Kikwete ampigia chapuo Profesa Mkenda uchaguzi ujao
Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete akiweka shada la maua katika kaburi la aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha, Basili Mramba wakati alipohani kwenye familia yake.
Muktasari:
- Rais wa awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amewataka wakazi wa Wilayani Rombo kuendelea kumuamini mbunge wao, Profesa Adolf Mkenda.
Rombo. Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewataka wakazi wa Wilayani Rombo, kumshikilia Mbunge wao, Profesa Adolf Mkenda kwa kuwa ni miongoni mwa wabunge wanaofanya vizuri nchini.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo Julai, 15 nyumbani kwa aliyekuwa Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya Shirika la Ndege la Precision Air, Michael Shirima katika Kijiji cha Nayeme alipokwenda kuhani.
"Namshukuru sana Waziri wetu na mbunge wa Rombo kwa maandalizi na mapokezi mazuri kuja kuwoambea hawa marafiki zangu ambapo wakati wanazikwa sikuwepo, Mbunge huyu ni moja ya wabunge wazuri hapa nchini 'he's a good guy 'ni mtu mzuri'," amesema.
Rais huyo wa awamu ya nne nchini, amesema ni bahati kwa wakazi wa eneo hilo kuwa na Mbunge hiyo.
"Mnabahati sana kuwa na mbunge kama huyu, kuna sehemu nyingine wanatafuta wabunge wazuri kama huyu wanapata tabu, kwa hiyo mimi nakuombea kila la heri uchaguzi unakaribia hakika Warombo watakuchagua tena," amesema.
Aliongeza, "Nakushukuru kwa sababu wewe ndiye uliyeniunganisha na hizi familia, nakushukuru sana kwa maandalizi na mapokezi mazuri kuja kutoa heshima kwa hawa marafiki zangu.
"Nilianza nao mbali katika maisha yetu ya siasa na maisha yetu ya kawaida, naombeni muendelee kuwa na moyo wa subira na ustahimilivu, wazee wenu hawapo ninyi sasa mpo ndio wazee, hata huku walipo wanajua kazi walizoziacha zinaenda vizuri na wao wanafurahi," amesema.
Naye Mbunge wa Rombo, ambayo pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amemshukuru Rais Mstaafu Kikwete kwa kuthamini mchango wa waasisi katika Taifa hili.
" Tunakushukuru Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kwa kuja kwenye familia hizi ambazo zilipoteza wapendwa wao, umeenda kwa Mramba, kwa Isdori Shirima, na hapa kwa Michael Ngaleku familia zimefarijika sana Wanaronbo na watanzania wamefarijika sana kwa kuona hawa waliotutangulia na kufanya mchango mkubwa katika taifa hili wanakumbukwa ,"amesema Mkenda
Kikwete alihani makaburi ya aliyewahi kuwa Waziri wa fedha nchini Tanzania, Basil Pesambili Mramba, Michael Ngaleku Shirima, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya shirika la ndege la Precision Air, aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mara, Arusha na maeneo mengine, Isdori Shirima na mfanyabiashara maarufu nchini, Steven Kangero, mkazi wa Wilaya wa Mwanga