Kigamboni waanza operesheni kudhibiti panya road

Muktasari:
- Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa amekutana na wenyeviti wa Serikali za mitaa wa wilaya hiyo, huku akiwaonya vijana waliopanga kufanya uhalifu akisema polisi imeanza operesheni ya kukabiliana na vitendo hivyo.
Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa amekutana na wenyeviti wa Serikali za mitaa wa wilaya hiyo, huku akiwaonya vijana waliopanga kufanya uhalifu akisema polisi imeanza operesheni ya kukabiliana na vitendo hivyo.
Mkutano wa Nyangasa na wenyeviti hao pamoja na wajumbe kamati ya ulinzi na usalama umefanyika leo Alhamisi Septemba 15, 2022 katika ofisi ya mkuu wa huyo. Nyangasa amewaelekeza wenyeviti hao kuhakikisha ulinzi shirikishi unafanyika kikamilifu na kutoa taarifa ya hali ya usalama katika maeneo yao.
"Kuanzia leo tumeanza operesheni maalumu katika maeneo na mitaa yote ya Kigamboni. Nyie (wenyeviti) ni viongozi kwenye mitaa kwa hiyo mtashiriki hili kikamilifu.
" Lengo kuhakikisha hakuna mtu mwenye nia au mipango ya kufanya uhalifu kwa Wanakigamboni. Jukumu letu kuwalinda wananchi wa Kigamboni, sote tuwajibike, polisi wataingia mitaani na viongozi tushirikiane kwa kutoa taarifa sahihi," amesema Nyangasa
Mkuu wa Polisi wilaya ya Kigamboni, ( OCD) Thobias Walelo amesema timu yake ipo tayari kuhakikisha ulinzi na usalama unaendelea kuimarika Kigamboni, huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano katika upatikanaji taarifa za watu au kikundu kinachojihusisha vitendo vya uhalifu.