Kilio cha walalahoi na bei ya dagaa ikipaa

Muktasari:

  • Bei ya dagaa, kitoweo kimbilio la watu wengi nchini, imepanda katika mikoa mbalimbali nchini kwa wastani wa Sh2,000 hadi Sh15,000 kutegemeana na kipimo au uzito kwa wauzaji na wanunuzi wa jumla.


Mikoani. Bei ya dagaa, kitoweo kimbilio la watu wengi nchini, imepanda katika mikoa mbalimbali nchini kwa wastani wa Sh2,000 hadi Sh15,000 kutegemeana na kipimo au uzito kwa wauzaji na wanunuzi wa jumla.

Huo ni mwendelezo wa kupanda bei kwa bidhaa mbalimbali za vyakula na nyinginezo, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika mikoa ya Mwanza, Mbeya, Ruvuma, Kilimanjaro, Dodoma, Kigoma na Dar es Salaam.

Ili kuendelea kushawishi wateja, wauzaji wa rejareja wa dagaa wamepunguza ujazo wa mafungu ili kusalia na bei inayofikiwa na watu wengi.

Katika kudhibiti usafirishaji holela wa dagaa unaoweza kusababisha ziadimike, Ofisa Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Bernard Semwaiko alisema ofisi yake kwa kushirikiana na taasisi na mamlaka nyingine za Serikali, imeimarisha doria ndani ya Ziwa Nyasa kukabiliana na tishio la uvuvi haramu unaoweza kusababishwa na mahitaji makubwa sokoni ya samaki na dagaa wakati vitoweo hivyo vimeadimika ziwani.

Sababu za bei kupaa

“Kupanda kwa bei ya dagaa kunatokana na mabadiliko ya hali ya hewa, baridi na upepo unaovuma unaosababisha dagaa kuadimika,” alisema Muzamiru Juma, muuza dagaa katika Soko la Temeke Stereo, jijini Dar es Salaam.

Mfanyabiashara mwingine, Mahamod Mtabi alisema hali ya baridi ziwani na baharini inasababisha dagaa kukimbilia maeneo ya mbali yenye joto na kusababisha kitoweo hicho kuadimika na bei kupaa sokoni.

Lakini Jackson Pascal, mkazi wa Kigoma Ujiji alisema dagaa wameadimika kwa sababu huu si msimu wake, hasa katika Ziwa Tanganyika ambako dagaa wengi wanatarajiwa kuanza kupatikana kuanzia mwezi Agosti.

Sababu nyingine ya dagaa kuadimika ni kuhitajika kwake katika nchi mbalimbali, wachache wanaopatikana wanagombewa na wafanyabiashara, kwa mujibu wa Jumanne Chabhaba, muuzaji wa kitoweo hicho mjini Dodoma.

Vilevile, vyombo vya uvuvi kuwa duni na wavuvi kutumia teknolojia ya zamani kumechangia hali hiyo.

Lakini Msemaji Chama cha Wavuvi Tanzania (Tafu), Karoli Sijaona yeye alisema kupanda kwa gharama za maisha kumesababisha wananchi kugeukia dagaa kutokana na kushindwa kumudu bei ya vitoweo vingine kama samaki, nyama na kuku.

Hata hivyo, Sijaona alisema “licha ya kupanda bei sokoni, dagaa bado ni nafuu kwa wananchi wenye kipato cha chini kulinganisha na nyama, kuku na samaki.”

Wakati Tafu ikitaja gharama za maisha za ongezeko, Dotto Sosi, mvuvi wa dagaa kutoka Kijiji cha Chibasi Kisiwa cha Ukara mkoani Mwanza alisema mahitaji ya dagaa kwenye soko la ndani na nje yameongezeka, huku uzalishaji ukiwa mdogo na kuwa sababu za bei yake kupanda.

Alipotafutwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema huwezi kuzuia soko la nje kwa kuwa kwa kuwa kila mvuvi anauza dagaa pale anapoona pana soko na ukilizuia litaleta mgogoro na wavuvi.

Alisema mkakati wa Serikali ni kuangalia namna ya kuongeza uzalishaji kwa kutumia uvuvi wa kisasa.


Hali ilivyo sokoni

Mfanyabiashara wa dagaa katika eneo maarufu la Relini pembezoni mwa Ziwa Victoria jijini Mwanza, Malice John alisema kisado cha dagaa zilizokaangwa kilichokuwa kinauzwa kati ya Sh14,000 hadi Sh15,000 hivi sasa kinauzwa kati ya Sh17, 000 hadi Sh18,000.

“Ndoo kubwa yenye ujazo wa lita 20 ya dagaa wabichi awali iliuzwa Sh35,000, sasa imepanda hadi Sh45,000 na wakati mwingine hufika hata Sh50,000 kutegemeana na upatikanaji wake,” alisema Malice.

Katika Soko la Iloganzara eneo la Sabasaba wilayani Ilemela, mfanyabiashara Leokardia Magesa alisema ndoo yenye ujazo wa lita 10 ya dagaa wakavu maarufu kama kauzu iliyokuwa ikiuzwa Sh10,000 imepanda hadi Sh12,000, huku kisado kilichouzwa Sh3,000 awali sasa kimefikia Sh5,000.

Hali ni hiyohiyo wilayani Ukerewe, ambako shughuli kuu ya kiuchumi ni uvuvi, kwa kuwa nao wanalazimika kufungua pochi zaidi wanapohitaji dagaa.

Bei yake kisiwani humo imepanda kutoka kati ya Sh2,500 hadi Sh3,000 kwa kisado, ndoo kubwa ya dagaa wakavu imetoka kati ya Sh10,000 na Sh15,000 hadi kati ya Sh25,000 na Sh30 000.

Vivyo hivyo katika Kisiwa cha Ukara gunia moja la ndoo tisa hadi 10 za dagaa ambalo awali liliuzwa kati ya Sh100,000 na Sh150,000 sasa limepanda maradufu hadi Sh300,000.

Mkoani Kilimanjaro, Happiness Shayo, mkazi wa manispaa ya Moshi alisema dagaa kauzu wamepanda bei hadi Sh10,000 kwa kisado kutoka Sh7,000 za awali, huku dagaa nyama kutoka Zanzibar waliokuwa wakiuzwa Sh8,000 kwa kilo sasa ni Sh12,000.

“Dagaa waliokaangwa kutoka Mwanza hivi sasa ni Sh15,000 kwa kilo tofauti na Sh10,000 za awali,” alisema Hapinness.

Hali ni hivyohivyo mkoani Mbeya, ambako Janeth Mwakalukwa wa Soko la Soweto alisema kopo la ujazo wa lita moja la dagaa wakavu lililokuwa linauzwa Sh2,000 sasa limefikia Sh3,000.

Ruvuma nako, Peter Sumuni, mwenyekiti wa Ushirika wa Wavuvi Mbambabay alisema dagaa walianza kuadimika kuanzia Mei ambapo sado moja ya kitoweo hicho ilipanda kutoka Sh3,500 hadi Sh8,000 kabla ya kufikia Sh17,000 mwezi huu.

Kwa mkoa wa Kigoma dagaa aina ya kauzu, wadogo na wenye ubora hafifu, sasa wanauzwa Sh18,000 hadi Sh20,000 kwa kilo kutoka bei ya awali ya Sh10,000 hadi Sh14,000 kwa kilo.

Wale dagaa wakubwa kutoka Ziwa Tanganyika, karumba, awali waliuzwa kati ya Sh15,000 hadi Sh20,000 kwa kilo, sasa wamefikia Sh35,000 hadi Sh37,000 kwa kilo.

Hali ni mbaya zaidi kwa mikoa ambayo haizalishi dagaa kama mkoa wa Dodoma ambako wakazi wanalazimika kununua kilo moja ya dagaa wa Mwanza kwa Sh7,000 au Sh8,000 kulinganisha na bei ya awali ya Sh5,000 hadi Sh6,000.

Mkoani Dodoma, dagaa aina ya karumba kutoka Kigoma wamepanda kutoka Sh30,000 hadi Sh60,000 kwa kilo na sababu ikitajwa ni ugumu wa upatikanaji unaotokana na hali ya hewa.Muuzaji wa dagaa katika soko kuu la Majengo jijini Dodoma, Jumanne Chabhaba alisema hivi sasa wananunua karumba kwa Sh45,000 kwa kilo kutoka Kigoma na kuiuza kwa Sh60,000.

Alisema dagaa hao wana soko katika nchi nyingi na yeye ana oda ya kupeleka kilo zisizopungua 50 kila mwezi Afrika Kusini, lakini anazipata kwa shida.

Jijini Dar es Salaam katika Soko la Temeke Stereo kilo ya dagaa inauzwa Sh8,500 kulinganisha na bei ya awali ya Sh5,000, sababu ikielezwa kuwa ni ongezeko la baridi na upepo mkali unaosababisha kitoweo hicho kuadimika, hakli ambayo haina tofauti sana na jijini Arusha.

“Hali ilikuwa mbaya zaidi wiki mbili zilizopita ambapo kilo ya dagaa iliuzwa hadi Sh12,000,” alisema Muzamiru Juma wa Soko la Stereo.

Dagaa wa Zanzibar maarufu kama dagaa nyama nao hawakuachwa, bei yake imepanda hadi Sh12,000 kutoka bei ya awali ya Sh7,000 kwa kilo.

Hali iko vivyo hivyo katika Soko la Buguruni Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam ambako kilo ya dagaa inauzwa kati ya Sh10,000 hadi Sh12,000 kutegemeana na ubora.

Pia katika Soko la Feri, Dar es Salaam kupanda ambako Shaibu Juma alisema bei ilifika kati ya Sh90,000 hadi Sh100, 000 kulinganisha na iliyozoeleka sokoni hapo ya Sh60,000 kwa ndoo moja yenye ujazo wa lita 20.

Imeandikwa na Joyce Joliga (Songea), Hawa Mathias (Mbeya), Damian Masyenene (Mwanza), Ramadhan Hassan (Dodoma) na Happiness Tesha (Kigoma), Fortune Francis, Jackson Ngowo, Happiness Samson (Dar) na Mussa Juma, Arusha.