Kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili watumishi 16 wa Jiji la Dar yaiva

Muktasari:

  • Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 142 yakiwamo ya kuongoza genge la uharifu, matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh 8.9bilioni.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Juni 7, 2024 kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo, watumishi 16 wa Jiji la Dar es Salaam, wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 142, yakiwamo ya kuongoza genge la uhalifu, matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia hasara jiji hilo ya Sh8.9bilioni.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 32/2023 kukamilika na upande wa mashtaka kukamilisha taratibu za kusajili taarifa na nyaraka muhimu Mahakama Kuu.

Kesi hiyo ilipagwa leo, Mei 30, 2024 kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo, lakini Wakili wa Serikali,  Glory Kilawa aliieleza Mahakama hiyo kuwa wakili  anayeendesha kesi hiyo yupo Mahakama Kuu kwenye kesi nyingine, hivyo kutokana na sababu hiyo wanaomba Mahakama ipange tarehe ya karibu ili waweze kuwasomea maelezo yao washtakiwa hao.

Hakimu Mkazi Mkuu, Mwankuga anayesikiliza shauri hilo, alikubaliana na ombi la upande wake mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 7, 2024 na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba Mahakaka Kuu.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Tulusubya Kamalamo(53) Mkazi wa Ukonga na mwenzake  James Bangu(57) Mkazi wa Kibada, ambao wote ni weka hazina.

Wengine ni wahasibu wa jiji hilo ambao ni Mohamed  Khais(41), Abdallah Mlwale(52), Deogratias Lutataza(55) na karani wa fedha Judica Ngowo(51) maarufu Kama Lightness.

Wahasibu wengine ni Febronia Nangwa(44), Said Bakari, Glory Eugen(45), Josephine Sandewa(48), Dorica Gwichala(45) na Jesca Lugonzibwa(53).

Pia yumo, ofisa afya wa halmashauri hiyo, Patrick Chibwana(40), Ally Baruani(38) ambaye ni meneja mkuu, Khalid Nyakamande (34) ofisa mtendaji wa mtaa na mhasibu Alinanuswe Mwasasumbe(60) mkazi Mbagala Majimatitu.

Kati ya mashtaka hayo 142, lipo la kuongoza genge la uhalifu, matumizi mabaya ya madaraka, kuingiza taarifa za udanganyifu katika mfumo, ufujaji wa fedha na ubadhilifu, kughushi na kuisababishia hasara mamlaka.

Miongoni mwa mashtaka hayo, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Julai Mosi 2019 na Juni 6, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, waliongoza genge la uhalifu na kujipatia Sh8.9bilioni, mali ya Halmashauri ya Jiji.

Katika shtaka la matumizi mabaya ya madaraka, washtakiwa wote wanadaiwa  katika tarehe hizo, walishindwa kuingiza mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam yanayotokana na vyanzo mbalimbali vya mapato kwenye akaunti ya jiji hilo iliyopo katika benki za NMB, CRDB, NBC na DCB,  hivyo kujipatia manufaa yasiyo halali na kuisababishia hasara ya Sh8.9bilioni.

Katika shtaka la kuingiza taarifa za udanganyifu katika mfumo, washtakiwa hao wanadaiwa waliingiza taarifa za uongo kuonyesha mapato yaliyokusanywa  katika Jiji la Dar es Salaam, waliingiza mapato hayo katika akaunti ya benki za NBC, CRDB, NBC DCB, inayomilikiwa na jiji hilo.

Pia, wanadaiwa kughushi nyaraka kuonyesha kuwa ni halali wakati wakijua kuwa sio kweli.