Kongamano la uchumi wa buluu Novemba 8

Muktasari:

Kongamano kubwa la uchumi wa bluu litakalowakutanisha wataalamu wa mazao ya bahari kutoka visiwa vya shelisheli na nchini Tanzania linatarajiwa kufanyika Novemba 8 mwaka huu visiwani Zanzibar.

Dar es Salaam. Watanzania wanaotegemea mazao mbalimbali ya bahari wanatarajiwa kunufaika na kongamano kubwa la uchumi wa buluu lililolenga kuwakutanisha pamoja na wataalamu kutoka visiwa vya Shelisheli kujadili kwa pamoja fursa zilizopo.

Kongamano hilo litakalofanyika visiwani Zanzibar Novemba 8, 2022 limelenga kuwapa fursa zaidi vijana na kusaidia vikundi mbalimbali vya wajasiriamali vilivyojiunga pamoja kupitia Taasisi ya Pan African Leadership and Enterpreneurship development center (Paledec).

Hayo yamesemwa leo Jumatano, Novemba 2, 2022 na Balozi kutoka visiwa vya Shelisheli nchini Tanzania, Maryvonne Pool alipokuwa akielezea kongamano hilo kwa vyombo vya habari.

Balozi Maryvonne ambaye ni mwenyekiti wa taasisi ya Paledec, amesema Shelisheli ni kisiwa kinachotegemea uchumi wa bluu na kila mwaka wamekuwa wakifanya makongamano ambayo hugeuka chachu na fursa kwa wajasiriamali.

“Shelisheli tupo katika uchumi wa bluu, Januari mwaka huu taasisi waliniomba kuwa mwenyekiti wao kila mwaka tunafanya kongamano na programu huchagua eneo la kwenda kusaidia uwekezaji katika uchumi wa bluu na mwaka huu tumechagua kufanya kongamano nchini Tanzania visiwani Zanzibar,” amesema.

Amesema kongamano hilo litahudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka visiwani Shelisheli na nchi mbalimbali kujadili kwa pamoja fursa zilizopo Zanzibar na kuangalia namna ya kusaidia wakulima hasa wa zao la mwani.

“Tutafanya mjadala wa pamoja na kuongea na Serikali tunataka kuangalia maeneo gani ya kusaidia, tumeangalia zaidi ni maeneo yapi ya kuyagusia na kikubwa ni namna ya kuboresha miradi iliyopo na kutoa mbinu sahihi nini kifanyike kuboresha kilimo, masoko na kuangalia namna ya kuwawezesha wakulima kuyafikia masoko ya kimataifa,” amesema Maryvonne.