Kesi ya vyama vya siasa kusikilizwa Novemba

Kesi ya vyama vya siasa kusikilizwa Novemba

Muktasari:

  • Majaji watano wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), wamekubali maombi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, kuunganisha kesi namba 3 ya mwaka 2019 iliyofunguliwa na vyama vitano vya siasa na kesi namba 4 ya mwaka 2019 iliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Arusha. Majaji watano wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), wamekubali maombi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, kuunganisha kesi namba 3 ya mwaka 2019 iliyofunguliwa na vyama vitano vya siasa na kesi namba 4 ya mwaka 2019 iliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Jaji Kiongozi wa EACJ, Yohane Masara akiongoza majaji wenzake aliwahoji mawakili wa pande zote mbili; wa LHRC, Fulgence Massawe na wa Serikali, Vivian Method ambao watawasilisha hoja za kisheria kwa maandishi, kabla ya kusikiliza kesi ya msingi baadaye mwezi Novemba.

Katika kesi hizo mbili ambazo zilifunguliwa kwa nyakati tofauti, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, iliomba Mahakama hiyo kuziunganisha kuwa kesi moja, kwa kuwa hoja za walalamikaji zinalenga jambo moja la kupinga Sheria ya Vyama vya Siasa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Hata hivyo, wakili Massawe alisema licha ya kuwa Mahakama ina uamuzi wa kuziunganisha kuwa kesi moja, wao kama LHRC kuna baadhi ya vipengele wanavyovipigania wakiwa na mtazamo wa kitaasisi tofauti na vipengele vinavyopingwa na vyama vya siasa.

Kituo cha Sheria kinadai mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019, yanakiuka Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambao Tanzania iliridhia.

LHRC kinadai sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge la Muungano Januari 29,2019, kusainiwa na Rais na kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali Februari 22,2019 ina upungufu mwingi ambao kinaiomba EACJ iyabatilishe.

Katika kesi hiyo ambayo imefanyika kwa njia ya mtandao LHRC, kinadai mkataba ulioanzisha EAC ibara ya 4,6(d),7(2),8(1)(c), 27(1),30(1) na 38(2) pamoja na kanuni za mahakama hiyo ibara ya 1(2) na 24 ya mwaka 2013, zimekiukwa pia inadai mabadiliko ya sheria yanazuia demokrasia, utawala bora na haki ya kukusanyika.

Kwa upande wa vyama vya siasa, vikiwamo ACT, Chadema na vingine vitatu, vinadai mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa yanakiuka mkataba wa EAC ibara ya 6(d),7(2),8(1)(c),27(1),30 na kanuni za mahakama hiyo.

Wakili Jebra Kambole anayewakilisha vyama hivyo, alisema walishawalisha hoja mahakamani na hawana pingamizi za kuunganishwa kuwa kesi moja.