Kikwete aonya Serikali kupuuza ushauri
Muktasari:
- Mkutano wa nne wa Maendeleo ya Biashara na Uchumi ulioandaliwa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), umefanyika na kushirikisha watu mbalimbali akiwemo Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete ambaye ametumia mkutano huo kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo viongozi kutopuuzia ushauri unaotolewa.
Dodoma. Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema Serikali ikikosa ushauri mzuri ama ikipuuza nchi itakwenda pasipostahili.
Kikwete ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Novemba 22, 2023 alipokuwa akielezea umuhimu wa makongamano na mikutano katika kuishauri Serikali na Rais, kwenye mkutano wa nne wa Maendeleo ya Biashara na Uchumi ulioandaliwa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ambapo alikuwa mgeni rasmi.
“Ukikosa ushauri mzuri ama ukipata ushauri mzuri ukaupuuza hii nchi itakwenda kusikotakiwa kwenda. Ndio maana makongamano haya ni muhimu sana unachota mawazo,” amesema Kikwete aliyekuwa Rais wa nne wa Tanzania (2005-2015).
Amesema unapokuwa Rais hujui kila kitu lakini unatakiwa kushughulika na kila jambo na kwa sababu huwezi kujua kila kitu inakubidi kutegemea ushauri.
“Wenzako wanakuchagua kwamba unafaa kuwa Rais, lakini utakuwa hujui kila kitu, taaluma yako ni uchumi…lakini ukiwa Serikali na Rais hujui kila kitu. Kwa sababu huwezi kujua kila jambo, lazima utegemee sana ushauri,” amesema.
Amesema ndio maana Rais ana mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, makamishna, wakurugenzi na ofisi binafsi ambayo inawashauri.
Amewataka wasomi hao kutoa ushauri kwa Serikali juu ya mambo mazuri ya kufanya na kile ambacho si kizuri kiachwe na kirekebishwe.
Kikwete amesema uchumi hauwezi kukua bila uwekezaji, na unakuwa mahali ambapo mazingira ya biashara ni rafiki ikiwa vinginevyo wawekezaji wataondoka.
Ametoa mfano wa mfanyabiashara maarufu, marehemu Zacharia Hans Poppe ambaye wakati wa uhai wake alikutana naye nchini Afrika Kusini.
Amesema mfanyabiashara huyo alimweleza amehamishia biashara zake na magari yake yote nchini humo kutokana na mazingira ya biashara kutokaa vizuri nchini.
Amepongeza chuo hicho kwa kuandaa kongamano hilo, lakini akashauri kuangalia uwezekano wakuandaa lingine ambalo litashirikisha taasisi nyingine za elimu za juu.
Kikwete amesema kufanya utafiti ni njia ya kuboresha upeo na maarifa ya kila mtu na itasaidia katika maendeleo ya Taifa.
Bei za mafuta kupanda
Kikwete amesema iwapo bei ya mafuta imepanda katika nchi zinazozalisha ni wazi haiwezi kupungua nchini.
“Namshukuru Rais (Samia Suluhu Hassan) kwa utashi wa kisiasa ameweka ruzuku ya Sh100 bilioni lakini hii inapunguza kwa senti chache. Wakishaweka ruzuku ya Sh100 bilioni bei ya mafuta inapanda tena.
“Kwa hiyo ndio mazingira tuliyonayo hadi wakimaliza vita (Ukraine na Israel) na kuruhusu mafuta yao kuingia katika soko tutakuwa na nafuu,”amesema.
Kikwete amesema hali hiyo ipo pia kwa mbolea, mafuta ya kula na ngano ambazo wazalishaji wakubwa ndio nchi hizo zinazopigana vita.
Amesema nchi moja tu ni vigumu kutatua, hivyo kunatakiwa kuwe na ushirikiano wa nchi zaidi ya moja.
Amesema hakuna nchi iliyopiga hatua za maendeleo kwa kujifungia yenyewe bila kushirikiana na nchi nyingine.
Aidha, amesema maendeleo ya nchi yoyote ya uchumi huchochewa na matumizi sahihi ya tafiti na ushauri wa kitaalamu, kinyume cha hapo maendeleo ni madogo.
Akizungumza awali, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amesema sasa ni wakati wa kuwa na kozi fupi za wajasiriamali walioko nchini.
“Tumejiwekea malengo ya kuainisha wajasiriamali wale wanaoanza ndani ya mwaka mmoja tuweze kuwakuza baada ya miaka mitatu waweze kuwa wajasiriamali wa kati na hatimaye tutengeneze wafanyabiashara wakubwa na mabilionea,” amesema.
Amesema wao ndio wanaowafundisha wafanyabiashara wanapaswa kuwaonyesha namna ya kutoka walipo, mahali pa kupata mitaji ili waanzishe biashara.
Dk Kijaji amesema yapo machapisho duniani yanayoonyesha kuwa biashara baada ya miaka mitatu hufa, hivyo kuna kazi ambayo wao kama chuo hawajaifanya kikamilifu.
Naye Mkuu wa Chuo cha CBE, Profesa Edda Luoga amesema tafiti zitakazokuwa bora zaidi katika kongamano hilo wanatarajia zitachapishwa kwenye majarida, kmtandao wa chuo hicho.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo hicho, Profesa Wineaster Anderson amesema wana mpango wa kupanua huduma zake ili kuwafikia walengwa wengi nchini na mipango hiyo inatazama zaidi visiwa vya Zanzibar, mikoa ya Lindi na Iringa.