Kilio miundombinu mibovu soko la kimataifa Holili
Soko la nafaka Holili lililopo mpakani mwa Kenya na Tanzania wilayani Rombo ambapo wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi wamekuwa wakiuza bidhaa katika eneo hilo la soko licha ya kutokuwepo kwa miundombinu rafiki. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Wafanyabiashara wa nafaka katika soko la Kimataifa la Holili, ambalo lipo mpakani mwa Kenya na Tanzania, wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro wameiomba serikali kuwaboreshea miundo mbinu ya soko hilo kutokana na ubovu wa miundo mbinu iliyopo.
Rombo. Wafanyabiashara wa nafaka katika soko la Kimataifa la Holili, ambalo lipo mpakani mwa Kenya na Tanzania, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro wameiomba Serikali kuwaboreshea miundombinu ya soko hilo kutokana na ubovu uliopo.
Wamesema ubovu huo wa miundombinu ya soko inadumaza juhudi zao za kujikwamua kiuchumi na kwamba ni soko ambalo wamekuwa wakilitegemea kuuzia bidhaa zao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanya biashara hao, wamesema tangu soko hilo lijengwe limekuwa na changamoto nyingi ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, eneo maalum la kuuzia bidhaa na kuhifadhi nafaka.
Emmyglory Marandu, mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo, amesema soko hilo licha ya kwamba ni soko linalotumiwa na watu kutoka Mataifa mbalimbali halina sehemu maalumu ya kuhifadhia nafaka na wakati mwingine mvua zinavyonyesha hunyeshea bidhaa zao na kuwapa hasara.
"Miundo mbinu katika soko letu haijakaa vizuri tunaomba serikali iangalie kwa jicho la pili ili wafanyabiashara waweze kufanya shughuli vizuri maana hakuna sehemu sahihi ya kuweka mizigo na wakati mwingine mizigo inawekwa chini hali ambayo sio salama kwa afya,”amesema.
Mfanyabiashara mwingine wa soko hilo, Ramadhan Msabaha amesema wakati wa kipindi cha mvua wamekuwa wakitabika kwasababu hawana mahali pakuhifadhia nafaka zao na hivyo kuharibika kwa kunyeshewa na mvua.
"Soko hili tangu lianze kujengwa ni kama limetelekezwa na limeharibika miundombinu yake, maana halijawekwa sakafu hadi sasa, tunapoweka nafaka zetu hususani mahindi yanaharibika hasa wakati wa msimu wa mvua, hatuna pa kuyahifadhi, hali inakuwa sio nzuri kwenye biashara zetu,"
"Tunaomba serikali ituwekee miundo mbinu mizuri maana fedha zipo kwani tunatoa kodi na ushuru kwenye hili soko ili biashara zetu ziweze kufanyika vizuri,"
Diwani wa kata ya Holili, Kelvin Constantine amesema kwa kuwa soko hilo linaingiza fedha nyingi kwa Serikali ni wakati muafaka sasa wa soko hilo kuboreshwa na kujengwa soko la kisasa.
"Tunahitaji soko hili liboreshwe, maana lina tatizo kubwa la miundo mbinu, tunajua soko hili linawaletea halmshauri fedha nyingi hivyo ni lazima liboreshwe ili watu waweze kulipenda na waje kufanya biashara hapa,"
Kufuatia changamoto hizo, Mbunge wa Rombo ambaye ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema ndani ya wiki moja watahamasisha wadau ambao ni watumiaji wa soko hilo kuona namna ya kupata uongozi wa soko hilo ambao ndio changamoto kubwa inayoonekana katika soko hilo.
"Changamoto nyingi tulizoziona ni za kiutendaji lakini nyingine ni miundo mbinu ya soko letu wenyewe kwamba haitoshi, mfumo wa kitaasisi sio mzuri maana soko lenyewe halina uongozi, kwa hiyo tumezungumza kwamba kutakuwa na uhamasishaji wa wiki moja wa kuchagua viongozi wa soko ili mwisho wa mwezi huu wa kumi ningependa kuona kuna uongozi wa kuwasiliana nao mara kwa mara kukiwa na changamoto,"
"Tunachohitaji ni kuona soko hili la Kimataifa linauza matunda na mbogamboga lakini soko hili liwe kituo kikubwa cha kuhifadhia nafaka zaidi kusafirisha nje ya nchi, na maelekezo ya Rais wetu ni kwamba tuweke mazingira mepesi katika ufanyaji wa biashara,"
Naye, Mkuu wa wilaya ya Rombo, Kanali Hamis Maiga amesema kama Serikali watajitahidi kutatua changamoto ya soko hilo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
"Changamoto hizi tumezipokea na kama serikali tunaahidi kutatua changamoto hizi kwa muda na kwa ubora wanaohitaji hawa wafanyabishara,"amesema DC Maiga.