ameshuhudiwa kiongozi wa kiroho ambaye ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Solomon Masangwa.

Leo Novemba 2, 2021 shughuli za mahakama zimehamia katika Kituo jumuishi cha utoaji haki Arusha, ambapo Askofu huyo alishiriki katika uzinduzi akiwa na viongozi wengine kisha kuingia katika shauri hilo la Sabaya na wenzake na kufuatilia mwenendo kuanzia mwanzo hadi lilipoahirishwa.

Dk Masangwa aliingia mahakamani wakati kesi hiyo ilipokuwa inaendelea kusikilizwa ambapo aliungana na wasikilizaji wengine katika kesi hiyo.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Patricia Kisinda, shahidi wa nane wa Jamhuri, ofisa uchunguzi wa maabara ya uchunguzi wa kielektroniki kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Johnson Kisaka alimaliza kutoa ushahidi wake.

Shahidi huyo amemaliza kutoa ushahidi wake baada ya kuhojiwa na jopo la mawakili sita wa utetezi wakiongozwa na Wakili Mosses Mahuna.

Baada ya shahidi kumaliza kuhojiwa na mawakili wa utetezi, upande wa Jamhuri uliieleza mahakama kuwa kesho wataendelea na shahidi mwingine.

Jana mahakama hiyo kupitia shahidi huyo ilionyeshwa video clip sita zinazoonyesha matukio yaliyotokea benki ya CRDB Arusha,tawi la Kwa Moromboo Januari 22, mwaka huu.