Kilio cha Watanzania kimetoka kwenye demokrasia hadi tozo

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba

Muktasari:

  • Machi 19, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia ofisini akiwa ni Mkuu wa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nchi ilikuwa inahitaji hewa safi. Demokrasia ilikuwa changamoto.

Machi 19, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia ofisini akiwa ni Mkuu wa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nchi ilikuwa inahitaji hewa safi. Demokrasia ilikuwa changamoto.

Mwaka mmoja na zaidi ya miezi mitano baadaye, taifa halilii tena kilio cha demokrasia. Inawezekana wananchi hawakumbuki tena maumivu yaliyokuwepo ya ukosefu wa uhuru na demokrasia kuminywa. Wanahitaji hewa nyingine mpya.

Tozo ndio kilio kipya kwa sasa. Jumlisha ugumu wa maisha na ufinyu wa kipato. Hapohapo kuna kumbukumbu ya kauli ya Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kuwa asiyetaka tozo aende Burundi.

Tafsiri ya Mwigulu ni kuwa tayari “wao wenye mamlaka wameamua, ambaye hakubaliani na tozo aache kuwa Mtanzania akawe raia wa Burundi”. Je, ni kiburi au dharau? Umepewa dhamana ya kuwaendeshea watu nchi yao, halafu unawaambia waliokudhamini wabadili uraia.

Kutoka kauli ya Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela, kipindi akiwa Waziri wa Uchukuzi, akiwajibu waliolalamikia kuzorota kwa usafiri wa treni kuwa “waende kuzimu”, kisha aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, akasema “wananchi wale nyasi” ili ndege ya Rais inunuliwe.

Ikaibuka kauli ya wasiotaka kulipa Sh200 ya kivuko cha Kigamboni wapige mbizi kutoka kwa Rais wa Tano, John Magufuli, wakati akiwa Waziri wa Ujenzi, na nyingine zenye kuwakosea staha wananchi, Mwigulu naye amekuja na yake.

Kama kauli ya “waende kuzimu” ilivyomkera Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ndivyo na “waende Burundi”, ingemuumiza. Alitaka na alijitahidi kujenga nchi yenye misingi ya viongozi kuwaheshimu wananchi.

Tuendelee na mada yetu; tozo zimekuwa wimbo kwenye mitandao ya simu mpaka benki. Inavyoonekana, Wizara ya Fedha imekosa mbinu za kubuni vyanzo vipya vya mapato, inaamua kumkamua mwananchi kwa kidogo alichonacho.

Waziri Mwigulu alipokuwa anasoma bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022-2023, alisema tozo za miamala ya simu zimepungua kwa kiasi kikubwa. Hali ya sasa ni kwamba zimepunguzwa kidogo kwenye simu na kuongezwa zaidi benki.

Makato mengi ya fedha kwenye miamala ya simu na benki, yanaweza kuchagiza watu kuwa na fikra za kijima. Watanzania wataona bora wahifadhi pesa zao ndani kuliko kwenye simu ambako kila thumni wanayotumia imejaa makato. Benki wanakata ada za miamala, Serikali nayo inatoza.

Dunia ilishahama. Maisha ya mobile money na sim-banking, yalishatengeneza tabaka kubwa la wasiotembea na fedha. Huduma za malipo kwa simu zilikuwa zinaongezeka. Haya ni mapinduzi makubwa ya kiteknokojia ambayo Serikali inapaswa kuyakumbatia.

Namna pekee kwa Serikali kuwezesha jambo kufanyika au kukua ni kulitengeneza kuwa rahisi. Mwananchi anapaswa kuona kubeba fedha taslimu ni gharama kuliko kuziweka benki au kuhifadhi kwenye akaunti za simu katika huduma za kifedha.

Miaka 20 kurudi nyuma, Tanzania kulikuwa na matukio mengi ya majambazi kuvamia nyumba za watu usiku na kupora fedha. Maduka na kadhalika. Ulimwengu wa sasa, hakuna mtu anayeweka pesa ndani. Teknolojia imerahisisha.

Siku hizi matukio ya majambazi kuvamia nyumba za watu sio mengi. Ni kwa sababu ni vigumu kumkuta mtu na pesa nyingi chumbani. Si kwamba Jeshi la Polisi limekuwa na ufanisi kuliko zamani. Tabia za watu zimebadilika.

Historia inaonesha kuwa fursa ya ujambazi huchagiza matukio mengi hata pale vyombo vya usalama vinapokuwa macho kiasi gani. Kipindi cha nyuma, utekaji wa vyombo vya usafiri ulikuwa mkubwa sana, siku hizi umepungua. Si ufanisi wa kijeshi pekee, ni mabadiliko ya tabia. Wananchi hawasafiri na pesa. Teknolojia imerahisisha.

Serikali inapaswa kukumbuka mahali nchi ilipotoka. Zama za wananchi kulala roho mkononi na abiria kusafiri wakiwa na hofu kubwa ya kuvamiwa na kutekwa, kisha kupukutishwa fedha. Na izingatiwe kuwa dawa kubwa ya kudhibiti matukio ya uvamizi nyumbani na vyombo vya usafiri ni watu kuachana na maisha ya fedha taslimu.

Ripoti ya mwaka 2021 ya Kituo cha Taifa cha Takwimu za Matumizi Mabaya ya Dawa nchini Marekani (NCDAS), inaeleza kuwa Wamarekani milioni 32 wanatumia dawa za kukevya. Idadi hiyo ni zaidi ya nusu ya Watanzania wote. Hii ni kulingana na makadirio ya watu milioni 60 ambao inadhaniwa Tanzania ipo nao kabla ya Sensa 2022.

Pitia idadi ya watu milioni 32 wanaotumia dawa za kulevya, soma ulinzi mkali uliopo Marekani. Jibu unalo kwamba uimara wa kijeshi unasaidia lakini mabadiliko ya tabia ni muhimu mno katika kutokomeza uhalifu.

Fursa za uhalifu zikiwepo nyingi, jinsi unavyoongeza uimara na maarifa ya kijeshi, ndivyo na wahalifu wanavyobadili mbinu ili kufanikisha mipango yao. Hicho ndicho kinaendelea Marekani.

Serikali ya Marekani ina ulinzi mipakani kuliko nchi yoyote duniani. Bandari zake na viwanja vya ndege vinalindwa kwa teknolojia ya hali ya juu. Serikali ya Marekani pia hufadhili majeshi ya Mexico, Colombia na nchi nyingine jirani ili ziwe imara kupambana na dawa za kulevya.

Pamoja na uwekezaji wote huo, Ofisi ya Dawa na Uhalifu ya Umoja wa Mataifa, inaitaja Marekani kuwa taifa linaloingiza dawa za kulevya kwa wingi kuliko nchi yoyote duniani. Asilimia 30 ya dawa za kulevya zinazopatikana duniani, huuzwa Marekani peke yake.

Mfano wa dawa za kulevya na Marekani ni kutoa angalizo kuwa kama wananchi wataona hasara kuhifadhi pesa benki, maana yake wataziweka ndani ya nyumba zao. Na uhalifu wa kuvunja milango na mageti usiku utaongezeka hata kama polisi watakuwa imara kiasi gani.

Huoni sasa hivi vibaka hawaishi? Wezi wa mitandaoni wanakamatwa na wengine wanachipua upya. Thamani ya uhalifu wa mitandao unapanda ngazi kutoka mamilioni mpaka mabilioni. Polisi wapo, mamlaka zipo, sheria zinafanya kazi, tatizo fursa ya uhalifu mtandaoni ni mkubwa. Wizi unaendelea.


Tafakari na hili

Agosti 25, 2022, Taasisi ya Utafiti ya Twaweza, ilichapisha ripoti yake ya “Uchumi na Tozo”. Imeonesha kuwa asilimia 70 ya wakazi wa Dar es Salaam wamepunguza matumizi ya fedha kwa simu.

Kwa mwendo huo, maana yake kuna athari kubwa ya kupungua kwa uchumi wa simu za mkononi. Mwisho kabisa hata Serikali itashindwa kupata kodi ambayo ingepata kama kusingekuwa na tozo.

Awali, kulikuwa na makadirio ya Serikali kukusanya Sh1.25 trilioni kutokana na tozo. Serikali ikapata Sh360 bilioni. Hicho ni kipimo kuwa wananchi walipunguza kutumia njia ya simu kutuma au kupokea fedha.

Mwendo huo unakwenda kuathiri kampuni za simu ambazo kwa miaka ya karibuni, mapato yao mengi yamekuwa yakitegemea huduma za kifedha. Kuathirika kwao, kunadumaza uchumi, na Serikali itakosa kodi.

Kama athari za uchumi zimeshaanza kuzitesa kampuni za simu, maana yake benki nazo safari ipo njiani. Watakumbwa na anguko baada ya wananchi kuamua kubadili tabia ya utunzaji wa fedha.

Benki zinahitaji watu waweke fedha ili wazifanyie biashara. Ghafla nusu ya wateja wa benki waamue kutunza fedha nyumbani, maana yake sio tu mapato yatashuka kwa nusu nzima, bali pia hata operesheni za kibenki zitapungua.

Lipo pia suala la bando. Waziri wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano, Nape Nnauye, amekuwa akijibu kuwa bando ni nafuu. Hata hivyo, wananchi wanalalamika. Inawezekana maumivu ya bando ni makubwa kuliko tozo za simu na benki.

Mtu ambaye mwaka jana alikuwa ananunua bando la wiki anatumia siku saba, siku hizi ananunua bando la wiki na kutumia siku moja. Bando la mwezi linaisha ndani ya wiki. Hali si nzuri kabisa.

Haya ni mambo ambayo yanawatesa mno wananchi. Hawaoni unafuu. Mawaziri hawazungumzi nafuu. Lugha yao haitoi matumaini kwamba kuna nyota njema itaonekana.

Kilio cha wananchi kuhusu bando za intaneti, kitasababisha kupungua kwa matumizi. Wapo watakaoona si muhimu, wengine watashindwa kumudu, juu ya hayo yote, ununuzi wa bando utashuka kwa kila mtandao. Mapato ya kampuni yatapungua na Serikali itakosa kodi.


Tozo na ustawi

Ripoti ya Twaweza imeonesha kuwa kilio cha Watanzania hadi asilimia 56 ni ugumu wa maisha. Na maombi yao ni Rais Samia kushusha gharama za maisha. Hili ni la kutazamwa kwa macho yote mawili.

Serikali ina wajibu wa kuweka mazingira yasiyomuumiza mwananchi katika ukusanyaji wa mapato yake. Mshahara wa mfanyakazi wenye makato mengi ya kodi na michango mbalimbali, kuutumia tena benki, Serikali inataka itoze.

Yaani fedha ambazo Serikali imeshazitoza kodi, inazifuata na benki kuzitoza tozo. Je, wakati wataalamu wanaketi na kufanya uamuzi huu, walifikiria kuwa ustawi wa mwananchi ni muhimu katika kukuza uchumi?

Moja ya nadharia za uchumi wa soko ni kumfanya mtu awe na pesa halafu muwekee huduma ambazo atavutiwa kuzitumia, ili pesa yake itumike, ifanye mzunguko wa kifedha kuwa mkubwa. Hivyo ndivyo na uchumi wa nchi utakua.

Tatizo linakuja, mwananchi anabanwa kwenye thumni yake anayopata. Anapata woga. Serikali inaweza kuchekelea kukusanya tozo, kisha inaharibu mzunguko wa kifedha mtaani.

Kipindi cha uongozi wa Rais John Magufuli, uchumi wa benki ulidorora mno kwa sababu ya mzunguko wa kifedha mtaani kudumaa. Kuna shaka tozo nyingi za miamala zikashusha operesheni za benki.

Rais Samia alimwambia Waziri wa Fedha aje na vyanzo vipya vya mapato na sio kuwabana wafanyabiashara. Hiki chanzo cha tozo sio kizuri. Maana kimekuwa maumivu makali kwa mwananchi anayeishi katika mazingira magumu.

Kuongeza mapato ni kutanua fursa za biashara. Nchi iwe na wafanyabiashara wengi na ajira ziwe nyingi. Mzunguko wa fedha unapokuwa mzuri, mapato lazima yaongezeke. Sio kuitamani Sh50,000 ya bodaboda aliyoiweka benki, kwamba akitaka kuitoa au kuituma, itozwe kodi kwa jina la tozo.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Brazil ilipokumbwa na dhoruba ya uchumi na mfumuko wa bei hadi asilimia 2,400, Rais Itamar Franco alifanya kazi na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Fernando Henrique Cardoso ‘FHC’ yenye msingi mkubwa wa kufanya mageuzi ya kiuchumi na kuwapa nafuu wananchi.

Marekani ilipokuwa inapitia mdororo mkubwa wa kiuchumi kati ya mwaka 1929 mpaka 1939, Rais Franklin Delano Roosevelt, alitambulisha kanuni aliyoiita “R tatu”. R ya kwanza kabisa ilikuwa “Relief” – “Unafuu”. Kwamba mwanzo wa kila kitu, mwananchi lazima aone maisha ni nafuu.

Kipindi hiki mwananchi anashuhudia kupanda kwa bei za bidhaa. Mafuta yamepaa. Gharama za huduma hazishikiki. Kipato hakiongezeki na pengine kimepungua. Halafu anakutana tozo nyingi kwenye fedha zake. Maumivu yaliyoje? Hana budi kuhitaji hewa safi ambayo ni unafuu wa maisha yake.

R ya pili ni “Recovery” – “Uhuishaji”. Lengo lilikuwa kuhuisha uchumi mpaka kufikia kiwango cha kawaida. R ya tatu ikawa “Reform” – “Mageuzi”. Yaani kufanya mageuzi ya mfumo wa kifedha na kudhibiti kutojirudia kwa msukosuko wa uchumi wa viwanda. Bado tunabaki palepale, R ya kwanza ililenga nafuu kwa wananchi.

Kipindi hiki mwananchi anashuhudia kupanda kwa bei za bidhaa. Mafuta yamepaa. Gharama za huduma hazishikiki. Kipato hakiongezeki na pengine kimepungua. Halafu anakutana tozo nyingi kwenye fedha zake. Maumivu yaliyoje? Hana budi kuhitaji hewa safi ambayo ni unafuu wa maisha yake.