Kilio cha mbolea ya ruzuku chashika kasi

Muktasari:

  • Serikali imetakiwa kutazama upya mfumo wa huduma za usambazaji wa mbolea ya ruzuku kwa wakulima nchini kutokana na changamoto lukuki, ikiwamo uhaba wa vituo.

Dar/mikoani. Serikali imetakiwa kutazama upya mfumo wa huduma za usambazaji wa mbolea ya ruzuku kwa wakulima nchini kutokana na changamoto lukuki, ikiwamo uhaba wa vituo.

Baadhi ya wakulima wanasema wananunua mbolea kwa bei kubwa hivyo hakuna maana ya ruzuku iliyotangazwa na Serikali.

Changamoto nyingine zilizoibuliwa ni kukosekana kwa taarifa za kutosha kuhusu bei pamoja na mfumo wa kutambua orodha ya wanufaika.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini changamoto hizo kujitokeza katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Dodoma, Geita, Mwanza na Tabora, ambako wakulima, mawakala, maofisa wa ugani, maofisa kilimo walikiri changamoto hizo na kushauri Serikali kuingilia kati, licha ya unafuu katika punguzo la bei za mbolea.

Hali hiyo inaakisi taarifa ya Wizara ya Kilimo inayoonyesha hadi Aprili, mwaka huu, tani 436,452 za mbolea zilikuwa zimepatikana, sawa na asilimia 63 ya mahitaji ya tani 698,260 ya msimu wa 2021/2022.

Aidha tani 34,391, zenye thamani ya Sh63 bilioni zilikuwa zimeshasambazwa katika vyama vya Ushirika.

Mkulima wa Mbarika, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Jasmini Yohana aliiomba Serikali kutatua changamoto ya kutumia gharama kubwa, huku Ofisa Kilimo wa wilaya hiyo, Sagire Samwel akikiri kutokuwa na wakala wa mbolea hivyo husafiri zaidi ya kilomita 70 kufuatilia mbolea hiyo.

Mkulima wa Bustani, Kata ya Nyaguge wilayani Magu mkoani humo, Renatus Mhangwa alisema wanalazimika kukaa muda mrefu kusubiri ujumbe mfupi wa simu (SMS) kujua iwapo wamechaguliwa kuchukua mbolea, jambo linalofanya baadhi yao kughairi kufuatilia mbolea hiyo kutokana na umbali wa maduka.

Alisema gunia lenye ujazo wa kilo 50 la mbolea ya kupandia (DAP) wilayani Magu linauzwa Sh60,000, huku ya kukuzia ikiuzwa Sh70,000, mkulima anaisafirisha hadi kijijini lilipo shamba lake.

Katika mji mdogo wa Katoro, Mkoa wa Geita baadhi ya wakulima wanaotumia duka la Yohana Zakaria walisema hukaa kwenye foleni kwa siku nzima kutokana na ukosefu wa mbolea ya ruzuku kwenye maeneo yao.

Numira Swalehe, mkazi wa Chato alisafiri hadi wilayani Geita kufuatilia mbolea ya ruzuku, hatua inayoongeza gharama za mbolea kupitia nauli na muda wa kufuatilia.

Elizabeth Masuka wa Kata ya Buseresere aliiomba Serikali kuongeza mawakala ili kupata mbolea hiyo kwa haraka, huku wakala wa mbolea hiyo wilaya ya Bukombe, Katoro, Muleba, Misenyi na Karagwe, Yohana Zacharia akidai udogo wa mtaji umeathiri kufikisha mbolea Muleba, Misenyi na Karagwe.

“Leo (jana) nimetoa mbolea kwa wakulima 200, changamoto wakulima ni wengi, ningeomba Serikali iongezee nguvu mawakala ili kufikia mahitaji ya wakulima,” alisema Zakaria.

Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Geita, Richard Kapyela alisema wilaya hiyo iliandikisha mawakala 11, lakini hadi sasa wenye mbolea ya ruzuku ni watatu pekee.

Alisema tayari halmashauri hiyo imeshaorodhesha maeneo ya vituo 34 vitakavyosogeza huduma za mbolea kwa wakulima.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dk Stephan Ngailo alisema wamesajili zaidi ya mawakala 2,500, lakini wengi wao hawatoi huduma hiyo kutokana na changamoto za kimitaji. “Hiyo ndiyo root course (msingi wa tatizo), lakini hatuna changamoto ya upatikanaji wa mbolea isipokuwa usambazaji, tayari tani 400,000 kati ya 600,000 zimeshaingia nchini, kesho tutatoa ripoti ya usambazaji na ufafanuzi wa taarifa nyingine pia tutaeleza,” alisema Dk Ngailo.

Dodoma na Mbeya

Mkulima kutoka kijiji cha Nondwa jijini Dodoma, Issa Shaban alisema hawajawahi kuiona mbolea ya ruzuku kutoka serikalini na hutumia mbolea ya asili, huku wakulima wa Kijiji cha Manzase wakitumia mbolea za kienyeji baada ya kata hiyo kutofikiwa na ruzuku ya mbolea.

Mfanyabiashara wa mbolea, Mariam Ramadhan, jijini hapo alisema hali ya upatikanaji wa mbolea sio rafiki, kwani bei yake imepanda ukilinganisha na awali. Alisema mbolea aina ya DAP mfuko mmoja unauzwa Sh 80,000 hadi 100,000 wakati mbolea ya Urea ilikuwa Sh50,000 hadi 70,000.

Mkoani Mbeya, wakulima walisema Serikali inafikisha pembejeo za kilimo kwa wakati, lakini changamoto ni namna ya kuwafikia na usambazaji unaosababisha kupanda holela huku wafanyabiashara wakishauri kuweka ushindani wa mawakala wa usambazaji pembejeo ili kwenda na wakati katika misimu ya kilimo.

Mkulima Witness Kamwela alisema uchache wa mawakala ni kikwazo kwao, akiomba msimu ujao wa kilimo kuweka ushindani utakaoleta tija katika sekta ya kilimo na wakulima kufikia malengo yao.

Akijibu hoja hiyo, wakala wa Pembejeo za kilimo mkoani hapo, Sadeni Mbwaga alisema changamoto ni mawakala wakubwa, kwani msimu huu wamepokea mifuko 7,000 na tayari imesambazwa kwa wakulima mashambani.

“Kwa msimu huu huenda pembejeo zisitoshe kwa sababu mwamko wa wakulima ni mkubwa sambamba na kushuka kwa bei kutoka Sh140,000 mpaka Sh70,000 kwa mfuko mmoja wa mbolea,” alisema.

Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Nyanda za juu kusini, Michael Sanga alisema mpaka sasa mbolea iliyoingizwa inajitosheleza na hakuna maeneo ambayo kuna malalamiko.


Kicheko kwa wengine

Hali ni tofauti mkoani Tabora, baada ya wakulima wa Manispaa ya Tabora waliodai wanapata mbolea hiyo bila changamoto, wakisema namba ya siri waliyotumiwa kwa ujumbe mfupi baada ya kujiandikisha imewasaidia kwa kuwa wakifika kwa wakala wanamuonyesha na kupewa mbolea.

Mkoani Iringa, Azeria Mbwambo, mkulima Skimu ya Luganga Tarafa ya Pawaga alisema wakulima wa mpunga wilayani Iringa wanatarajiwa kuongeza uzalishaji kwa asilimia zaidi ya 50 baada ya kuongeza eneo la uzalishaji, huku Serikali ikishusha bei ya mbolea, hatua inayopunguza gharama za uzalishaji.

Ofisa ugani wa kampuni ya usindikaji mazao ya kilimo ya Ruaha Milling, Zacharia Luvanga alisema punguzo la bei za mbolea limeongeza matumaini ya kampuni ya usindikaji mazao ya kilimo kupata uhakika wa malighafi ya kutosha kutokana na uhakika wa mbolea kwa wakulima hao.

Wakala wa mbolea wa Kampuni ya Ayubu Trading Company mkoani hapo, Clement Ng’ong’osi alisema usambazaji wa mbolea kwa wakulima mkoani hapo umefanyika na ziada kubakia.

Katika kampuni hiyo aliuza zaidi ya mifuko 700 ya mbolea kwa wakulima wa kata nzima ya Ihanga iliyopo Halmashauri ya mji wa Njombe. “Walihudumiwa mpaka mwisho na wakulima walitosheka na Ihanga katani walibakiza na ikapelekwa kijiji cha Iboya kilichopo kwenye kata hiyo,” alisema Clement.

Ripoti hii imeandaliwa na Kelvin Matandiko (Dar), Hawa Mathias (Mbeya), Berdina Majinge (Iringa), Seif Jumanne (Njombe), Mainda Mhando (Dodoma), Rehema Matowo (Geita), Saada Amir na Mgongo Kaitira (Mwanza) na Robert Kakwesi (Tabora),