Kikwete ateta na Wajackoyah akiwa kijijini

Kikwete ateta na Wajackoyah akiwa kijijini

Muktasari:

Kiongozi wa Wasimamizi wa Uchaguzi Mkuu Kenya wa Kenya uliofanyika Agosti, 9, 2022 kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Jakaya Kikwete ameeleza kuwa alishindwa kukutana na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na mgombea urais wa tiketi ya chama cha Roots, George Wajackoyah kama alivyofanya kwa wagombea wengine.

Nairobi. Kiongozi wa Wasimamizi wa Uchaguzi Mkuu Kenya wa Kenya uliofanyika Agosti, 9, 2022 kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Jakaya Kikwete ameeleza kuwa alishindwa kukutana na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na mgombea urais wa tiketi ya chama cha Roots, George Wajackoyah kama alivyofanya kwa wagombea wengine.

Amesema alilazimika kuwasiliana naye kwa simu kwa kuwa mgombea huyo alikuwa kijijini kwake akijiandaa kupiga kura lakini akamuahidi akirejea jijini Nairobi watazungumza.

Kikwete ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Agosti 11, 2022 alipokuwa akitoa ripoti ya uangalizi kuhusu mchakato wa uchaguzi huo aliosema umefanyika kwa amani na utulivu mkubwa.

Amesema katika utekelezaji wa majukumu yao nchini humo, wamekutana na wasimamizi wa uchaguzi, na wagombea wa nafasi ya urais, vyombo vya habari, vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi hiyo pamoja na wadau mbalimbali.

“Kabla kufanya kazi hii tulikutana na Tume ya uchaguzi ikiongozwa na Mwenyekiti Wafula Chebukati, wagombea wote wa uchaguzi Raila Odinga, William Ruto, David Waihiga lakini profesa George Wajackoyah nilizungumza nae kwa njia ya simu kwasababu alikuwa kijijini kwake na tukakubaliana tutakutana akirudi,” amesema.

Kuhusu matumizi ya vifaa vya kielektroniki, Kikwete amesema kuwa vifaa hivyo vimeongeza ufanisi japokuwa kulikuwa na baadhi ya kasoro zilizoibuka siku ya kupiga kura hivyo kuitaka IEBC kuboresha mfumo huo kwenye chaguzi zijazo.

Amesema kuwa wamebaini kuwepo kwa amani na utulivu kabla, wakati na baada ya kupiga kura.